Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed ametembelea na kukagua mradi wa maji wa miji 28 kutoka Wizara ya Maji unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa mlMazingira Manispaa ya Songea (SOUWASA) ambapo amesema kuwa kiu yake kuona mradi huo unakamilika kwa wakati ili wananchi wapate huduma ya MLmaji safi.

Kanali Abbas ametembelea mradi huyo jana kwenye eneo la Chandamali Manispaa ya Songea ambako limejengwa tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita milioni 2 kati ya matenki matatu yenye uwezo wa kuhifadhia lita milioni 9.

Amesema kuwa amejiridhisha matenki yamekamilika, kichobaki ni mtandao wa kuelekea kwenye chanzo lakini pia changamoto ya malipo ya bilioni 3 ambayo mmepeleka wizarani ambako wanaifanyia kazi na wameiweka kwenye kipaumbele cha malipo yajayo ili kazi ziendelee.

“Wito wangu tuendelee kufanya kazi zile ndogo ndogo zilizopo ambazo mnaziweza kwa pesa zenu lakini zile ambazo zinahitaji hiyo pesa tuendelee kusubiri na zikija tufanye kazi usiku na mchana kuhakikisha miradi hii inaenda kukidhi mahitaji ya wananchi” amesema Kanali Abbas.

Amesema takwimu za mkoa kwa maana ya ongezeko la watu la asilimia 2.7 za ukuaji zinafanya mahitaji ya maji kuwa makubwa na mradi huu unaenda kuwa mkombozi kwa hiyo ni kujitahidi kufanya kazi kwa bidii.

Hata hivyo amemtaka mkandarasi China Civil Engineering Consttruction Corporation (CCECC) asisubirie malipo tu kutoka serikalini bali aangalie vyanzo vingine kwa kutumia kampuni yake kwani watafidiwa na Serikali na kuendelea kusubiri husababisha kazi kusimama .

Awali akisoma taarifa ya hali ya utekelezaji wa mradi huo wa maji miji 28 katika Manispaa ya Songea mhandisi Vicent Bahemana amesema kuwa mradi huo ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuboresha huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika miji 28 nchini Tanzania.

Amesema kuwa mradi huo unalenga kuongeza upatikanaji wa maji safi na kuboresha miundombinu ya maji ili kuhakikisha huduma bora kwa wakazi wa mji Songea,ambapo mkataba wa mradi ulisainiwa Machi10, 2023 kati ya Wizara ya Maji na mkandarasi CCECC na ameanza ujenzi wa mradi Januari 22024 na mpaka sasa amefikia asilimia 5 za utekelezaji wa mradi.

Kwa upande wake mkurugenzi wa SOUWASA mhandisi Patric Kibasa alisema kuwa mradi huo ambao hadi kukamilika utagharimu bilioni 145.77 ambao utahusisha ujenzi wa miundombinu ya kudaka maji ( inteke) katika mto Anjuga uliopo kijiji cha Kikunja katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea ili kuongeza uzalishaji maji lita milioni 17 kwa siku.

Aliitaja miundombinu mingine kuwa ni ujenzi wa matenki ya kuhifadhia maji matatu yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 9 na mpaka sasa mkandarasi ameanza kujenga matenki yote matatu ya kuhifadhi maji pamoja na kujenga miundombinu ya bomba za usambazaji maji km.34.7 ili kufikia wakazi wengi zaidi wa Manispaa ya Songea.