Na Chrispin Kalinga, JamhuriMedia, Njombe

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka ameongoza mkutano wa pareto na mdau mkuu wa PCT uliofanyika Halmashauri ya Wilaya ya Makete.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wilaya ya hiyo wakiwemo Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Kilimo kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Njombe pamoja na wananchi wa maeneo hayo wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Makete m Juma Sweda leo Januari 11, 2024

Akizungumza na wananchi waliojitokeza Mtaka amesema kuwa, Wilaya ya Makete inakwenda kukua kiuchumi kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa haswa kwenye maeneo ya kilimo cha pareto pamoja na kilimo cha ngano.

Aidha Mtaka amesema kuwa, katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete yenye kata 23, jumla ya kata 21 zinafaa kwa kilimo cha zao la pareto ambapo jumla ya eneo lenye ukubwa wa hekta 2800 zinafaa kwa kilimo cha zao la pareto katika kata 21.


Ikumbukwe kwamba zao la pareto hapa nchini Tanzania linaumuhimu mkubwa kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa madawa mbalimbali ya kuua wadudu ambapo makampuni ya madawa duniani hutumia sumu ya pareto katika kutengeneza madawa (Viuadudu), unga wa maua ya pareto hutumika kuhifadhi nafaka kama vile mahindi, maharage ili yasishambuliwe na wadudu waharibifu.

Sambamba na hayo Mtaka amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuutazama na kuukuza kiuchumi Mkoa wa Njombe kwenye sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta ya kilimo ambapo amesema, Wilaya ya Makete ina jumla ya Maafisa Ugani Kilimo 59, ambapo kati ya hao watatu (3) wapo ngazi ya Makao Makuu ya Wilaya hiyo na Maafisa Ugani 56 wapo ngazi ya Kijiji na Kata na wote hao wamepatiwa Pikipiki kwa ajili ya utendaji kazi wa kuwahudumia wakulima.

Uwepo wa Maafisa Ugani ngazi hizo unasaidia kutoa ushauri wa Kitaalam kwa wakulima ngazi ya Jamii, Watendaji wa Kata na Vijiji wanasaidia katika uhamasishaji wa Kilimo cha Pareto na kuwezesha tija na uzalishaji kuongezeka.