Rais wa Benki ya Dunia (WBG), Bw. Ajay Banga amewasili nchini kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati utakaofanyika tarehe 27 hadi 28 Januari 2025.Mkutano huo utakaofanyika katika ukumbi wa Mikutano Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam Bw.Banga amepokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Cosato Chumi kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.Aidha katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu Mwamba, Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe.Dkt.Elsie Kanza, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Bw. Nathan Belete pamoja na viongozi wa Serikali.
Lengo la Mkutano huu ni kuwakutanisha Wakuu wa Nchi za Afrika na wadau muhimu wa sekta ya nishati ili kujadili namna ya upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu na endelevu kwa watu milioni 300 barani Afrika ifikapo mwaka 2030.
Mbali na Rais wa Benki ya Dunia, Viongozi wengine Wakuu wa Nchi na Mashirikia waliowasili nchini hadi sasa ni Rais wa Jamhuri ya Sierra Leone, Mheshimiwa Julius Maada Bio na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina.
Mkutano huu unatarajia kusaini Mpango Mahsusi wa Nishati Afrika aidha kusaini Awamu ya kwanza ya Mipango ya Kitaifa ya Nishati kwa kipindi cha miaka mitano 2025 – 2030.