Wananchi wa Kata ya Shibula Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza wameiomba Serikali kuharakisha ulipaji wa fidia ili waweze kuendelea na uwekezaji katika maeneo mengine huku wakieleza kuwa ucheleweshwaji wa fidia hiyo umekuwa ukirudusha nyuma maendeleo yao.
Hayo wameyabainisha February 21, 2025 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa wa Nyamwilolelwa uliowahusisha wananchi wa mitaa mitano iliyoko Kata ya shibula na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Said Mtanda.

Katika mkutano huo wananchi hao walitarajia kupata majibu ambayo yangekuwa ni suluhu ya kumaliza mgogoro kati yao na mipaka ya uwanja wa ndege wa Mwanza uliodumu kwa muda mrefu.
“Leo tulitarajia kupata suluhu ya mgogoro huu lakini imekuwa tofauti na matarajio yetu hivyo tunazidi kuiomba Serikalu yetu ituangalie Kwa jicho la huruma ili iweze kutulipa fidia tujiendeleze kiuchumi”, Wamesema.
Wameeleza kuwa wamekuwa wakiishi maisha ya shida sana kutokana na kuzuiliwa kuendeleza ujenzi hatua inayopelekea watu wazima kulala chumba kimoja na watoto.
Kwaupande wake mjumbe wa Kamati ya mgogoro Kata ya Shibula, Michael Materego amesema tangu mgogoro huo uanze kufukuta ni miaka 11 hadi sasa na wananchi wamekuwa wakikosa usingizi.

Amesema wanatamani sana mgogoro huo uishe ili maisha mengine yaendeelee na wananchi waweze kujiimarisha kiuchumi.
“Siku zote mtu anae kupotezea muda huwa ni adui wa maendeleo hivyo tunaiomba sana Serikali iharakishe ulipaji wa fidia ili nasisi tuwe na maisha mazuri kama watu wengine”, Amesema Materego.
Awali akizungumza kwenye kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amewasihi wananchi hao kuwa watulivu kwani suala hilo linaendelea kutafutiwa suluhu na Serikali.
Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni sikivu sana hivyo hakuna mwananchi yoyote atakae nyanganywa haki yake.
