Na Happy Lazaro, JamhuriMedia, Arusha
Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda ameutaka uongozi wa halmashauri ya jiji la Arusha kuhakikisha wanawapa kipaumbele wazawa wa makampuni katika kuwapatia kazi za tenda.
Makonda ameyasema hayo leo mkoani Arusha katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri ya jiji la Arusha ambalo limeonekana kusua sua kwa muda mrefu bila kukamilika kwa wakati.
Aidha Makonda amesisitiza Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha kutumia wenyeji wa Arusha na wenye sifa kwenye tenda mbalimbali ili kukuza pato la mkoa.
Hata hivyo amemwagiza mkandarasi anayesimamia Ujenzi huo kwa awamu ya pili kuhakikisha kuwa anakamilisha kazi yake mwezi Mei mwaka huu badala ya mwezi Julai iliyokuwa imepangwa awali.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa ametembelea jengo hilo baada ya kuelezwa kuwa mradi huo umekuwa ukisuasua bila sababu za msingi ilihali tayari Rais Samia Suluhu Hassan alikwisha idhinisha zaidi ya Bilioni 6 za ujenzi wa awamu ya pili ya jengo hilo la ghorofa sita.
“Naomba sana taratibu za kimkataba na Ujenzi kwa awamu ya tatu kuanza kuandaliwa haraka badala ya kusubiri kukamilika kwa ujenzi awamu ya pili ili kuondokana na.changamoto mbalimbali.ambazo zinapelekea kuchelewa kwa jengo hili.”amesema Makonda.
Aidha Makonda amewataka pia Madiwani, Wataalamu na Viongozi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha kushikamana na kuhakikisha kila wanachokifanya kinakuwa na matokeo chanya kwa Wananchi kama sehemu ya Kumpa sifa na Shukrani Rais Samia Suluhu Hassan anayehakikisha mara zote kuwa serikali yake haiwi kikwazo kwa maendeleo na ustawi wa wananchi wake.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Arusha John Kayombo amesema kuwa amepokea maelekezo yote ya mkuu wa mkoa na wataenda kuyatekeleza huku wakihakikisha jengo hilo linakamilika kwa wakati kama walivyoelekezwa .
Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe amemshukuru Makonda kwa namna anavyokuza uwajibikaji Mkoani Arusha, huki akiahidi kushirikiana na Wataalamu na Watendaji wengine katika kusimamia kikamilifu maelekezo hayo ili kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na Ujenzi wa Jengo hilo haraka iwezekanavyo.