Serikali mkoani Tabora imeiagiza kampuni ya Voedsel inayojihusisha na ununuzi wa zao la tumbaku mkoani hapa kulipata deni la wakulima kiasi cha sh bil 20 ndani ya siku 7.
Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Burian alipokutana na viongozi wa kampuni hiyo ofisini kwake baada yakupokea malalamiko ya wakulima wa tumbaku juu ya ucheleweshwaji malipo yao ya msimu huu.
Balozi Dkt. Batilda amesema serikali haipo tayari kuona mkulima akinyanyasika wakati ametumia nguvu na gharama kubwa kuandaa shamba lake halafu mnunuzi amcheleweshee malipo.
Amesisitiza kuwa maelekezo ya serikali kwa msimu huu wa masoko kila mkulima alipwe chake ndani ya saa 48 baada ya kuuza lakini kampuni hiyo imekaa na pesa zao kwa zaidi ya siku 40 kinyume na makubaliano.
‘Sisi hatulichukulii hili kama deni bali ni wizi wa kuaminika maana Rais alitaka wakulima walipwe ndani ya siku 2 na vyama vingine vimelipa, hatuta waruhusu kuendelea kununua mpaka mlipe madeni yenu yote,’ amesema.
Meneja wa Bodi ya Tumbaku Kanda ya Magharibi Albert Charles amesema bodi yake imeondoa kampuni hiyo kwenye ratiba ya masoko mpaka itakapokamilisha ulipaji madeni ya wakulima.
Naye Meneja wa kampuni hiyo Mkoani hapa Victor Matawa alimhakikishia Mkuu wa mkoa kuwa wataanzaa kulipa madeni yote ya wakulima kuanzia wiki ijayo.
Amebainisha kuwa mchakato wa kuwalipa utaanza mara moja baada ya kukamilisha kwa mchakato wa hela zao kutoka benki ya CRDB.
Hadi sasa kampuni hiyo imeshalipa dola mil 1 kati ya dola mil 8 wanazodaiwa na vyama vya ushirika vya wakulima wa union za WETCU na Milambo.