Rais Tserese Khama Ian Khama

Na Mkinga Mkinga

Aliyekuwa Gaborone, Botswana.

Kusini mwa jangwa la Sahara, pamezoeleka kuwa na majangwa kadhaa, ukienda nchini Namibia, utakutana na jangwa la Namib ambalo linakwenda kuungana na jangwa jingine la Kalahari, lililoko nchini Botswana.

Nimepata fursa ya ‘kupita’ Botswana mara kadhaa, lakini kipindi hiki nimepata fursa adhimu ya kuitembelea Botswana, kwa siku kadhaa, kutokana na shughuli za kikazi. Hivyo nimepata fursa za kujifunza na kujionea mambo kadhaa yanayoendelea katika nchi hii ambayo ndiyo Makao Makuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Katika mazungumzo ya kawaida nchini Tanzania na ikatokea mtu mmoja akagusia suala la nchi za Afrika zinavyonufaika na madini yake, basi mmoja wa walioko kwenye mjadala huo ataitaja nchi ya Botswana, yenye Makao Makuu, hapa jijini Gaborone (wenyeji wakipaita Haborone).

Kiu hiyo inanifanya nidadisi zaidi kwa wenyeji wangu hapa Gaborone, wameyafikia namna gani mafanikio hayo makubwa katika sekta ya madini, hasa ikizingatiwa kumekuwepo na dhana kwamba Waafrika si wazuri katika mapatano ya kimkataba.

Maswali yangu hayo, wanawafanya wenyeji kuniambia picha kubwa iliyoko nyuma ya mafanikio. Katika mafanikio hayo anatajwa Luteni Jenerali Khama, ambaye pia amekuwa Rais wa Botswana katika vipindi viwili.

Moja kati ya habari kubwa katika viunga vya jijini la Gaborone, ni Rais Tserese Khama Ian Khama, kumaliza mhula wake wa pili wa utawala na ameondoka ofisini rasmi, siku ya Pasaka, April Mosi. Rais Khama, ambaye ni mtoto wa mwasisi wa taifa la Botswana, Sir Tserese Khama, amehudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka kumi.

Kabla ya hapo alikuwa Makamu wa Rais, huku Rais wake akiwa ni Mzee Festus Mogae, Rais huyo ambaye kabla ya kuingia katika siasa alikuwa ni mmoja wa majenerali wav yeo vya juu kabisa katika jeshi la Botswana, alihudumu katika nafasi ya Makamu wa Rais, kwa kipindi cha miaka kumi. Hivyo amekuwa katika uongozi wa juu wa Botswana kwa miaka 20.

Luteni Jenerali Tserese Khama Ian Khama ni nani?

Ian Khama ni mtoto wa kwanza wa kiume na mtoto wa pili kwa Sir Tserese Khama, ambaye ndiye Baba wa Taifa la Botswana. Baba yake ameiongoza Botswana tangu mwaka 1966 ilipopata uhuru hadi 1980.

Alizaliwa Februari 27, 1953, Chertsey, Surrey nchini Uingereza, Mama yake Tserese Khama Ian Khama, anaitwa Ruth Williams, ambaye mama raia wa Uingereza.

Luteni Jenerali Ian Khama ambaye pia kitaaluma ni rubani wa ndege za kijeshi, alizaliwa Chertsey, Surrey nchini Uingereza, katika kipindi ambacho baba yake (Sir Tserese Khama) alikuwa akiishi uhamishoni nchini Uingereza, kutokana na ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiendelea nchini humo, hasa ikizingatiwa alikuwa amemwoa mwanamke wa kizungu.

Rais Ian Khama, anatoka katika familia ya watawala, hata babu yake Sekgoma II alikuwa ni chifu wa kabila la Bamangwato kati ya mwaka 1869-1925, Rais Ian Khama ni kitukuu cha chifu Khama wa III aliyehudumu kati ya mwaka 1837-1923. Kwa mujibu wa Watswana jina la Tserese maana yake ni kichuguu.

Jina la Tserese alipewa baba yake na Ian Khama, baada ya kusameheana na baba yake, na baada ya msamaha huo aliamini katika kufanikiwa na hata baada ya kifo cha baba yake mwaka 1925. Hivyo baada ya Tserese kuzaa mtoto wa kiume, aliamua kumwita Tserese Khama Ian Khama kama sehemu ya kumbukumbu adhimu katika maisha yake.

