Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahamed Abbas Ahamed amesema kuwa mkoa huo unakabiliwa na changamoto ya watoto wanaoishi na kufanyakazi za mitaani hususani katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea jambo ambalo linapelekea kuwa katika mazingira hatarishi ya uporaji na matumizi ya dawa za kulevya.
Hayo ameyasema jana kwenye kikao cha utambulisho wa uanzishwaji wa Mradi wa Dawati la Usatwi wa Jamii (SWSD) katika stendi kuu ya mabasi ya Manispaa ya Songea kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea.

Alisema kuwa changamoto hii husababisha watoto hao kujifunza na kujiingiza katika tabia hatarishi zaidi na wakati mwingine wanaweza kutumwa na watu wazima katika matukio ya wizi,uporaji, biashara za ngono,ulevi na matumizi ya madawa ya kulevya.
” Hali ilivyo kuwa katika Manispaa ya Songea kuna ongezeko la watoto wanaotumiwa katika uuzaji wa bidhaa kama vifungashio katika maeneo ya masoko,kuuza karanga, mayai na korosho hali hii hufanya watoto wengi kuwa katika hatari ya kufanyiwa vitendo vya ukatili na hivyo kuhatarisha ustawi wao.” Alisema Kanali Ahamed.
Kanali Ahamed ameeleza kuwa uanzishwaji wa Dawati la Usatwi wa Jamii katika stendi ya mabasi ni hatua moja wapo itakayosaidia katika kuwabaini watoto mapema mara tu wanaposhuka na mabasi lakini pia kuzuia kuingia mitaani na kuweza kubaini mahitaji na changamoto zao.
” Nimeelezwa kuwa mradi huu utafanya kazi katika stendi ya mabasi ya manispaa ya Songea hadi 2026 hivyo ni wajibu wetu sote kuhakikisha huduma zitakazotolewa kupitia mradi zinakuwa endelevu ili kufikia adhima hiyo” alisema.
Hata hivyo amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kutenga chumba maalumu katika miundombinu ya stendi kuu ya mabasi kitakachotumika kama ofisi ya dawati la ustawi wa Jamii na ateuwe Afisa ustawi wa Jamii na kumpatia majukumu ya kuwa mratibu wa dawati la ustawi stendi atakayekuwa anafanya kazi na kusimamia dawati hilo.

Pia amemtaka Mkurugenzi kuteua kamati ya uendeshaji wa Dawati la Ustawi stendi kwa mujibu wa mwongozo,kutoa elimu ndani na nje ya stend juu ya uwepo wa dawati hilo na majukumu yake,kuwepo na ushirikishwaji wa wadau hasa wanaoshughulikia masuala ya watoto pamoja na shughuli za watoto wanapofanya kazi na kuishi mtaani ziingizwe katika bajeti.
Kwa upande wake kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Hilda Ndambalile akiutambulisha mradi huo kwa wajumbe alisema kuwa lengo kuu ni kuweza kuimarisha usalama wa mtoto hususani watoto ambao wako mitaani na wanafanyishwa kazi pamoja na kuwaunganisha watoto waishio mtaani, kwenye stend za mabasi na wanafanyishwa kazi na kuwaunganisha wao na wazazi wao ili kuwa imara na kuweza kujitegemea hapo baadae kwa usatawi wa maisha yao .