SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA

MHESHIMIWA DKT. SAMIA SULUHU HASSAN,

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

KWA WATANZANIA – TAREHE 31 DESEMBA 2022

Ndugu Wananchi na Watanzania wenzangu;

NAWASALIMU KWA JINA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA! 

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwingi wa Rehema kwa kutujaalia baadhi yetu kuiona siku ya leo tunapouaga mwaka wa 2022 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2023.

Pamoja na changamoto tulizopitia mwaka 2022, nawaomba tusikate tamaa, bali, changamoto zozote zile zitupe nguvu na tuutazame mwaka mpya kwa matumaini makubwa mbele yetu. Kila mmoja wetu ajidhatiti na awe na uthubutu wa kusimama tena kukabiliana nazo. 

Ni katika mustakabali na utamaduni huo wa kutokata tamaa na kupambana, ndio ndoto na matumaini ya Taifa letu na Wananchi wake yamekuwa yakihuishwa mwaka hadi mwaka. 

Natumia fursa hii, kumuomba Mwenyezi Mungu Mkarimu atuondolee kila aina ya dhiki, atupe faraja na furaha; na awalaze mahali pema peponi wapendwa wetu wote waliokwisha kutangulia katika ufalme wa milele.

Aidha, napenda kuwapongeza wale wote waliopata mafanikio ya kimaisha; nikimuomba Mwenyezi Mungu Muweza atujaalie mafanikio zaidi katika mwaka ujao 2023. Amina.

Ndugu Wananchi;

Kwa ujumla inafurahisha kuwa, kama Taifa, tunauaga mwaka 2022 tukiwa tumeendeleza mshikamano wetu, kuilinda amani na kupiga hatua kubwa za maendeleo ya nchi yetu. 

Pamoja na mafanikio hayo, nitumie fursa hii kuwakumbusha viongozi wenzangu tuliobeba jukumu zito la kuhudumia Taifa hili, kwamba Watanzania wana matumani makubwa kwetu, na kwamba tunatarajiwa kuendelea kuliongoza Taifa hili kwa juhudi, uadilifu na kwa misingi ya haki na sheria. Hivyo basi, mwaka 2023 uizidi miaka iliyopita kwa kasi kubwa zaidi ya utendaji kazi, na kudumisha umoja na amani kwa maendeleo zaidi.  

Ndugu Wananchi;

Hapana shaka kwamba kila mwisho unaanzisha mwanzo mpya, mwisho wa 2022 ndio mwanzo wa 2023. Hakuna anaeweza kuurudisha muda nyuma na akarekebisha yaliyoharibika, hivyo basi, tufanyie kazi sasa changamoto zilizotukwaza 2022, ili tujenge mustakabali mzuri mbele yetu.

Mwaka mpya ni kitabu kisicho na maandishi, kalamu ya kuandika mema au mabaya ndani ya kitabu hicho iko mikononi mwa kila mmoja wetu, niwasihi kutumia vyema wakati huu, kujiandikia hadithi njema ya mafanikio ya baadae. Serikali kwa upande wake, itaendelea kufanya kila litalowezekana ili mwaka wa 2023 kwa uwezo wa Molla uwe wa mafanikio makubwa zaidi. 

Wito wangu kwenu wananchi ni kuwa, tuendelee kushikamana, tuzidi kuupa nguvu umoja wetu, tutunze amani na utulivu wa nchi yetu, ili tuwe na maisha ya furaha na maendeleo ya juu zaidi. Mwisho kabisa, niwaombe tujitahidi kadri tuwezavyo kuepuka misiba isiyo ya lazima katika sherehe hizi za mwisho na mwanzo wa mwaka.
Nimalizie kwa kurudia kuwatakia kila la kheri, afya njema na mafanikio zaidi ya kiuchumi na kijamii kwa kila mmoja wetu na Taifa zima. Tuwe na mwaka mwema 2023.  

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA