Kimewaka
*Serikali ya Muungano kuwa na wizara nne
*Makao makuu ya Tanzania kuhamia Dar
* Tanganyika ni Dodoma , Wazanzibari wanalo
Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano yataleta mtikisiko mkubwa katika mfumo wa uongozi wa Taifa hili. Makao makuu ya Serikali za Tanganyika na Tanzania ni miongoni mwa mambo hayo.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, zinasema kuwa yapo makubaliano yaliyofikiwa kuwa Katiba mpya itakapokamilika, Serikali ya Muungano iwe na mawaziri wanne pekee.
“Tulijadili sana suala hili kwenye Tume na lilikuwa na mvutano mkubwa. Pamoja na kwamba tumeweka ukomo wa wizara 15 kwenye rasimu, ukweli tuliona na ilidhihirika kuwa wizara zitakuwa nne tu,” kilisema chanzo chetu cha habari kutoka kwenye Tume hiyo.
“Kihalali ilibainika kuwa wizara hizo ni ya Ulinzi, Mambo ya Ndani, Fedha; na Mambo ya Nje.”
Chanzo hicho kimelieleza JAMHURI kwamba kutokana na hali hiyo, ishawishiwe Makao Makuu ya Tanzania sasa yahamie rasmi Dar es Salaam kutoka Dodoma , wakati Makao Makuu ya Serikali ya Tanganyika yawe Dodoma.
“Hapa napo paliibuka mjadala mzito. Wajumbe walikuwa na hoja kuwa Ikulu ya Dar es Salaam kimsingi ni ya Tanganyika iliyoachwa na mkoloni. Sasa inakuwaje tukisema Ikulu ya Tanganyika iwe Dodoma uhalali wa majengo ya Ikulu kumilikiwa na Serikali ya Muungano utakuwapo?” Alihoji mmoja wa wajumbe wa Tume na kuongeza:
“Hata hivyo, baada ya kushauriana mno, ikaonekana huo unaweza kuwa mchango sahihi wa Tanganyika katika Serikali ya Muungano, sawa na Zanzibar watakavyotoa mchango mwingine. Tanganyika makao makuu yake yakiwa Dodoma , hii itaongeza kasi ya maendeleo kwa nchi ya Tanganyika kwa sababu watu watakuwa hawalazimiki kusafiri kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kazi za maendeleo.”
Chanzo kingine kimesema nia ya kushauri Tanganyika makao makuu yake yawe Dodoma ni kwamba huko ndiko katikati ya nchi ya Tanganyika na kwa uhalisia Dar es Salaam ni karibu na Zanzibar na hivyo itakuwa rahisi kwa washirika wa Muungano kuendesha Serikali ya Muungano ikiwa Dar es Salaam kuliko Dodoma.
Hoja nyingine ya kuhamisha makao makuu iliyotumika, ni kwamba mabalozi wa nchi mbalimbali wamejenga ofisi na makazi yao Dar es Salaam , hivyo kuwahamisha itakuwa vigumu.
“Na kimsingi, ukiacha suala la ulinzi, jukumu kubwa la Serikali ya Muungano ni Mambo ya Nje, na hivyo kwa kuwa mabalozi wako Dar es Salaam na Serikali ya Muungano ndiyo yenye kusimamia jukumu hili, ni bora ikaendesha shughuli zake ikiwa Dar es Salaam ,” kilisema chanzo chetu.
“ Tanganyika ikiwa pale Dodoma itafungua uchumi wa nchi kwenda kusini, kaskazini na mgharibi kwani angalau tayari mashariki kuna nafuu,” ameongeza mtoa habari wetu.
Hofu ya jina Tanzania kufutika
Hofu ya jina Tanzania kufutika ilikuwa mjadala mzito kwenye Tume ya Marekebisho ya Katiba.
“Mjadala ulikuwa ni iwapo tuko tayari kuruhusu jina Tanzania kufutika kwenye ramani ya dunia. Kwa sasa wanaokwenda nje ya nchi wakajitambulisha kama Watanzania ni watu kutoka Tanzania Bara. Wazanzibari wanajitambulisha kama Wazanzibar,” kimesema chanzo chetu.
“Kutokana na hofu hiyo, ndiyo maana tukasita kuwa tukiruhusu kutumika kwa jina Tanganyika , hawa nao watakwenda nje ya nchi wakijitambulisha kama Watanganyika, na hivyo ramani ya Tanzania itafutika katika dunia ya sasa. Hatujui fufanyeje,” kimeongeza chanzo chetu.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azavel Lwaitama, ameliambia JAMHURI mwishoni mwa wiki kuwa hofu ya watu kujitambulisha kama Wazanzibari au Watanganyika na kuua Tanzania ni ulegelege wa Serikali.
“Rais Obama anakuja na ujumbe wa watu 700, hawa wanatoka majimbo mbalimbali kama Mississippi , Minnesota , California , Washington , New York na mengine, lakini hata siku moja hawa hawajitambulishi kwa majimbo yao . Wakiwa nje ya nchi wanatakiwa kujitambulisha kama Wamarekani.
