Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
 
Kodi, kodi, kodi…Nimetaja neno kodi mara tatu mwanzoni mwa makala hii. Nimetaja kodi kutokana na matukio makuu matatu ndani ya wiki iliyopita. Tukio la kwanza ni mgomo wa wafanyabiashara ulioanzia Kariakoo, Dar es Salaam ukasambaa katika mikoa mbalimbali nchini.

Tukio la pili ni mdahalo wa wagombea Uwaziri Mkuu nchini Uingereza, ambao ni Waziri Mkuu wa sasa anayetokana na Chama cha Conservative, Rish Sunaki na kiongozi wa Chama cha Labour, Sir Keir Starmer.

Tukio la tatu ni mjadala kati ya wagombea urais wa Marekani; Rais wa sasa Joe Biden na mpinzani wake, mgombea wa Republican; Donald Trump. Matukio yote haya, mjadala mkubwa uliotawala ni wa kodi. Matukio haya yote yametokea wiki iliyopita.

Juni 18, 2024 tulikuwa na Kongamano la Wadau wa Habari pale Mlimani City, Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ndiye alikuwa mgeni rasmi, alitupa changamoto waandishi wa habari; anataka kuona habari za uchambuzi zimsaidie kufanya uamuzi.

Sitanii, ni kutokana na hilo, leo nimeamua kufanya uchambuzi wa kodi na jinsi kodi ilivyo sumu au mbolea katika uchumi wa nchi yoyote iwayo. Jambo moja niliseme mapema. Kodi ni kichocheo cha uzalishaji, lakini kodi pia ni chanzo cha kukatisha tamaa wazalishaji. Suala la pili, naomba niseme kodi ni taaluma, lakini usimamizi wa kodi unahitaji ujuzi na maarifa zaidi ya taaluma.

Ndiyo maana kwa mfano, wapo watu wengi waliosomea sheria, nieleweke si kusoma sheria, kusomea sheria, lakini si mawakili. Tunao watu wengi wanaosoma sheria, bila kusomea sheria wakadhani wao ni mawakili, kumbe ni wanasheria tu au msomaji wa andiko la kisheria. Kumbe vivyo hivyo, mtu kusoma uhasibu, ugavi au sheria ya kodi, haimpi ujuzi wa kuwa mkusanya kodi mzuri.

Sitanii, wafanyabiashara wetu wamegoma wiki iliyopita hadi serikali ikaingilia kati. Sitaki kuingia kwa undani katika eneo hilo, maana naamini wengi tunafahamu kilichotokea na ilikoishia, ila kubwa nililojifunza ni moja ya sentensi za wafanyabiashara kuwa kodi ni nyingi, ni utiriri. Wanataka ziwepo kodi mbili zinazofahamika.

Hapa naomba niwasilishe ombi rasmi kwa Mhe. Rais Samia kuwa nakuomba uunde Kikosi Kazi cha Kuchunguza Kodi za nchi hii. Kuna baadhi ya kodi ni za kichaa. Mfano kuna kodi inaitwa Service Levy (Kodi ya Huduma).Kodi hii inatozwa kwa kiwango cha asilimia 0.3 ya mapato ghafi. Hii maana yake ni kuwa mauzo yote kabla ya kutoa matumizi, unapaswa kulipa asilimia 30 ya mauzo.

Waliotunga sheria hii hawakujiuliza ukweli kwamba biashara haina faida ya kiasi hiki. Nitoe mfano wa saruji. Kiwandani mfuko unauzwa Sh 16,000. Rejareja mfuko wa saruji unauzwa Sh 17,000.

Asilimia 30 ya Sh 17,000 ni Sh 5,100. Hii ina maana mtu akinunua saruji Sh 16,000 akaiuza Sh 17,000, akilipa kodi moja tu ya huduma Sh 5,100, mtaji wake unakatika na kubaki Sh 11,900. Sijui unanielewa? Akitaka kununua mfuko mwinginne akauuze, inabidi akakope Sh 4,100 aongezee kwenye mtaji wa Sh 11,900 uliosalia, ndipo afikishe Sh 16,000 anunue mfuko mpya wa kuuza, kisha arejee mchezo wa kupoteza mtaji. Kodi hii inafilisi biashara.

Sitanii, zipo kodi nyingi, wala sitazitaja hapa, ila nafikiri wengi tunazifahamu ikiwamo Kodi ya Makampuni asilimia 30 ya faida, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) asilimia 18, Kodi ya Lipa Kadiri Unavyopata inaanzia asilimia 9 hadi 30 kwa wafanyakazi, ila uhalisia zinatokana na mwajiri. Kodi ya Maendeleo ya Ujuzi (SDL), Bima ya Afya kuna kodi zaidi ya 30, ambazo ukilipa kwa utiifu zinafikia asilimia 230 ya mtaji. Sijui naeleweka?