Rais Khama anao ndugu zake, Tshekedi Khama II, ambaye alipewa jina la baba yao mkubwa, ambaye alikuwa mlezi wa Tserese Khama.

Uongozi wake

Waswana wanamuelezea Rais Ian Khama, kama mmoja wa viongozi waliosaidia sana nchi hiyo kupiga hatua kubwa za kiuchumi pamoja na kusimamia utangamano wa taifa lao, huku akitumia muda mwingi kushughulikia mambo ya wananchi.

Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa wananchi wa Botswana, Tsepiso Nkhlung amesema, yeye atamkumbuka Rais Ian Khama, mmoja wa Marais wa nchi hiyo aliyeifanya sarafu ya Botswana (Pula) kuwa na thamani kubwa katika ukanda huu wa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara.

Ukilinganisha na fedha ya Tanzania, Pula moja ya Botswana na sawa na Sh185 ya Tanzania. Waswana wanamwona kiongozi huyo aliyemaliza muda wake kama mmoja wa watu wa kukumbukwa katika historia ya nchi hiyo.

Namna alivyoingia katika siasa

Rais Khama ambaye amelitumikia jeshi la Botswana kama mmoja wa majerali wa juu kabisa, alitangaza kustaafu kulitumikia jeshi hilo tarehe 16 Disemba, mwaka 1997, huku akijipatia miezi mitatu ya kukamilisha azma hiyo, hadi Machi 31, 1998 tarehe ambayo alivua rasmi magwanga ya kijeshi.

Wachunguzi wa mambo nchini humo wanasema huo ulikuwa ni mkakati uliofanywa na Rais Mstaafu wa Botswana, Festus Mogae, maana siku yeye anajiachia ngazi jeshini ndiyo siku ambayo pia Rais mtangulizi wa Mogae, Ketumire Masire, alikiwa anang’atuka madarakani kwa mujibu wa katiba yay a nchi hiyo.

Botswana wanao utaratibu wa kikatiba, kwamba Rais anapomaliza muda wake basi Makamu wa Rais anapanda na kuwa Rais katika kipindi cha mwaka mmoja huku wakisubiri uchaguzi mkuu. Hivyo Makamu wa Rais wa kipindi cha Ketumire Masire, mzee Festus Mogae, alipanda na kuwa Rais wa Botswana.

Kitendo cha Luteni Jenerali, Tserese Khama Ian Khama, kujiuzulu nafasi yake jeshini kikaanza kuleta minong’ono ya chini chini kwa wafuatiliaji wa siasa za Botswana, kwamba huenda atateuliwa na Festus Mogae, kuwa Makamu wa Rais.

Kama wengi walivyotaraji, Aprili Mos, 1998, siku ambayo Rais Festus Mogae alichukua ofisi, alimtangaza Luteni Jenerali Tserese Khama Ian Khama kuwa Makamu wa Rais wa Botswana, nafasi aliyohudumu kwa miaka 10, wakati Rais Khama anateuliwa hakuwa hata mbunge, hivyo kwa mujibu wa katiba ya Botswana, hakutakiwa kushika madaraka hayo mara moja.

Julai 1998, palitokea uchaguzi mdogo katika jimbo la Serowe Kaskazini, jimbo ambalo ni asili ya familia ya Rais Khama, alipata ushindi wa kishindo kwa kupata kura 2986 dhidi ya mpinzani wake aliyeambulia kura 86 tu, Luteni Jenerali, akapata kiti ndani ya Bunge na hivyo kuapishwa kuwa Makamu wa Rais, Julai 13, 1998.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1999, chama tawala cha Botswana Democratic Party (BDP) kikashinda uchaguzi huo na Tserese Khama Ian Khama, akaendelea na madaraka yake ya Makamu wa Rais na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Utawala, baada ya mwaka mmoja (2000), Rais Festus Mogae, alimpatia Khama likizo ya mwaka mmoja, uamuzi ambao ulipigiwa kelele na chama cha upinzani cha Botswana Congress Party pamoja na baraza la mashirika yasiyokuwa ya kiserikali nchini Botswana.

Makala hii imeandikwa chini ya udhamini wa wakfu wa vyombo vya habari Tanzania (TMF).