Mbunge-wa-Jimbo-la-Mvomero-Amos-Makala-akifafanua-jambo-kwa-wananchi-hawapo-pichani.Serikali mkoani Kilimanjaro imekabidhi ekari 2,470 kwa Chama cha Ushirika cha Wakulima na Wafugaji Lokolova.

Hatua hiyo imefuta mpango wa awali wa Serikali wa kulifanya eneo hilo la ardhi litumike kujenga soko la nafaka la kimataifa na mji wa viwanda.

Hafla ya kukabidhi eneo hilo ilifanyika kwenye mkutano wa hadhara wa wanachama wa ushirika huo ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla, mwishoni mwa wiki.

Ulikuwa ni utekelezaji wa uamuzi wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).

Akikabidhi eneo hilo, RC Makalla amesema Serikali imeridhia kuendelea na ujenzi wa soko la kimataifa la nafaka kwa kutumia ekari 140 ambazo ilipewa na chama hicho cha ushirika; na kwamba ekari 2,470 zinarejeshwa kwa wanachama.

“Ofisi yangu kwa dhati kabisa inawashukuru ushirika wa Lokolova kwa kuipa Serikali ekari 140 kwa ajili ya kujenga soko la nafaka, hivyo sioni sababu ya Serikali kuingia katika mgogoro na wananchi badala yake ofisi yangu inatakiwa kuwa kimbilio la wananchi, hivyo nawakabidhi eneo lenu lenye ukubwa wa ekari 2,470 mwendelee na shughuli zenu kama ilivyo kuwa hapo awali,” amesema.

 Amewaeleza wana ushirika hao kuwa nia ya Serikali ni kulinda na kuimarisha vyama vya ushirika.

Ametaka ardhi waliyorejeshewa waitumie vizuri kwa ajili ya manufaa ya ushirika na Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha, yakiwamo mafunzo.

Serikali imewaonya wana ushirika hao kuepuka migogoro kwa maelezo kuwa ushirika wenye migogoro hauwezi kupiga hatua yoyote kimaendeleo.

Awali, akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mwenyekiti wa Ushirika huo, Samuel Lyimo, alisema  mgogoro wa ushirika huo na Serikali ulianza  wakati wa uongozi wa aliyekuwa RC wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, kwa kisingizio cha kujenga mji wa viwanda ambako ofisi yake ilifuta ushirika huo na kutangaza kuwa ekari 2,470 zitatumika kujenga mji huo pasipo kushirikisha ushirika. Mgogoro huo ulidumu kwa miaka mitatu.

Akishukuru kwa niaba ya wananchi, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia, alimshukuru RC Makalla kwa busara na ujasiri katika kuingilia kati mgogoro huo ambao ulikuwa ukihatarisha amani na usalama.

Mbatia aliwataka wana ushirika kukaa na kumaliza tofauti baina ya wakulima na wafugaji, akisema kukabidhiwa ardhi ni hatua nyingine na kuliendeleaza kwa amani na mshikamano ni jambo muhimu.

Katika hatua nyingine, RC Makalla ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kilimanjaro kuchunguza na kuchukua hatua za kisheria kwa viongozi walioidhinisha Sh milioni 260 kwa fidia.

Makalla ametoa agizo hilo alipotembelea Kiwanda cha Saruji Moshi akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

Amesema kuna dalili za kuwapo kwa harafu ya rushwa katika uidhinishwaji fedha za malipo ya fidia.

Amesema fedha hizo zimelipwa na Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Rombo kwa wananchi tisa kwa ajili ya kupisha ujenzi wa Kiwanda  cha Saruji kilichopo Holili.

Amesema mchakato wake unatia shaka kutokana na wawekezaji kudai hati ya eneo hilo ilhali halmashauri ikiwa ndiyo iliyolipa fidia.

Amesema kiwanda hicho kilianza uzalishaji Septemba, mwaka jana na kwamba hadi sasa halmashauri si mbia na haipati kodi yoyote, ikiwamo ya huduma.

“Umiliki wa ardhi hii ni jipu, halmashauri walifidia watu milioni 259 fedha za serikali na mwwekezaji akaja akaweka kiwanda hiki.  Kisingizio ni kwamba Baraza la Madiwani lilikaa likapitisha fedha hizo, lakini cha kushangaza halmashauri haimiliki na wawekezaji wanataka hati kwa jina lao,” ameeleza Makalla kwa mshangao.

Ameongeza: “Nawaagiza TAKUKURU kuchunguza suala hili kama kuna watu walishinikiza kutoa fedha hizo na kutufikisha hapa tulipo sheria ifuate mkondo wake- wakajibu mahakamani maana mpaka sasa ninavyoongea halmashauri haipati kodi yoyote kutoka katika kiwanda hiki.”

Amesema wawekezaji walipaswa kukodishiwa eneo hilo, na si kumilikishwa.

“Sitaki kuwa sehemu ya jipu, siwezi kuvumilia mambo haya na sasa wanatumia anuani ya Mkuu wa Mkoa; nimeshawaambia ni marufuku, watumie anuani yao maana mwisho wa mambo yote nitaambiwa mawasiliano yanaendelea na Mkuu wa Mkoa ambaye ni mimi mpya, hivyo sitaki kuingia katika matatizo haya,” amesema.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa mkoa ametoa wiki nne katika kiwanda hicho kuchukua hatua za dharura za kudhibiti uchafuzi wa mazingira.

“Nilikuja hapa baada ya kusikia kuna uchafuzi wa mazingira na kukiukwa kwa sheria na taratibu zilizowekwa na Baraza la Mazingira na tuhuma nyingine zimethibitika kwamba mnawatesa wafanyakazi na hamuwapi vifaa vya kazi. Nawatakeni mrekebishe hali kabla ya Serikali haijawachukulia hatua kali zaidi,” ameagiza Makalla

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya (DC) ya Rombo, Lembris Kipuyo, amesema upatikanaji wa eneo hilo la uwekezaji ulianza kwa kufanya vikao na wananchi wamiliki baada ya kuwapo wazo la Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro chini Gama.

“Chini ya vikao vya halmashauri sina uhakika kama ni vya kisheria ama laah… viliidhinisha fedha zitafutwe za kuwalipa wananchi waliokubali maeneo yao kufanyiwa uthamini na ekari 129.31 zitengwe kwa ajili ya uwekezaji. Sh milioni 259.9 zililipwa kama fidia wamiliki tisa kwa ekari 70.31,” amesema DC.

Mratibu wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) Kanda ya Kaskazini, Menan Jangu, amesema kuna ukiukwaji mkubwa ya sheria za mazingira katika kiwanda hicho.