Rais Samia amevitaka vyombo vya habari kuhamasisha kupokea ujuzi mpya, taarifa za
maendeleo ya kiteknolojia katika sekta za uzalishaji na maendeleo ya jamii, vifichue maovu na kutowajibika kunakofanywa na
Watumishi na Watendaji wa Serikali, vinatoa mrejesho wa hisia na mtazamo wa wananchi kwa Serikali yao, na kwa ujumla, vinafanya kazi ya kuelimisha na kukuza demokrasia.

Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa masuala haya ndiyo yanayoifanya Serikali kujenga na kuimarisha uhusiano mwema na vyombo vya habari.


Vyombo vya habari sio mshindani wa Serikali bali ni mdau na mshiriki muhimu katika yanayotendwa na Serikali hivyo, Serikali itaendelea kuweka mifumo mizuri ya Kisera, Kisheria na Kitaasisi, katika kuimarisha uhuru na mazingira ya kazi kwa vyombo vya habari.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Moses Nnauye kabla ya kufungua Kongamano la Pili la Maendeleo ya Sekta ya Habari katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Juni, 2024.