Jiji la Dodoma linabuni mbinu za kubadili mandhari yake, lengo likiwa kuleta mvuto zaidi kwa wenyeji na wageni.

Miongoni mwa mambo yaliyobuniwa ni kuwapo kwa sheria ndogo inayowalazimu wenye nyumba kuwa na rangi fulani fulani za mapaa ya nyumba kulingana na eneo husika.

Kwa lugha nyepesi ni kuwa rangi itakayotumiwa eneo moja haipaswi kufanana na inayotumika katika eneo jingine. Hatua hii, kwa vyovyote vile itakuwa ni gharama nyingine kwa wananchi, hasa waliokwishajenga.

Tunatambua na kuheshimu uamuzi wa kuipendezesha miji, majiji na hata vijiji vyetu. Miji ikipangwa vizuri na ikawa inajengwa kwa taratibu zinazoeleweka, huwa inawavutia wenyeji na wageni. Ni dalili ya ustaarabu.

Pamoja na nia njema ya Jiji la Dodoma, tunaamini kuna mambo makubwa, muhimu na  ya maana zaidi ya kushughulikia kuliko hili la rangi za mapaa. Suala la rangi kwenye mapaa ni dogo mno, kiasi kwamba halistahili kuchukua muda wa watendaji na viongozi kulishughulikia. Tunapoteza muda kwa jambo lisilo na tija.

Dodoma ndiyo Makao Makuu ya nchi yetu. Dodoma sasa inakuwa ndiyo mji wa mfano wa kufaulu au kufeli kwetu. Sidhani kama wananchi wa Dodoma na wageni watakaozuru mji huo watakuwa na sababu ya kutazama rangi za mapaa ya nyumba na kuzichukulia kama kigezo cha kustaarabika au kuendelea kwetu.

Kwa watu wanaojua maana ya maendeleo, wakiambiwa kwamba Dodoma walichoona cha maana wakati huu wa hekaheka za kulijenga jiji hilo ni rangi za mapaa ya nyumba, kwa hakika watashangaa.

Dodoma inahitaji kuwa na barabara nyingi, pana na safi. Dodoma inahitaji kuwa na maeneo ya wazi mengi. Dodoma inahitaji kuwa na viwanja vya michezo ya aina yote kwa rika zote. Dodoma inahitaji kuwa na wananchi wastaarabu kwa maana ya kuwajenga kitabia ili wazingatie usafi. Dodoma inahitaji miundombinu ya majisafi na majitaka kwa kiwango cha kimataifa.Jiji la Dodoma linapaswa kujengwa kwa namna kwamba mitaa au maeneo fulani yawe na nyumba za kawaida, maeneo fulani yajengwe ghorofa mbili mbili, maeneo mengine yawe ya ghorofa tano tano, na kadhalika. Usiwe mji ambao ghorofa linajengwa katikati ya nyumba za kawaida.

Dodoma inastahili kuwa na sheria ndogo ya kumbana kila mwenye nyumba kupanda miti kuzunguka eneo lake ili kuufanya mji wote uwe wa kijani. Hayo ndio mambo yenye tija.

Kuhangaika na rangi za mapaa ya nyumba ni kupoteza muda na rasilimali fedha. Ni kutafuta lawama kwa sababu hatuamini kama wananchi wote, baada ya kujenga kwa shida, watakuwa na hamu tena ya kutii amri ya kubadili rangi za mapaa ya nyumba zao.

Pamoja na kutambua uzuri wa kuwa na mapaa yenye rangi kulingana na maeneo husika, tunadhani jiji lina mambo mengine mengi ya maana zaidi kuliko hilo. Hayo yaliyo ya maana zaidi ndiyo yanayopaswa kupewa kipaumbele sasa.