Zinatolewa hoja dhaifu kuwa kodi hizi hazilipi mfanyabiashara, bali zinatokana na ununuzi wa wateja na kwa nchi nyingine kodi ziko chini kwa sababu tayari wao ni matajiri. Hapa ndipo tunapofeli. Unahitaji kuwa na mtaji mkubwa kuwa katika uzalishaji. Leo viwanda vya vinywaji, naambiwa vingi vinafunga si kwa kupenda, bali kutokana na utitiri wa kodi.

Nawafahamu wafanyabiashara nguli, ambalo ndani ya miezi miwili iliyopita akaunti zao zimekamatwa na TRA wakiwadai kodi za hadi miaka 17 iliyopita. Kwa mawazo finyu au kuwaza kijamaa, tunaweza kusema ni haki walipe, kumbe tunaua biashara na kuua ajira na mapato tarajiwa.
Nimesema kuna matukio matatu. Nimesikiliza midahalo ya wagombea wa Uingereza na Marekani, ambayo ni mawili ninayoyajumuisha kwenye mgomo wa wafanyabiashara hapa nchini na mfumo wa kodi za utitiri hapa kwetu.

Ukimsikiliza Sunaki na Trump, wanasema ukitaka kuua uchumi ongeza kodi. Kodi ikiwa kubwa, unakuwa na uhakika wa kuua uchumi. Kodi ikiwa ndogo unakuwa na uhakika wa kukuza uchumi.

Sitanii, leo naomba niwape mfano mdogo tu. Wakati sisi hapa Tanzania Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni asilimia 18, nchi zilizofanikiwa kiuchumi kodi hii iko chini mno kuhamasisha uwekezaji na uzalishaji kwa nia ya kukuza ajira. Marekani wanatoza VAT 2.9% na 7.5%. China wanatoza 13%, 9%, 6% na baadhi za viwanda 0.5%. Andorra wanatoza 4.5% na bidhaa chache 9%. Canada wanatoza 5%. UAE 5%. India ina viwango tofauti vya VAT kulingana na bidhaa 0.25%, 1.5%, 3%, 5%, 12%, 18% na 28%.

Nigeria wanatoza VAT 7.5%, Oman 5%. Taiwani 5%. Kuna bidhaa zinapata bei ya chini zaidi. Korea Kusini VAT ni asilimia 10. Vietnam (8%). Nchi nyingi duniani, VAT wana kiwango cha asilimia 10, lakini baadhi ya bidhaa zinashushiwa kiwango ili kukuza uzalishaji hadi asilimia 0.5. Bahati mbaya hapa kwetu ni asilimia 18. Iwe unauza mbao, unauza mchicha, unatengeneza magari, risasi au mabomu. Hili ni kosa. Tubadilike. Tunaua uchumi wetu.

Sitanii, kosa jingine nimetangulia kusema kuwa mtu kusoma uhasibu, haimaanishi kuwa anafahamu maana ya kodi au biashara ni nini. Unakuta kijana aliyetoka chuoni, mtu anamwambia anaomba zabuni ya Sh milioni 500, kijana wa TRA ampatie Tax Clearance ashinde zabuni apate biashara hiyo, ila anakwama. Vijana hawa wasiojua biashara, wanamwambia unadaiwa Sh milioni 6, wanamnyima Tax Clearance mfanyabiashara anashindwa kushiriki zabuni ya Sh milioni 500 ambayo angeshinda angelipa hata hizo Sh milioni 6, wanakosa wote!

Mhe. Rais, mdahalo wa wagombea urais Marekani na wagombea uwaziri mkuu Uingereza, umenifumbua macho. Kodi zikiwa chini, uzalishaji unakua, uchumi unakua. Ebu unda Kikosi Kazi kama ulivyounda kwenye Hali ya Siasa na Haki Jinai, Kikosi Kazi hiki kije na majibu ya kodi zinazolipika.

Tukiendelea na kodi za sasa za kikoloni, kwa hakika tusahau kukuza uchumi wetu. Nchi zilizoendelea kodi ziko chini, uzalishaji uko juu. Hivi tunadhani Marekani na China kuwa na kodi za chini ni wajinga? Mungu ibariki Tanzania.
 
Ends

Please follow and like us:
Pin Share