Baadhi ya Wafanyakazi wakiwa katika Sherehe ya Mei Mosi ambazo Kitaifa zimefanyika katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro tarehe 01 Mei, 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wafanyakazi wakati wa Sherehe ya Mei Mosi ambazo Kitaifa zimefanyika katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro tarehe 01 Mei, 2023.

………………………………………………………………………………..

Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa wafanyakazi nchini wana mchango mkubwa katika kusadia ustahimilivu wa nchi yeyote ile duniani.

Akizungumza leo Mei 1, 2023 mkoani Morogoro katika Sherehe za Siku ya Wafanyakazi, Mhe. Rais Dkt. Samia alisema kuwa maadhimisho ya sherehe za Mei Mosi ni siku ya kutambua mchango wa wafanyakazi kwenye uchumi na ustawi wa taifa.

“Ni siku ya kuonesha heshima na kutoa shukrani kwa wafanyakazi kwa kazi kubwa wanayofanya ndani ya taifa. Kujitoa kwetu wafanyakazi kwa bidii, kusaidiana kujenga taifa linalojitambua na kila taifa linavyokuwa kuna nguvu ya wafanyakazi kwa kiasi kikubwa, kwa hiyo wafanyakazi lazima tujipongeze, umadhubuti na ustawi wa taifa hili ni kwa sababu sisi wafanyakazi tunafanyakazi kubwa ya kulijenga kwa hiyo nguvu zetu tulizoweka katika taifa hili zichukuliwe kwa uzito mkubwa”. Alisema Rais Samia.

Aliongeza kuwa kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu inayosema kuwa Mishahara Bora na Ajira za Staha ni nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi na wakati ni Sasa inalenga kuhimiza uboreshaji wa maisha ya wafanyakazi kwa upana wake, hata hivyo na yeye aliongeza kauli mbiu inayosema kuwa Uadilifu na Uweledi kazini ndio chimbuko la Maisha Bora kwa Wafanyakazi hivyo pamoja na kudai maisha bora lakini uadilifu na uwajibikaji kazini ndio utaleta maisha bora kwa wafanyakazi.

Aidha,  Rais  Samia alibainisha  kuwa Serikali itaendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kazi serikalini  na katika sekta binafsi ili kupatikana ajira zenye usalama na ajira za staha kwa wote.