Mjadala huu ninaoenda kuuzungumza ni mtazamo na maoni yangu. Nitashukuru kama mjadala huu utagonganisha fikra na mitazamo ya Watanzania wengi. Binafsi, ninaamini kwenye falsafa ya mgongano wa kifkra kwani unazaa mawazo mapya na ambayo hayakuwapo.
Mwezi Agosti wa mwaka 386 akiwa katika bustani, Mwanateolojia mashuhuri wa Kanisa Katoliki, Agustino, alisikia sauti ikimwambia, ‘Twaa na usome, twaa na usome’.
Maneno haya aliyoyasikia Mwanateolojia Agustino nami nayanukuu kwa kukuomba wewe ndugu msomaji wangu kwa kusema, “Twaa na usome, twaa na usome’’. Askofu Fulton J. Sheen alipata kutusihi kwa namna hii, “Usiogope kukosolewa kama uko sahihi, na usikatae kukosolewa kama hauko sahihi’’.
Kwa sababu ninaenda kuongelea mustakabali wa Taifa letu itanilazimu kukosoa na kushauri, itanilazimu kusikitika na kupaza sauti kwa jamii yangu. Ninaamini katika maneno ya Mwanafalsafa George Gordon Byron [1788-1824] kwamba, “Tone moja la wino wa kalamu linaweza kuwafanya mamilioni ya watu kufikiri’’.
Kama ni kujipima, tumejipima sana. Kama ni kuona, tumeona sana, kama ni kutafakari, tumetafakari sana, kama ni kusikia, tumesikia sana, kama ni kuchekwa, tumechekwa sana, kama ni kuvumilia, tumevumilia sana, kama ni kupembua, tumepembua sana, kama ni ukimya, sasa imetosha na kama ni aibu tumeipata.
Jamii yoyote ile ni lazima itembee katika ukweli, haki, maadili, mwanga na elimu. Hakuna jamii inayoweza kuendelea pasipo watu wake kuwa wakweli na wenye maadili. Na akili tafakari na akili bainifu. Si lazima kufuata falsafa ya watu wengine. Tunaweza kutengeneza falsafa yetu inayolenga kuwatoa Watanzania katika giza na kuwaingiza katika mwanga.
Watanzania tuko kwenye wakati mgumu sana. Kama Taifa, kuna haja ya kuvisugua vichwa vyetu na kutafakari namna ya kuijenga Tanzania tunayoitaka. Kama kuna kipindi ambacho Tanzania inahitaji malezi ya kifalsafa ni hiki. Falsafa itatusaidia kuwa na maarifa yatakayotusaidia kufanya uamuzi sahihi kwa kufahamu lipi lifanyike na kwa namna gani; na kwa wakati gani, na lipi tuliache, na kwa nini tuliache.
Falsafa itatusaidia sisi wenyewe na watoto wetu kuwa watu wa tafakari ya kina. Baada ya kufikiri kuwa umaskini tulionao ni mapenzi ya Mungu, tutafikiri umaskini kama matokeo ya kutotumia vyema fikra zetu kwa usahihi katika mipango yetu.
Binafsi uhalisia, tafiti za kisomi, historia na vigezo vya kijiografia vya Taifa letu vinanifahamisha kwamba Tanzania haina laana ya rasilimali. Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi. Binafsi sioni sababu zinazofanya Taifa kama la Tanzania kuitwa taifa maskini. Watanzania wengi bado tunaishi katika umaskini, huku tukiwa hatuna mahitaji ya msingi ya kimaisha kama vile maji safi na huduma bora za afya.
Hii inawafanya watu wengi kufikiri na kuwaza kuwa Tanzania ni nchi maskini, jambo ambalo halina hata chembe ya ukweli ndani yake. Tanzania ni nchi ya fursa! Tuna utajiri wa maliasili, madini, mafuta, wanyamapori, na ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo.
Rasilimali hizi zinaweza kugeuzwa kuwa utajiri wa kumkwamua Mtanzania. Kila niutazamapo Mlima Kilimanjaro ulivyo mrefu na unavyosifika duniani, ninaamini Tanzania ni nchi ya fursa. Ni wapi kwenye madini adimu ya tanzanite? Ni hakika kwamba yanapatikana Tanzania.
Uhalisia huu unaniaminisha kwamba Tanzania ni nchi ya fursa. Hebu angalia, Kanda ya Ziwa imejaa dhahabu, almasi, nikeli. Kanda ya Magharibi imejaa shaba, mafuta na madini ya fedha. Kanda ya Kati ina madini ya urani yanayotumika kutengeneza mabomu ya nuclear. Kanda ya Pwani imejaa gesi na mafuta. Kanda ya Kusini imejaa makaa ya mawe.
Pamoja na utajiri wote huu, bado Watanzania ni maskini wa kupindukia. Hakika hii ni aibu. Kila kanda kuna utajiri mkubwa na wa aina yake. Lakini pia kila kanda wamejaa Watanzania ambao ni maskini waliojikatia tamaa ya kuishi katika nchi yao.
Kuna jambo la kujifunza hapa. Tunaishi kwenye nchi ya maziwa na asali, lakini maisha yetu hayaoneshi kama tunaishi kwenye nchi ya maziwa na asali.
Adui wa Tanzania yupo Tanzania