Si jambo jema sana kutumia safu hii kueleza shida ninazoguswa nazo moja kwa moja. Si vizuri kwa sababu naweza kuonekana najipendelea.
Hata hivyo, nitakuwa sina msaada endapo nitashindwa kutumia fursa hii kufikisha sauti ya ‘wasio na sauti’ kwa nia njema ya kuona wakisaidiwa.
Hivi karibuni Rais John Magufuli, alitoa msimamo mzuri alipoagiza kwa ukali kabisa wanafunzi wasizuiwe kupata haki yao ya elimu ya msingi hadi sekondari kwa sababu ya michango.
Akaagiza kusiwepo mamlaka ya kumzuia mwanafunzi ambaye mzazi wake hana uwezo wa kuchanga, kupata elimu. Akaagiza wenye michango waiwasilishe katika ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri. Kwa maneno mengine Rais hakuzuia michango, ila alizuia michango kutumika kama fimbo ya kuwakosesha watoto elimu.
Msimamo wa Rais ni utekelezaji wa uamuzi wa Serikali wa kutoa elimu bure kwa watoto kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
Uamuzi huu ni mzuri kwa sababu unaondolea wazazi kero, hasa kwa wale ambao kwa kweli hali zao za kiuchumi ni mbaya. Msimamo huu ni mzuri na unapaswa kuungwa mkono.
Baada ya agizo la Rais Magufuli, wananchi wakageuka ‘mbogo’. Kuna mifano hai kuwa katika baadhi ya maeneo kama wilayani Butiama, wapo wazazi waliofunga safari hadi shuleni kudai hata kile kidogo walichokuwa wamechanga. Kwanini walifanya hivyo? Walifanya hivyo kwa sababu Rais ametangaza kufuta michango!
Namshukuru kupata bahati ya kuzuru maeneo mengi ya nchi yetu kwa kipindi chote cha utumishi wangu wa umma kupitia maandishi. Nimeona matatizo mengi ya walimu na wanafunzi kwenye sekta zote. Kwa namna ya pekee naomba nijadili sekta ya elimu.
Tena basi, naomba radhi niruhusiwe kueleza hali ya elimu katika Wilaya ya Butiama, hususan kijijini Butiama na katika Kata ya Butiama inayojumuisha vijijini vitatu vya Butiama-Buturu na Rwamkoma. Butiama ni wilaya change. Hadi leo haina ofisi za mkuu wa wilaya wala halmashauri. Zinazotumika ni zile zilizokuwa za kijiji! Fikiria saizi ya kijiji na saizi ya wilaya!
Kata hii ina shule tano za msingi- ambazo ni Butiama ‘A’, Butiama ‘B’, na Makore (kijijini Butiama); Buturu (kijijini Buturu), na Rwamkoma iliyoko kijijini Rwamkoma. Butiama ina wakazi zaidi ya 25,000. Hapa napo fikiria, wakazi hao na sekondari moja!
Wanafunzi wanaofaulu kutoka kwenye shule zote tano wanapelekwa kusoma katika sekondari moja pekee ya kata iliyoko Butiama! Mwaka huu wa 2018 wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza ni 443. Mwakani idadi inakadiriwa kuongezeka.
Kwa matakwa ya kitaaluma, wanafunzi hawa walistahili kuwa na vyumba 10 vya madarasa kwa maana ya kuwa na wanafunzi walau 45 katika kila chumba kimoja.
Wanafunzi wote 443 wana vyumba viwili vya madarasa! Viwili tu. Vyumba vingine viwili wanavyotumia ni vya maabara ambazo hazijakamilika. Sasa imeonekana afadhali maabara ‘zikwame’ kwa muda ili wanafunzi wapate sehemu ya kusomea. Idadi nyingine ya wanafunzi zaidi ya 200 wanasomea chini ya miti! Nimezungumza na baadhi ya viongozi wamesema wanahitaji vyumba vingine 7 vya madarasa kwa watoto wa kidato cha kwanza pekee.
Vijiji vinavyounda kata hii ya Butiama viliweka utaratibu wa kujenga vyumba vya madarasa. Kuna pagale lililojengwa kwa michango ya wananchi wa Buturu. Hili limekwama njiani baada ya mkandarasi kutafuna fedha. Wananchi wamegoma kuchanga wakihoji utafunwaji wa fedha hizo za awali. Pagale la pili limejengwa na wananchi wa Rwamkoma. Baada ya agizo la Rais la ‘kufuta michango’ mapagale hayo yote yamebaki kama yalivyo.
