Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100.

Mkulima huyo wa zamani wa karanga aliishi muda mrefu kuliko rais yeyote katika historia ambapo alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 100 mnamo Oktoba 2024.

Kituo cha Carter, ambacho kinatetea demokrasia na haki za binadamu kote duniani, kilisema alifariki Jumapili mchana nyumbani kwake huko Plains, Georgia.

Mwanademokrasia huyo alihudumu kama rais kuanzia mwaka 1977 hadi 1981, kipindi ambacho kilikumbwa na migogoro ya kiuchumi na kidiplomasia.

Baada ya kuondoka Ikulu ya White House na viwango vya chini vya idhini, sifa yake ilirejeshwa kupitia kazi ya kibinadamu ambayo ilimletea Tuzo ya Amani ya Nobel.

“Baba yangu alikuwa shujaa, sio kwangu tu bali kwa kila mtu anayeamini katika amani, haki za binadamu, na upendo usio na ubinafsi,” mwanawe, Chip Carter, alisema katika taarifa.

“Dunia ni familia yetu kwa sababu ya jinsi alivyoleta watu pamoja, na tunakushukuru kwa kuheshimu kumbukumbu yake kwa kuendelea kuishi imani hizi za pamoja.”

Carter – ambaye kabla ya kuwa rais alikuwa gavana wa Georgia, luteni katika jeshi la wanamaji la Marekani na mkulima – ameacha watoto wake wanne, wajukuu 11 na vitukuu 14.

Mkewe, Rosalynn, ambaye alikuwa walioana miaka 77, alikufa mnamo Novemba 2023.