Na Deodatus Balile
Wiki iliyopita nilihitimisha makala yangu kwa aya hizi: “Sitanii, ukurasa umekuwa finyu. Hili la miundombinu nitalidadavua zaidi wiki ijayo. Tunatumia wastani wa Sh trilioni 7 kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi kwa mwaka. Tunaweza kuachana na utumwa huu tukipenda. Tunayo neema katika nchi yetu.
“Wakati Waarabu wanayo mafuta, sisi hapa kwetu tuna gesi kwa viwango vya Trillion Cubic Feet (TCF) 57 iliyogunduliwa, na bado ipo nyingi haijagunduliwa. Hiki ni kiwango tunachoweza kuchimba kwa hadi miaka 600 ijayo. Je, unafahamu kuwa malori ya Dangote zaidi ya 1,000 yote yanatumia gesi badala ya mafuta? Je, Tanzania hatuwezi kwenda huko? Usikose makala ya wiki ijayo.”
Ni kutokana na ahadi yangu hii, leo nazungumzia tena suala la mafuta na gesi. Bei ya mafuta haishikiki kwa sasa. Kuna suala la miundombinu hapa ambalo ni changamoto. Katika makala ya wiki iliyopita, nilionyesha kuwa meli inashusha mafuta kwa siku 8 hadi 10, mafuta ambayo ni wastani wa tani 120. Hapa mimi si injinia, ila tunaweza kuongeza ukubwa wa mabomba na idadi ya mita za kupima mafuta, kisha tukaongeza kasi ya upakuaji.
Kubwa ninalotaka kulizungumza kwa kina leo ni gesi asilia. Hapo juu nimeonyesha kuwa Tanzania imegundua gesi ya ujazo kwa kipimo cha TCF 57. Kwa mujibu wa wataalamu, gesi hii inaweza kuchimbwa kwa hadi miaka 600. Hiki ni kiasi kikubwa mno cha gesi.
Wataalamu hawa hawa wanatwambia tukiamua kutumia gesi kwenye magari, tutapunguza matumizi ya mafuta kwa asilimia 50. Kwanza, gesi haitoi moshi, ikichomwa inaungua yote, hivyo ni rafiki kwa mazingira. Pia inapatikana hapa nchini.
Sitanii, inawezekana wataalamu wetu hawajakaa chini kupiga hesabu iwapo magari yote hapa nchini yakitumia gesi nchi itapata faida kiasi gani. Kuna nafuu kubwa itaingia katika uchumi wa taifa hili. Kabla sijaingia kwenye unafuu, naomba nizungumzie gharama za kubadili mfumo kutoka petroli au dizeli kwenda kwenye gesi.
Kwa magari madogo, mfano kama IST ninalolitumia, naambiwa nikiweka gesi ya Sh 25,000 nakwenda Morogoro na kurudi Dar es Salaam. Hata hivyo, kikwazo ni gharama ya kubadili mfumo. Gari moja kubadili mfumo inagharimu si chini ya Sh milioni 2.
Sitanii, mimi ninalo suluhisho la tatizo hili ambalo wakubwa wanaweza kulichukua na likawa na faida lukuki kama nitakavyoainisha hapa chini. Njia ya kwanza ni serikali kukubali kufanya uwekezaji wa muda mrefu. Kodi inayotozwa kwa gari kama IST kwa sasa ni kuanzia Sh milioni 5 kwenda juu ukilinunua kutoka Japan.
Kwa nia ya kufanya uwekezaji, nashauri serikali irekebishe kanuni katika bajeti zijazo, na iweke utaratibu kwamba magari yote yatakayokuja kutumika hapa nchini yabadili mfumo uwe wa kutumia gesi badala ya mafuta, yatapunguziwa kodi kwa asilimia 50.
Hapa napendekeza kuwa gari ukiliagiza likatoka Japan na kuingia hapa nchini likiwa na mfumo wa gesi au likatoka bandarini na kwenda kwenye kiwanda cha kurekebishia hapa nchini likarekebishwa, basi ukitoa uthibitisho usiotiliwa shaka, unalipa kodi nusu.
Hii ina maana kama kodi ilikuwa ni Sh milioni 5, basi utalipa Sh milioni 2.5. Najua hapa kuna watu wataibuka haraka na kusema serikali itapoteza mapato kwa asilimia 50. Tulieni, si kweli. Hiyo asilimia 50 itakayotumika kurekebisha gari, ni wazi anayeipokea naye atalipa kodi si chini ya asilimia 18 ya VAT mara tu anapoipokea hiyo fedha.
Huyu anayerekebisha magari atalipa kodi nyingine kama SDL, PEYE na mwisho wa mwaka akipata faida atalipa Kodi ya Mashirika (Corporate Tax). Si hilo tu, viwanda vya kurekebisha magari kuwa ya gesi vitaajiri wafanyakazi, nao watalipwa mishahara. Hizi ni faida za moja kwa moja.
Viwanda hivi vikiishakuwa na utaalamu wa kutosha, hata nchi zinazotuzunguka mara moja wataanza kuleta magari yao kwenye viwanda hivi, ambapo teknolojia itaendelea kukua na tutakuwa tumetengeneza ajira na mtaji mkubwa kwa taifa letu.
