Miaka miwili iliyopita Rais Jakaya Kikwete alipofanya uteuzi wa wakuu wa mikoa, nilifurahi. Nilifurahi baada ya kusikia wamo vijana walioteuliwa, na hasa mmoja tuliyekuwa tukifanya kazi wote chumba cha habari Majira, Fatma Mwassa. Huyu sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora na anaendelea vyema.
Nilimpigia simu Mwassa nikampongeza na hakika sijakatishwa tamaa na utendaji wake. Amedhihirisha kuwa kumbe baadhi ya watu wakipewa nafasi wanaweza kutenda. Nitumie fursa hii kumpongeza Mwassa kwa utendaji wake uliotukuka. Nimekaa Tabora hivi karibuni sikusikia wananchi wakimlalamikia.
Mtu mwingine aliyetuliwa nikafurahi ni Mwagesa Mulongo. Huyu kijana alikuwa Mkuu wa Wilaya pale Bagamoyo, na ilikuwa ni siku chache tangu nilipotoka kumtembelea ofisini kwake. Baada ya uteuzi wake, nilimpigia simu hakupokea. Nikamtumia ujumbe mfupi wa pongezi (sms) hakujibu.
Hii haikunipa shida sana. Nikadhani labda alikuwa amebanwa na shughuli za hapa na pale. Mwaka mmoja baadaye nikampigia simu hakupokea. Lakini hapo katikati nikapata taarifa kwenye mitandao ya kijamii wakiandika maneno nisiyojua waliyatoa wapi.
Wakasema Mulongo hana uwezo wa kuongoza, amepelekwa Arusha kufanya kazi moja tu ya ushushushu dhidi ya Edward Lowassa. Wakasema Mulongo alipelekwa pale kuunganisha nguvu na Mary Chatanda kudhibiti nguvu ya Lowassa. Ulivyofika uchaguzi wa CCM kazi aliyoifanya sina haja ya kuirudia, wote waliosikia walithibitisha maneno haya.
Binafsi nilidhani kuwa tatizo la Mulongo ni Lowassa, basi. Baadaye nikaona ameanza kujiingiza kichwa kichwa katika suala la kuidhibiti Chadema. Akawa anavaa mabomu bila kujua. Akaanza kuendekeza ujinga dhidi ya Mbunge wa Chadema, Godbless Lema. Akaanza kufanya kazi sawa na wakoloni. Akaanza kuwatumia polisi.
Mulongo ni kijana mdogo, lakini kwa sasa amevimba kichwa. Anadhani kwa kuwatumia polisi anaweza kuisambaratisha Chadema Arusha kumbe anaijenga zaidi. Wakati naandika makala haya, nasikia Lema aliyekamatwa mwishoni mwa wiki huenda akafikishwa mahakamani wiki hii kwa kosa la uchochezi.
Binafsi nimejiuliza na sipati jibu. Sipati jibu nini maana ya uchochezi. Nimemsikiliza Lema maneno aliyokuwa akiwaambia wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha. Amewataka kuwa makini na usalama wao. Amewaasa kujiepusha na masuala ya kwenda disko hadi usiku wa manane bila kujali usalama wao.
Akawazuia wasiandamane na wamsubiri mkuu wa mkoa kuzungumza naye. Mkuu wa Mkoa Mulongo amefika kwenye eneo la tukio. Badala ya kuzungumza na wanachuo, akasusa. Akasusa eti kwa sababu wamemzomea. Hivi Mulongo katika masomo yake hakupata kusoma somo liitwalo ‘conflict management?’
Maana nilitaraji Mulongo awe wa kwanza kufahamu kuwa katika mgogoro kama ule ambao wanafunzi wanaona hawapewi ulinzi wa kutosha kuzomewa, kusonywa, kupigiwa mbinja na mengine ni jambo la kawaida. Alitarajia katika mazingira yale wamwimbie wimbo wa ‘CHAMA CHETU CHA MAPINDUZI EHEEE CHAJENGA NCHI….’
Kama alitarajia hilo, basi hana hata chembe ya uongozi ndani yake. Hizi kesi za kutunga dhidi ya wanasiasa huwa zinajenga umaarufu zaidi kwao badala ya kuwabomoa. Nimesikia baadhi ya watu wakisema viongozi wa aina ya Mulongo huenda wakaweka rekodi ya kuwa wakuu wa mikoa wa kipindi kimoja.
Nchi hii ilikuwa imepiga hatua katika uhuru wa watu kutoa mawazo. Mulongo kwa kudhani ataziba midomo ya watu kwa kutumia polisi na farasi, hasomi alama za nyakati. Ningekuwa Mulongo, katika kikao hicho ningeshirikiana na wanachuo kuandaa hata utaratibu wa polisi jamii. Kuwasusa wanachuo au kumshitaki Lema si suluhisho. Mulongo, anagalia ‘ligwaride lisikushinde.’