“Hata Gavana wa Jimbo lolote la Marekani anaposafiri nje ya nchi anasafiri na Bendera ya Marekani, si ya Jimbo lake. Ni marufuku kwa Mmarekani yeyote kujitambulisha kwa Jimbo analotoka, bali taifa lake kama Mmarekani,” anasema Dk. Lwaitama.
Mwanasheria Mwandamizi aliyeomba asitajwe gazetini, anasema hofu hiyo imezaa wazo la Tume ya Marekebisho ya Katiba kukataa matumizi ya jina la Tanganyika , na kupendekeza Tanzania Bara angalau Watanganyika wakienda nje ya nchi wajitambulishe kama Watanzania kwani Wazanzibari hawafanyi hivyo.
“Hapa ni rahisi tu. Katiba ya Muungano inapaswa kutamka bayana kuwa kila Mtanzania akienda nje ya nchi anawajibika kujitangaza kama Mtanzania na si Mtanganyika au Mzanzibari. Iwekwe sharti la kikatiba kuwa mtu akijitambulisha kama Mzanzibari au Mtanganyika, basi anyang’anywe passport (hati ya kusafiria) milele. Hii itawajengea hofu watu kutotumia u-Tanganyika au u-Zanzibari,” anasema mwanasheria huyo.
Ardhi si mali ya Muungano
Mwanasheria huyo anasema Wazanzibari wanajidanganya kama wanakimbia kununua ardhi katika maeneo mbalimbali ya Tanganyika , kwani watapoteza fedha zao bure.
“Bila hata kubadili sheria ya sasa, kitakachobadilika katika sheria za ardhi Na. 4 na Na. 5 za mwaka 1999 ni jina kutoka Tanzania kwenda Tanganyika. Sheria iko wazi, kuwa mtu ambaye si Mtanganyika ataruhusiwa kupewa ardhi ya Tanganyika iwapo tu anafanya kazi ya uwekezaji.
“Inatamka wazi kuwa ardhi ya Tanganyika si kwa ajili ya watu kuja kujenga makazi, bali uwekezaji. Hivyo kama kuna Mzanzibari anayejidanganya kuwa akinunua ardhi Tanganyika atajenga na kuishi hapa kama si mwekezaji anapoteza kuda na fedha zake. Ardhi hiyo itachukuliwa na Rais wa Tanganyika bila kulipwa fidia. Wazanzibari wameyataka haya, lazima tuelezane ukweli mgumu,” anasema mwanasheria huyo.
“Umiliki wa ardhi, haki za wenyeji na mipaka ya matumizi ya ardhi kwa wageni utawekwa wazi. Na sasa wageni ni pamoja na Wazanzibari. Nasema Tanganyika wana haki ya kutunga sheria yao na wana haki ya kuweka mipaka kwa walio wageni.
“Wageni hawatapewa haki ya kumiliki ardhi ila watakuwa na haki ya kutumia ardhi. Zanzibar kilichowapa access (umiliki) wa ardhi ya Tanganyika awali ni kwa sababu sisi Tanzania Bara imo ndani ya Muungano. Itabidi Wazanzibari wajue kuwa nao ni wageni wakija Tanganyika .
“Tuliwatahadhalisha na tunaendelea kuwatahadharisha kuwa hata ukinunua ardhi Katiba ya Tanzania Bara itakuwa na haki ya kufuta umiliki wa ardhi. Mzanzibari atatumia ardhi kama mwekezaji ila si makazi, au kilimo cha kujikimu.
“Ni kama ambavyo Wakenya wanakuja wananunua ardhi na nyumba kumbe wanapoteza fedha zao, hata wakikimbilia kununua wanapoteza hela zao bure,” anasema Mwanasheria huyo.
Sheria ya Ardhi ya Zanzibar ya mwaka 1992 hairuhusu mtu asiye Mzanzibari (wakiwamo Watanganyika) kumiliki ardhi Zanzibar.
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, alipoulizwa na JAMHURI juu ya mshikemshike wa ardhi na kuhamishwa kwa makao makuu ya Serikali ya Tanzania kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, alisema kwa ufupi, “Mawazo haya yalikuwapo na yalizungumzwa, ila tusubiri wananchi ndiyo waamue.”
Tafsiri rahisi juu ya mabadiliko haya ina maana Wazanzibari waliojenga Tanganyika wanaokadiriwa kufikia 600,000 wanaweza kulazimika kurejea Zanzibar kwanza na kurudi Tanganyika baada ya kuomba, ama kibali cha ukaazi, au uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kukubaliwa kupewa ardhi baada ya kutimiza masharti.
Moja ya masharti ya uwekezaji watakayopaswa kuyatimiza kupitia TIC ni kwamba lazima mwekezaji kama anataka kwenda kuwekeza Tanganyika awe na mtaji usiopungua dola 100,000 sawa na Sh milioni 160 za Tanzania ndipo apewe vibali vya kuishi. Wazanzibari wanaweza kutakiwa kutekeleza sharti hilo la kisheria.