Kwa lugha nyingine, ile asilimia 50 ya kodi aliyosamehewa aliyeleta gari, inakuwa ni mtaji kwa hivyo viwanda utakaozalisha fedha nyingi zaidi. Inahitaji kufikiri kwa kina kuliona hili.
Sitanii, faida ya pili ya moja kwa moja itakwenda kwa serikali. Magari yatakayoingia yote yakiishakarabatiwa na kuwa ya gesi, na hapa ieleweke hadi malori yanatumia gesi kama ilivyo kwa malori ya Dangote, Tanzania itakuwa na uhakika wa soko la gesi asilia.
Kwa sasa tunatumia wastani wa Sh trilioni 7 kwa mwaka kuagiza mafuta. Ikiwa tutabadili nusu ya magari yakatumia gesi, ina maana tutatumia Sh trilioni 3.5 kwa mwaka kuagiza mafuta. Hizi Sh trilioni 3.5 zinazosalia, wenye magari watatumia Sh trilioni 2 kununua gesi kwa ajili ya magari yao, na Sh trilioni 1.5 zitabaki mifukoni mwa wananchi.
Hapa pande zote zitakuwa zimepata. Serikali itakuwa na chanzo kipya cha mapato kwenye bajeti kinachoingiza Sh trilioni 2 au zaidi na wananchi watasalia na Sh trilioni 1.5 mifukoni mwao, hivyo tutajenga matajiri kwa kasi zaidi.
Sitanii, hesabu za mafuta zinatisha. Leo kwa mfano natumia wastani wa lita 42 kwa wiki kwa kuwa nina hili gari dogo la injini yenye CC 1290, maana wenye njini za kuanzia CC 1800 wanatumia hadi lita 80 kwa wiki. Nikitumia mfano wetu akina pangu pakavu, ukinunua wastani wa lita moja ya mafuta kwa Sh 2,820, inakuwa ni sawa na Sh 118,440 kwa wiki. Ukizidisha kwa wiki 52 kwa maana kwa mwaka ni Sh 6,158,880. Nafahamu watu wengi hamjapiga hesabu juu ya matumizi ya mafuta ya magari yenu kwa mwaka mnatumia kiasi gani, hivyo hesabu hizi zinaweza kuwashtua kidogo.
Na pengine hamzihisi kwa kuwa kila siku unakwenda kituo cha mafuta unajaza Sh 10,000 au Sh 15,000. Ukiwa nazo unajaza Sh 30,000 na ukibahatika kutunza risiti, ndipo utafahamu fedha nyingi kiasi gani unatumia kwenye mafuta ya gari. Na hapo hujazungumzia matengenezo ya gari, maana injini inayotumia gesi inadumu miaka mingi kuliko ya petroli na dizeli.
Sitanii, tukichukulia wastani wa Sh 6,000,000 za kuhudumia mafuta ya gari lako dogo kwa mwaka, ukikaa na gari kwa miaka 5, sekta ya mafuta unakuwa umewachangia wastani wa Sh milioni 30 kwa muda huo hadi gari linachakaa na unaanza kulichoka.
Ingekuwa gesi, ungekuwa umetumia wastani wa Sh milioni 3 kwa mwaka, kwani gesi inatumika chini ya nusu ya matumizi ya petroli au dizeli. Hivyo ina maana kwa miaka 5 ungekuwa umetumia wastani wa Sh milioni 15. Jambo zuri zaidi, hizi Sh milioni 3 kwa mwaka au Sh milioni 15 kwa miaka mitano ukizitumia kwenye gesi, zinakuwa zimeingia katika uchumi wa Tanzania, si kusafirishwa kwenda Uarabuni kununua mafuta. Sasa piga hesabu ya magari 8,000 hadi 14,000 yanayotembea mitaani yakijaza gesi kwa hesabu hizo nchi itapata fedha kiasi gani?
Sitanii, hapa ndipo ilipolala faida ya muda mrefu. Nchi jirani zikiona tunaitumia teknolojia hii, zitakuja kuomba tuwauzie gesi. Tutajenga mabomba ya gesi kwenda katika nchi zao, tutauza gesi, tutawatengenezea magari yao yatumie gesi na tutapata fedha za kigeni. Mradi huu pekee, unatosha kutuhamisha kutoka katika nchi inayotegemea wafadhili, kuwa taifa la kufadhili majirani zetu.
Kwa sasa tuna vituo vitatu vinavyouza gesi kwa magari yanayotumia gesi, ambavyo vipo kwa Dangote Mtwara, kingine Ubungo na kimoja Tazara. Hapa napendekeza kubadili masharti ya Kanuni za leseni ya vituo vya mafuta zinazotolewa na EWURA. Kanuni imtake kila mwenye kituo cha mafuta nchini auze na gesi asilia iliyoshindiliwa (Compressed Natural Gas – CNG).
Kwa ubunifu huu, nakuhakikishia baada ya miaka 20, nchi yetu itaondokana na kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi, tutaokoa fedha nyingi za kigeni, serikali itabakiza fedha nchini, gesi yetu itatuzalishia matrilioni ya fedha na uchumi wetu utakua kwa kasi ya aina yake. Tusiogope, tulijaribu wazo hili. Kazi kwenu mawaziri kulichakata. Mungu ibariki Tanzania.