-Awakutanisha DART, Manispaa ya Ubungo na Wafanyabishara wadogo.
-Aeleza dhamira ya Serikali kutekeleza mradi huo
-Asisitiza bado Serikali itaendelea kujali na kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wadogo
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar ea Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila leo Julai 13,2024 amekutana na wafanyabishara wa Simu 2000 ikiwa ni ahadi aliyoitoa wiki iliyopita baada ya wafanyabiashara hao kufanya mgomo katika eneo hilo.
RC Chalamila akiwa katika eneo la kituo cha Simu 2000 amewakutanisha wafanyabiashara hao na Wakala wa Mabasi Yaendayo Kasi (DAR), na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ambapo mawasilisho ya utekelezaji wa mradi wa kujenga karakana kwa ajili ya mabasi ya mwendokasi na umuhimu wake kwa pande zote mbili Manispaa na DART yaliwasilishwa kwa uwazi mbele ya wafanyabiashara hao.
Aidha RC Chalamila alitoa nafasi kwa wafanyabiashara hao kutoa maoni huku akiweka wazi dhamira ya serikali kutekeleza mradi huo ambao una masilahi mapana kwa umma na kuwahakikishia pamoja na kutekelezwa kwa mradi huo bado kuna sehemu ambayo wafanyabiashara hao watapatiwa ili kufanya biashara zao lakini pia katika kipindi chote cha kutekeleza mradi huo utaratibu utawekwa ili kutovuruga biashara zilizoko.
Vilevile RC Chalamila amesema hakuna Serikali isiyojali wafanyabiashara bali inapotokea kuna mradi wenye masilahi mapana kwa umma lazima tupishe,pia sio vizuri kuwa na migomo ya mara kwa mara kama una maoni au ushauri wasilisha katika njia nzuri “wale wote waliotoa maoni leo yenye tija wakati wa kutekeleza mradi huo yatazingatiwa kwa umakini mkubwa” amesema Chalamila.
Mwisho RC Chalamila ametoa rai kwa wakazi wa mkoa huo kuilinda Dar es Salaam kwa nguvu zote amani ikitoweka athari zake ni kubwa.