ZANZIBAR

Na Mwandishi Maalumu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,
amesema uhusiano na ushirikiano kati ya
Malawi na Zanzibar una historia ya muda
mrefu, hivyo kuna haja ya kuuendeleza na
kushirikiana katika sekta za maendeleo
ikiwamo utalii.
Dk. Shein amesema hayo Ikulu mjini
Zanzibar mwishoni mwa wiki
alipozungumza na Balozi wa Malawi nchini
Tanzania, Hawa Ndilowe, aliyefika Ikulu
kuaga baada ya kumaliza muda wake wa
kazi hapa nchini.

Dk. Shein alimweleza Balozi Ndilowe kuwa
Zanzibar na Malawi zina mambo mengi ya
kushirikiana yanayoweza kuleta mafanikio
makubwa kwa pande zote.
Amesema uhusiano na ushirikiano wa
kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Malawi
ni njia mojawapo kubwa itakayoimarisha
sekta ya utalii, ambapo wananchi wa pande
zote watapata fursa ya kuzuru pande zote.
Amemweleza balozi huyo kuwa Zanzibar na
Malawi zina mambo mengi ya kujifunza,
hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar imeanza
kupata mafanikio makubwa katika sekta
hiyo.
Uhusiano huo wa kihistoria uliazishwa na
waasisi wa nchi mbili, mzee Abeid Aman
Karume, ambaye alitembelea Malawi
mwaka 1958 na Dk. Kamuzu Banda
aliyefika Zanzibar mwaka 1959.
Viongozi hao walijenga urafiki kupitia vyama
vyao vya siasa vya Afro Shiraz (ASP) kwa
upande wa Zanzibar na Chama cha Malawi
Congress (MCP) cha Malawi.
Kwa upande wa elimu, Dk. Shein amesema
ipo haja ya kuendeleza ushirikiano kati ya
vyuo vikuu vya Zanzibar, kikiwamo Chuo
Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)
sambamba na kushirikiana katika sekta ya

michezo na utamaduni.
Naye Balozi Ndilowe amemweleza Dk.
Shein kuwa Malawi itaendelea na dhamira
yake ya kuimarisha uhusiano wa kidugu
uliopo kati yake na Tanzania, ambao
umejengwa kwa muda mrefu.
Amempongeza Rais Dk. Shein kwa
ushirikiano mkubwa aliopata Zanzibar katika
kipindi chake chote alichofanya kazi
akiiwakilisha Malawi.