Na Raphael Okello, JamhuriMedia,Musoma
MKUU wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda amewataka watendaji wakuu katika halmashauri za Wilaya ya Musoma na Bunda kuhamia katika majengo ya ofisi zao mpya ifikapo Oktoba 20, mwaka huu .
Mtanda ametoa agizo hilo Septemba 23, 2023 wakati alipokuwa kwenye ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi ya ujenzi wa hospitali na vituo vya afya na shule mpya za sekondari katika halmashauri ya Musoma.
Amekumbusha kuwa ujenzi wa majengo ya halmashauri hizo zilianza tangu 2021 lakini hadi sasa halmashauri hizo zimeshindwa kuhamia katika ofisi hizo ili kuwahudumia wananchi kwa karibu.
“Nawaagiza ifikapo Oktoba ishirini mwaka huu msipohamia katika majengo ya ofisi zenu za halmashauri nitawatumia JKT kuhamisha vifaa vyote na kuzileta katika majengo haya” amesema Mtanda.
“…….Hivyo vivyo ujumbe huu uwafikie halmashauri ya wilaya ya Bunda ,ameongeza Mtanda.
Akiwa katika ukaguzi wa miradi hiyo katika halmashauri ya Musoma aliwapongeza viongozi wa halmashauri hizo kusimamia vizuri manunuzi ya vifaa vya ujenzi wa miradi na kushirikiana vizuri na wananchi katika ujenzi wa miradi.
Amewaomba viongozi wa CCM katika Wilaya za Mkoa wa Mara kuendelea kusimamia kikamilifu bila kuona aibu utekelezaji wa miradi mbalimbali kama ilani ya CCM inavyosema.
Mtanda alipokea pia taarifa ya ujenzi wa vituo vya afya katika halmashauri ya wilaya ya Musoma na kuhimiza utoaji Bora za huduma za afya katika halmashauri hiyo.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo cha afya cha kiriba, Mtendaji wa kata ya kiriba, Victor Edward amesema wamepokea jumla ya shilingi Milioni 750 .
Amefafanua kuwa awamu ya kwanza walipokea milioni 500 na awamu ya pili kiasi cha shilingi milioni 250.