Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Leo katika makala hii, naomba, narudia, naomba sana niandike juu ya mambo mawili. Mambo haya ni treni yetu ya mwendokasi (SGR) na uzinduzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa KV400 kutoka Chalinze hadi Dodoma.
Napata mtanziko nianze na lipi. Nilipata furaha nikiwa pale Dodoma, pale Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, alipotangazia umma wa Watanzania kuwa nchi yetu inao umeme mwingi kwa kiwango ambacho hadi sasa tumezima baadhi ya mitambo ya Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Dk. Biteko akasema kwa sasa umeme wa kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere unasafirishwa kwa kutumia njia ya Reli ya Kisasa ya SGR kutoka Chalinze kwenda Dodoma.
Akasema kwa Desemba 11, 2024 kuzindua msongo wa KV 400, na njia ambayo sasa inapeleka umeme Dodoma badala ya kutumia njia ya SGR, basi Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), litakuwa limeingia katika mkondo sahihi wa kutengeneza faida.
Katika makala zijazo au niseme tu bayana nitaeleza kwenye toleo lijalo juu ya kazi kubwa na ya kipekee aliyoifanya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusaidiwa na wateule wake kama Dk. Biteko kumalizia ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na ujenzi wa njia hii yenye msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze kwenda Dodoma, njia ambayo inasafirisha umeme mkubwa.
Sitanii, ni bahati mbaya tu, kwamba baadhi ya watu katika nchi yetu wamefikia hatua hawataki kusikia ukweli bali jambo wanaloliamini. Kwamba leo kama hapa ninavyoelekea kusema na nasema kwamba kila awaye anapaswa kumpongeza Rais Samia kwa ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere lililofikia asilimia 99.6 kwa mujibu wa Dk. Biteko. Wasio heri wanasema anayesifia ni ‘chawa’.
Narukia, heri kusifia jambo jema kama hili la Rais Samia aliyeukuta mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere katika asilimia 33 wakati anachukua nchi na leo limefikia asilimia hizo 99.6, na kwamba unajengwa msongo wa KV 400 kusafirisha umeme kati ya Chalinze na Dodoma kama alivyosema Dk. Biteko kuliko kuwalisha vumbi Watanzania.
Sitanii, katika hali ya kawaida kila mtu anaweza kupeleka sifa kwa Rais Samia au Dk. Biteko kwa kukamilisha mradi huu wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na mingine.
Hata hivyo, nimepokea na kutafsiri kuwa ni unyenyekevu wa hali ya juu kauli ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Biteko, aliyoitoa pale Zuzu, Dodoma, Desemba 11, 2024.
Dk. Biteko amesema: “Hizi pongezi ninazopewa zinapaswa kuwaendea watendaji.” Hapa alimaanisha watendaji wa wizara na TANESCO. Kwa TANESCO watendaji wanaongozwa na Mtedaji Mkuu wa shirika hilo, Injinia Boniface Gissima Nyamo-Hanga.
Huyu tutakumbuka kuwa alipewa miezi sita na Rais Samia. Wakati anateuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESO, hali ya umeme ilikuwa mbaya nchini. Rais Samia alimwambia anampa miezi sita kuthibitisha utendaji wake.
Ni zaidi ya mwaka mmoja sasa Nyamo-Hanga anaendelea na kazi. Ni wazi ameushinda mtihani aliopewa na Rais Samia wa miezi sita. Kwamba umeme umeacha kukatika si kwa misingi ya ubora wa miundombinu, bali uzalishaji.
Nitaandika katika makala ijayo. Uhalisia ni kwamba leo nchi yetu inazalisha umeme mwingi kuliko mahitaji. Nyamo-Hanga amethibitisha umahili wake na ndiyo maana hajatumbuliwa baada ya hiyo miezi sita.
Sitanii, narejea hoja yangu kuwa nitaandika kwa kina juu ya uzinduzi wa ujenzi wa njia ya msongo wa umeme wa KV 400 kutoka Chalinze kwenda Dodoma wiki ijayo, ila leo kutokana na hoja ya hatari ya pili ninayoiendea sasa, naomba niandikie ajenda iliyonishitua ya matumizi ya vichwa vya dizeli kwenye miundombinu wa kisasa wa reli – SGR.
