Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Albert Chalamila amesema hivi karibu wataanza oparesheni maalum inayolenga waganga wa kienyeji wanaofanya ramli chonganishi.
Amesema hayo leo Dar es Salaam wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambayo yanafanyika kila mwaka Juni 16.
“Nataka niwaambie rasmi nitaanza oparesheni maalum kwa waganga wa kienyeji, nawatangazia rasmi hakuna atakayenitisha narudia tena, hakuna mganga anayenitisha. Mganga anayewaambia watu wakaue mtoto halafu awapelekea viungo kwa ajili ya ushirikina hatavumilika,”amesisitiza.
Amesema lazima kuweka utaratibu maalum katika mkoa huo kwani watawasafisha waende kwingine huku akitaja tabia hizo kuwa ni tabia mbovu, asiyovumilika na ushamba.
Chalamila amesema: “Tukiwaacha waganga watoto wataisha, leo watasema wanataka viungo vya albino baadae watasema mtoto mwenye kitambi baadae watasema tunataka mtu aliyewahi kuwa kiongozi kama mkuu wa mkoa mwenye kitambia na upara kidogo.”
Mkuu huyo wa mkoa amesema ni lazima kukemea vitendo hivyo kwa sababu watu vinaleta madhara wa jamii.