Tume ya Uratibu wa Muungano kusawazisha mambo
Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa, katika Ibara za 102, 103 na 104 inazungumza Tume ya Uratibu. Tume hiyo inapandekezwa iwajumuishe Makamu wa Rais wa Muungano, Rais wa Zanzibar na Rais wa Tanganyika . Kila nchi itapaswa kuteua Waziri Mkazi (Resident Minister) atakayekuwa kiungo kati ya Serikali yake na Serikali ya Muungano.
Kwa mujibu wa rasimu, Tume hiyo itasimamia uratibu wa mikataba ya kimataifa chini ya Serikali ya Muungano na hapo ndiko hata Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mashirika na taasisi kama Umoja wa Mataifa (UN), Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na meingine yataratibiwa.
“Ikumbuwe hawa wa Tanganyika na Zanzibar watakuwa ni wakuu wa Serikali na si wakuu wa nchi,” anasema mmoja wa wajumbe wa Tume.
Wadau wanena
Njelu Kasaka, Mbunge wa zamani wa Lupa (CCM) anasema udhaifu wa viongozi wa Serikali ya Muungano ndiyo umeifikisha nchi kuwa katika vipande vipande.
Akizungumza na JAMHURI katika mahojiano maalum jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, alisema Zanzibar walianza kidogo kidogo kujiondoa kwenye Muungano na Serikali ikawa inawachekea.
“Walitaka wimbo wa taifa, wakaruhusiwa. Wakataka bendera wakaruhusiwa. Mwaka 2010 wakajitangaza kuwa Zanzibar ni nchi, ambao ni uasi wa wazi kabisa, Serikali ikawaachia. Leo tulikofika ni hapo.
“Kwa hali ilipokwishafikia, kulikuwapo na njia mbili tu. Ama, Serikali tatu, au kuvunja Muungano; na ya pili kwa hali yoyote isingekuwa chaguo sahihi. Naupenda sana Muungano, ila pia nimefurahishwa na mapendekezo ya Tume ya Katiba. Suala tulilolipigania miaka 20 iliyopita, leo limetekelezeka,” anasema Kasaka.
Hata hivyo, anasema suala la ardhi, mafuta, gesi na urani vinapaswa kubaki katika mikono ya Muungano kwa nia ya kuipa nguvu ya kifedha Serikali ya Muungano.
Mwanazuoni mkongwe, Profesa Abdul Mohammed Sheriff, anasema tatizo la ardhi ni moja kati ya matatizo mengi yatakayojitokeza. Ameliambia JAMHURI kuwa matatizo mengi ya Muungano yametokana na ukweli kwamba Mwalimu Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume hawakushirikisha Watanganyika na Wazanzibari katika kufikia uamuzi wa kuunda Muungano wa sasa.
“Walikaa watu wawili huko, wakatia saini Muungano na mmoja akachanganya udongo, basi ndivyo ilivyokuwa. Wananchi hatukuhusishwa kwa kila hali na hili ndilo chimbuko la matatizo yote kwani Muungano hauna ridhaa ya wananchi,” anasema.
Salma Omar Ahmed, Mzanzibari mkazi wa Temeke, Dar es Salaam anasema maombezi yake ni kuwa busara itawale katika mioyo ya viongozi wa kitaifa wakae na kukubaliana juu ya suala la ardhi na mengine.
“Mimi nimejenga hapa Temeke na nimeishi hapa kwa miaka zaidi ya 40 iliyopita. Wapo Wazanzibari wengi wamejenga huko Kigoma, Kahama na kwingineko hapa nchini. Leo kusema Wazanzibari tuondoke au tuishi hapa Tanganyika kama wawekezaji kwa kulipa kodi ni jambo lisiloingia akilini. Mbaya zaidi wengi wetu hatuna uwezo wa kulipa kodi kama wawekezaji,” ameliambia JAMHURI.
Kwa upande wake, Dk. Lwaitama anasema kuwa Watanzania hawapaswi kuhofu.
“Kwa kuwa uraia ni wa Tanzania , naamini Katiba yetu itatoa haki ya kila Mtanzania kuishi eneo lolote la Muungano bila kubughudhiwa. Haya masuala ya ardhi na mengine ni madogo yatapatiwa ufumbuzi,” anasema.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Profesa Josephat Kanywanyi, ameliambia JAMHURI kuwa njia pekee ya kuondoa matatizo yaliyoanza kujitokeza ni kwa viongozi kukaa na kushauriana nini la kufanya kwa nia ya kuepusha Muungano kuvunjika.
Anaongeza kuwa Muungano ni muhimu kwa maendeleo, hivyo unapaswa kulindwa na kila mwananchi.
Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amekaririwa akisema hivi karibuni kuwa kilichotolewa ni rasimu, na si Katiba; hivyo mapendekezo ya wananchi yatatiliwa maanani kwa lengo la kupata ufumbuzi wa kudumu.