Nimezungumza na madiwani kadhaa pamoja na viongozi wengine kwa namna ya kuona wanafunzi na walimu katika sekondari hii wanasaidiwa haraka kuwaepusha na adha kubwa wanazopata.
Majibu ya madiwani ni kuwa uwezo wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kupata fedha za kuongeza vyumba vya madarasa, si tu kuwa ni mdogo, bali haupo kabisa. Wanalia hakuna mapato.
Nimewauliza namna gani wanawahamasisha wananchi kuchangia maendeleo, hasa elimu katika eneo lao. Wanasema majibu wanayoyapata kutoka kwa wazazi yanawakatisha tamaa.
Mosi, wanaambiwa kuwa Serikali imeshasema elimu ni bure!
Pili, wanasema hata kama moyo huo wa kuchanga wangekuwa nao, bado uwezo wao kiuchumi ni duni mno. Wanatoa mfano wa zao la muhogo ambalo limekufa baada ya kuingia ugonjwa hatari.
Ndugu zangu, haya niliyoyaona Butiama endapo nitakaa kimya nitakuwa sehemu ya tatizo. Napongeza juhudi za viongozi, hasa madiwani lakini kwa kweli wamefikia ukingoni. Hawana vyanzo vya mapato vya kuwawezesha kufanya kazi hii.
Naamini kwa kuyaweka hapa tunaweza kushirikiana sote kupata suluhu ili watoto hawa-kama walivyo watoto wengine katika taifa letu, waweze kupata fursa njema ya kufaidi elimu.
Historia ya Kijiji cha Butiama inajulikana. Butiama ilivyo leo ni matokeo ya uadilifu wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mwalimu alifariki dunia mwaka 1999 Butiama ikiwa haina sekondari. Si kwamba alipenda watoto wa eneo analotoka wabaki mbumbumbu, bali inawezekana ni kwa kuamini kwamba yeye kama mzazi alikuwa na wajibu wa kuhakikisha kile kidogo kilichopo kinawafaidisha watoto wote wa taifa letu. Tumeona alifanya hivyo pia kwenye ukombozi wa mataifa ya Kusini mwa Afrika. Mwalimu ameongoza ukombozi wa Msumbiji, Angola, Namibia, Zimbabwe, Afrika Kusini na kwingineko bila kujali uwezo wa taifa kifedha. Alitumwa na dhamira yake njema ya kuwakomboa wanadamu wengine. Angeipendelea Tanzania bila shaka historia ya Afrika isingekuwa hii tunayoizungumza sasa.
Sekondari ya Butiama ni matokeo ya uwekezaji ‘wa ujanja ujanja’ uliofanywa na kampuni ya Meremeta iliyokuwa ikichimba dhahabu Buhemba. Ilijengwa kama sehemu ya mkataba wa kampuni hiyo kupata ruhusa ya kuvuta maji kutoka katika Bwawa la Kyarano lililopo katika vijiji vya Butiama, Rwamkoma na Bisarye. Sidhani kama kulijengwa vyumba vitatu vya madarasa!
Nimejituma kuwasilisha kilio hiki cha wana Butiama kwa Serikali na wadau wote wa elimu, nikiomba eneo hili litazamwe kwa jicho la huruma.
Wasomaji wanaweza kuhoji, kwanini Butiama na si kwingineko? Najitetea. Tulipowekewa msimamo na Afrika Kusini kuwa Watanzania lazima tupate viza kuingia nchini humo, tupo tuliohoji, “Haya ndiyo malipo ya ukombozi wetu kwa Waafrika Kusini?” Wenye akili wakaona swali la Watanzania halijibiki isipokuwa Afrika Kusini kufuta viza. Leo hakuna viza.
Natumia hoja hii kuhalalisha maombi yangu kwa Serikali na kwa wadau juu ya Butiama. Kama Mwalimu angeamua, nadhani leo, si shule tu, bali hata vyuo vikuu vyenye hadhi vingekuwa kama si Butiama, basi mkoani Mara!
Nadhani njia nzuri ya ‘kumlipa’ Mwalimu kwa wema wake aliolitendea taifa letu, si kuyapa jina lake majengo, barabara na vitu vingine; bali ni kuwakumbuka hawa Watyama kwa kuwawekea miundombinu mizuri ya elimu. Mwalimu alishasema kuwa ukitaka kwa kweli kumsaidia maskini ni kuhakikisha unampa mwanawe elimu.
