Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, leo tarehe 11 Machi, 2025 amefungua Mkutano wa Kibunge wakati wa Mkutano wa 69 wa Kamisheni ya Hadhi ya Mwanamke ya Umoja wa Mataifa (UNCSW) unaoendelea katika Ukumbi wa Baraza la Trusteeship, Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.

Mkutano huo unajadili taarifa ya Utekelezaji wa Miaka 30 ya Azimio la Beijing na Mpango Mkakati wake wa mwaka 1995, ambao ulilenga kuimarisha usawa wa kijinsia na ushiriki wa Wanawake katika Uongozi na maamuzi. Wakati wa kuanzishwa kwake, uwakilishi wa Wanawake katika Mabunge Duniani ulikuwa na wastani wa asilimia 11.5 lakini hadi sasa umefikia asilimia 27.2, ikionesha hatua kubwa katika usawa wa kijinsia kwenye siasa.

Aidha, Dkt. Tulia amezindua rasmi Ramani ya Uwakilishi wa Wanawake katika masuala ya Kisiasa Duniani, iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na UN Women. Ramani hii ni nyenzo muhimu ya kutathmini maendeleo na changamoto zilizopo katika kuhakikisha ushiriki wa Wanawake katika Uongozi wa kisiasa Duniani kote.