Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ameyasema hayo leo wakati wa kikao cha tathimini ya utekelezaji wa viashiria vya mkataba wa Lishe kwa Kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2023 katika ukumbi wa Arnatoglo Mnazimmoja Jijini Dar es Salaam.
RC Chalamila amesema kulingana na matokeo ya Tafiti ya Tanzania Demographic and health Survey (TDHS 2022) asilimia 18 (138,396) ya watoto walio chini ya miaka mitano katika Mkoa wa Dar es Salaam wamedumaa kwa upande wa Tanzania Bara matokeo hayo ya utafiti Mkoa wa Dar es Salaam ndio Mkoa wenye asilimia ndogo ya udumavu kuliko mikoa mingine ya Tanzania bara.
Aidha kulingana na athali kubwa za udumavu bado idadi hiyo ni kubwa kwa kuwa Lishe duni huchangia utapiamlo ambao husababisha kwa kiwango kikubwa cha vifo vya watoto walio na umri chini ya miaka mitano.
Hata hivyo tusipochukua hatua tutatengeneza Taifa lisiloendelea kwa kukosa nguvu kazi ya kutosha na maamuzi yenye tija, Pia lishe duni kwa wanawake wajawazito ni miongoni mwa sababu zinazowaweka katika mazingira hatarishi zaidi yanyoweza kusababisha kujifungua watoto wanaozaliwa na uzito pungufu, kuzaliwa kabla ya wakati/ njiti au wafu, watoto wenye mtindio wa ubongo au hata mimba kuharibika kabisa.
Vilevile RC Chalamila ametoa wito kuhamasisha jamii kuhusu mtindo wa maisha ikiwemo ulaji unaozingatia afya na kufanya mazoezi ya viungo, pia amezitaka Halmashauri zote za mkoa huo kutenga bajeti kwa ajili ya kutekeleza afua za Lishe kama ilivyo elekezwa na mamlaka husika.
Kwa upande wa Mganga mkuu wa Mkoa Dkt Rashid Mfaume amesema Rais Dkt Samia kwa kulipa kipaumbele suala la Lishe amesaini mkataba wa Utekelezaji afua za Lishe na wakuu wa mikoa yote 26 ili kuwapima utendaji wao hivyo Mkoa kupitia idara ya Afya, Ustawi wa jamii na Lishe imejipanga kikamilifu kumaliza au kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la Udumavu katika Mkoa wa Dar es Salaam.