Kuna taasisi nyingi zilizojengwa chini ya uongozi wa Mwalimu. Leo zimenona. Mashirika kama TANAPA, Posta, na mengine mengi yanaweza kabisa kutoa mchango wa ujenzi wa vyumba vya madarasa Butiama (shule za msingi na sekondari). Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inaweza kabisa kuona isaidie nini Butiama. Hoteli kubwa kubwa na kampuni zinazojihusisha na utalii kwa kutambua kuwa Mwalimu alisimama imara kulinda rasilimali hizi ambazo leo wanazifaidi, zinaweza kutoa michango ya hali na mali alimradi kuhakikisha Butiama walau inafaidi uadilifu wa Mwalimu. Viwanda vinavyosindika minofu vinajua Mwalimu angeweza kujimilikisha ziwa. Hakufanya hivyo. Kwa huruma vinaweza kuwasaidia watoto wa Butiama.
Kule Mererani kuna tanzanite. Wachimbaji wadogo kwa wakubwa wanajua bila msimamo wa Mwalimu, wasingepata hicho wanachopata sasa. Leo kuna mabilionea wengi. Hebu jitokezeni jamani mjenge japo vyumba viwili vya madarasa Butiama. Kufanya hivyo ni kumrejeshea asante kwa uadilifu wake kwa nchi na wananchi wake.
Buzwagi, North Mara, Bulyanhulu, Geita na kote kunakochimbwa dhahabu, wanajua hiyo dhahabu ipo kwa sababu Mwalimu alisema ibaki hapo. Nendeni Butiama muone shukrani gani muipeleke kwa hicho kizazi kilichoachwa na Mwalimu.
Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mkuu wa Mkoa wa Mara na mawaziri wenye dhamana ya elimu wanaweza kabisa kuitisha harambee ili zipatikane fedha za kuboresha elimu Butiama.
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambalo wazo la kuasisiwa kwake lilitolewa na mwana Butiama, Joseph Kizurira Nyerere, sidhani kama watasita kujenga vyumba vya madarasa kwa mfano lililouonyesha Mererani. Sioni kinachoshindikana.
Rais Magufuli, ni rais wa Tanzania nzima. Tanzania ni kubwa kweli kweli. Kumwambia aipendelee Butiama kunaweza kuwa si kumtendea haki yeye na wananchi wengine. Lakini kwa huruma yake, kama aliweza kujenga kilometa 11 za lami (Kyabakari-Butiama) ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Mwalimu, sioni ni kwa namna gani hivi vyumba vya madarasa asiweze.
Wasaidizi wakuu wa rais, kabla Rais Magufuli mwenyewe hajatamka neno, sioni kitu gani kinaweza kuwazuia kufika Butiama kujionea adha wanazopata watoto na walimu kwa lengo la kuziondoa. Wasisubiri kila kitu watiwe chaji na rais ndipo wagutuke.
Lakini lililo muhimu ni kwa viongozi na wadau mbalimbali kutumia ushawishi, kuwarejea wananchi kwa nia ya kuwahamasisha kujiletea maendeleo. Butiama hawana uwezo mkubwa kiuchumi, lakini naamini kwa kudunduliza wanaweza kufanya kitu cha maana. Mwalimu aliamini katika ‘kujitegemea’, lakini hakupinga kusaidiwa.
Nimeyasema haya ya elimu kwa sababu hii ndiyo silaha madhubuti ya kupambana na maadui wengine-ujinga na maradhi. Elimu ndiyo kila kitu. Nikipata ridhaa nitaomba wakubwa watazame huduma za afya na maji ambazo ni kero nyingine kubwa Butiama.
Narejea kuomba radhi kwa kuitumia safu hii kuwasilisha kilio cha watu ambao nina nasaba nao. Nimeshindwa kujizuia kwa sababu kwa kutofanya hivyo nitakuwa sehemu ya tatizo. Nimeyasema ya Butiama nikitambua kwa unyenyekevu mkubwa kuwa ndiyo hayo hayo yanayowapata Watanzania wa maeneo mengine. Kwa kuwa bado safu hii ipo naamini kwenye makala zijazo nitagusa hizo sehemu nyingine. Leo nimeanzia Butiama.
Naamini wadau, ikiwamo Serikali, wataitazama Butiama kwa jicho la huruma. Wanaweza kwenda mbali zaidi ili walau kuhakikisha kila kijiji katika kata hii kinakuwa na sekondari yake. Ilivyo sasa wanafunzi, wanatesema kwa kutembea hadi kilometa 20 kwa siku kwenda Sekondari ya Butiama kusoma. Kwa moyo wa huruma na utu yote haya yanawezekana. Naomba kuwasilisha.