Sitanii, narudia, sitanii, katika muda wa miaka 31 ya kufanya kazi hii ya uandishi wa habari. Hili la watendaji tuliowaamini kuwa watatuvusha kuja na mawazo ya kununua vichwa vya treni ya SGR vinavyotumia dizeli ni jambo lililoniumiza kuliko siku zote.
Sijawahi kuumia katika maisha yangu kwa kupata taarifa, kama ilivyokuja hii taarifa hii ya SGR uongozi kueleza nia ya kununua vichwa vya dizeli. Kwa sasa mimi ni Rais wa Wahariri Afrika Mashariki. Kila tukienda kwenye vikao nchi yetu inapigiwa mfano.
Wakenya ambao siku zote utuchukulia Watanzania kama daraja la tatu kwao, mara zote wananiambia Tanzania imekomesha. Imeonyesha SGR ni reli ya aina gani. Reli ya kwao ya Nairobi – Mombasa, wananiambia ni “gari moshi” kwa sababu inatumia dizeli. Leo na sisi tunataka kurejea kwenye gari moshi? Hapana.
Nakiri baada ya kupata taarifa hii, niliituma kwa Masanja Kadogosa, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC). Majibu yake kwangu, alisema si kweli, TRC haina mpango huo.
Baada ya muda mfupi nikatumiwa mahojiano yake na Gazeti la The Citizen. Hapa nilipata wakati mgumu sana. Nilimtumia ujumbe ambao hadi leo hajanijibu. Kwamba “Mbona umenidanganya?”
Kumbe awali sikujua kwamba aliishafanya mahojiano na The Citizen na akawathibitishia kuwa TRC wanaagiza vichwa vya dizeli. Nakiri na narudia, hayati Rais John Pombe Magufuli wakati anaanzisha mradi huu, aliandaa timu kadhaa. Ninazo taarifa, ambazo katika hili naamini ripoti hii hata Kadogosa anayo.
Kwamba timu hizi zilifanywa uchunguzi wa matumizi ya vichwa vya dizeli na umeme. Ilitumwa timu Kenya, Ethiopia na Afrika Kusini. Rais Magufuli wakati huo aliunda timu ambayo wajumbe walikuwa wake walikuwa ni pamoja na Masanja Kadogosa, mwingine ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bandari wakati huo, Deus Kakoko, aliyekuwa Mkurugenzi wa TANROADS, Patrick Aron Nipilima Mfugale na wataalamu wengine.
Ripoti ya kamati hii ilieleza kuwa treni ya kisasa itumie umeme badala ya dizeli. Ni kwa msingi huo, Tanzania imekuwa nchi pekee katika ukanda wetu kutumia vichwa vya treni vya umeme badala ya dizeli. Ulikuwa uamuzi wa kisera, haikutokea kwa bahati mbaya.
Kati ya yaliyobainika ni gharama kubwa za uendeshaji kupitia zabuni za kuuza dizeli kuwa na harufu ya rushwa na ikaamuliwa kuwa sisi tutumie umeme. Kenya wanalia. Mafuta yanakula kila senti inayoingia kwenye shirika.
Sitanii, kupitia hoja hii ya pili katika makala hii namwomba Rais Samia asikubali uamuzi wa kununua vichwa vya dizeli kwenye SGR. Pale Dodoma Desemba 11, 2024 Dk. Biteko ameliambia taifa kuwa baadhi ya mashine za kuzalisha umeme Bwawa la Mwalimu Nyerere zimezimwa kwani mahitaji ya umeme wa nchi yetu ni juu kidogo ya megawati 1,800, wakati uwezo wetu wa kuzalisha umeme sasa ni megawati zaidi ya 3,000.
Nimewaona manabii wa vichwa vya dizeli kwa SGR wakisema njia ya umeme ya sasa haina usaidizi, na ni gharama kubwa, yapata Sh bilioni 500 kujenga njia saidizi (backup) ya SGR.
Dk. Biteko ametwambia pale Dodoma kuwa uzinduzi wa ujenzi wa msongo wa KV 400 unaliondoa taifa letu katika utegemezi wa kusafirisha umeme kwa kutumia njia ya SGR na kuwa na msongo mkubwa wa umeme.
Sitanii, katika makundi sogozi, yupo nabii wa injini za dizeli aliyeandika hivi: “Kwa kawaida, njia za treni hizi maarufu kama SGR huwa na njia mbili za umeme. Moja hutumika kama backup iwapo moja itazimwa. Hata hivyo, sisi tuna njia moja tu, hivyo hitilafu yoyote ikitokea huathiri moja kwa moja usafiri.
