Rais Kais Saied wa Tunisia amemfuta kazi waziri mkuu wake, Ahmed Hachani, bila kutoa maelezo yoyote na badala yake kumteuwa waziri wake wa masuala ya kijamii, Kamel Madouri, kuchukuwa wadhifa huo.
Kupitia mitandao ya kijamii cha ofisi yake, Saied anaonekana kwenye picha akipeana mkono na Madouri, na chini ya picha hiyo kuna taarifa fupi inayosema kuwa rais huyo ameamua kumpa Madouri jukumu la kuongoza serikali, akichukuwa nafasi ya Hachani.
Hachani aliteuliwa tarehe 1 Agosti mwaka jana, akichukuwa nafasi ya Najla Bouden, ambaye pia aliondolewa bila maelezo rasmi. Madouri aliteuliwa kuwa waziri wa masuala ya kijamii mwezi Mei mwaka huu.
Rais Kais Saied, mwenye umri wa miaka 66, alichaguliwa kidemokrasia mwaka 2019, lakini mwaka 2021 alianzisha kampeni ya kujikusanyia madaraka yote mikononi mwake, na sasa anawania kuendelea kusalia madarakani kupitia uchaguzi wa Oktoba 6 mwaka huu.