“Kutengeneza njia nyingine ni gharama kubwa, ikikadiriwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 500 ili kufanikisha upatikanaji wa megawati 80 za kuendesha SGR kama backup.
“Hivyo, ni lazima kuwa na mpango wa dharura au njia mbadala ili kuhakikisha usafiri haukatizwi endapo hitilafu itatokea. Backup rahisi kwetu ni injini za dizeli, maana hata solar ni ghali sana na ngumu kuweza kutengeneza megawati nyingi.
“Pia zinaharibika kila baada ya miaka mitatu. Injini za dizeli zikitumika badala ya injini za umeme kwenye SGR mara umeme ukatikapo inaweza [ikachangia] kasi kupungua, lakini si kwa kiwango kikubwa sana.
“Ni sawa na magari yanayotumia gesi na hapo hapo petroli, gesi ikiisha gari halisimami, injini inachukua moto kutoka kwenye mfumo wa mafuta na wala mteja… hawatajua kuna badiliko la mfumo.
“Treni nyingi za dizeli zina kasi ya juu inayokaribiana na treni za umeme, ingawa kwa safari ya mwendo mrefu kasi hupungua kutokana na miundombinu kuwa rafiki zaidi kwa SGR ya umeme.
“Hivyo, kasi inaweza kupungua kidogo, hasa kwenye umbali mrefu. Treni za dizeli zinaweza kuwa na changamoto katika kufikia kasi sawa kwenye mwinuko au maeneo yenye kona nyingi kama Kilosa. Hata kwa sasa kuna backup ya panel za betri, lakini ufanisi na uharaka wa kurejesha umeme ukichukua muda lazima treni isimame.
“Kwa mazingira ya Ulaya ndani ya dakika tano mambo yanakuwa sawa, lakini hapa kwetu wahuni wanakata nyaya za umeme huko porini, hivyo ni lazima kuwa na backup ya uhakika.
“Kaka… alifanya kazi kwenye treni Cardiff ingawa sitawaeleza utaalamu wake ulikuwa ni nini. Kaka… tupe shule,” haya ni maelezo yanayoashiria mpango usio mwema. Namfahamu kwa wajihi aliyeandika maelezo haya na ukiniuliza huu si mwandiko wake!!!!
Sitanii, kwa maelezo thabiti tuliyopewa mara kwa mara, hizi treni mchongoko tumenunua seti 10 kutoka Korea Kusini. Mawazo kama haya hawatuelezi tukinunua injini za dizeli hivi vichwa vya umeme tunavipeleka wapi?
Mhe. Rais, nafahamu yanaweza kuwapo maelezo mazuri kama asali, ila sifa yetu Tanzania ni treni ya umeme. Si gari moshi. Piga ua, tuhakikishe haturudi kwenye vichwa vya treni vya dizeli. Sisi tumeondoka katika linaloitwa gari moshi.
SGR tangu imezinduliwa Julai mwaka huu, imetuingizia si chini ya Sh bilioni 30. Safari ya Dar es Salaam – Dodoma inatumia umeme wa Sh milioni 1 kwa treni. Tumeingiza kiasi hiki kwa kusafirisha abiria tu, na hapo bado mizigo.
Dizeli naambiwa itagharimu si chini ya Sh milioni 10 kwa safari moja. Tuukatae mchongo huu hewa. Nafahamu wapo wanaotafuta faida za kifedha, ila kuna hatari kuwa mpango huu hauna tofauti na hujuma za kisiasa kuelekea urais mwaka 2025.
Sitanii, nimeona kanusho la Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa. Amesema Tanzania haina mpango wa kununua injini za dizeli kwa SGR. Nasema ni heri, ila asome Gazeti la The Citizen la Ijumaa, Desemba 13, 2024, aone mahojiano yao na Kadogosa. Nadhani chui aliyemfukuza mwanambuzi hajarudi!
Niruhuru niweke kituo. Kubwa Mhe. Rais Samia zikatae injini za dizeli kwa SGR. Tanzania ndiyo pekee katika Afrika tunahesabiwa kwa treni ya umeme na tunapata faida. Hawa wanataka kukuingiza chaka. Wakatalie. Mungu ibariki Tanzania.
0784404827