Na Deodatus Balile

Wiki iliyopita nimesoma habari ya kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa njia nne katika Barabara ya Morogoro. Ujenzi huu unaelezwa kuwa utaanzia Kibaha Maili Moja hadi Morogoro kwa urefu wa kilomita 158. Taarifa hizi zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge na zikatiliwa mkazo na Ofisa Sayansi ya Jamii kutoka TANROADS Makao Makuu, Gibson Mwaya.

Kunenge wakati anatoa taarifa hizo amesema: “Ujenzi utakuwa wa barabara ya njia nne, mbili kwenda na mbili kurudi, lakini kabla ya ujenzi usanifu utabainisha kama kuna watakaotakiwa kulipwa kisha ndipo hatua za ujenzi zitaanza.” Kunenge ametoa taarifa hiyo katika kikao kati yake na maofisa kutoka TANROADS Makao Makuu Dar es Salaam wiki iliyopita.

Sitanii, nafahamu Watanzania wengi wanapenda siasa. Wengi wanauliza maoni yangu juu ya Spika ajaye na mengine mengi ya aina hiyo, lakini leo nimeona kwangu mimi na Watanzania wenye kutaka maendeleo ya kweli ya uchumi, habari hii ni kubwa na ya heri mno. Barabara ya Morogoro ni kiungo muhimu kwa uchumi wa nchi yetu.

Barabara hii ni lango la nchi za Malawi, Zimbabwe, Zambia, DRC, Rwanda, Burundi na Uganda zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam. Kwa matumizi ya bandari, barabara hii ni kitovu cha karibu mikoa yote ya Tanzania, ukiacha Lindi na Mtwara. Ni vigumu mtu kusisitiza umuhimu wa barabara hii hadi akaeleweka, ila ieleweke kuwa ina umuhimu wa pekee katika kukua kwa uchumi wa taifa letu.

Urefu wa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ni kilomita 189. Kutokana na jinsi barabara hii ilivyobanana, ukiwa na gari binafsi unatumia saa 5 kutoka Dar es Salaa hadi Morogoro. Ikiwa jioni ukabahatika kutanguliwa na malori unatumia hadi saa 7, wakati mwingine saa 10. Hii ina maana kihualisia unatembea wastani wa kilomita 27 kwa saa.

Matrafiki ndiyo barabara inayoongoza kwa kuwaingizia pato haramu. Barabara hii ina chochoro, zebra na mistari iliyofunga mingi kuliko barabara yoyote hapa nchini. Ukibahatika kutanguliwa na lori kati ya Mlandizi hadi Ubena Zombezi, unajihakikishia kutembea kasi ya kilomita 10 kwa saa. Umbali wa kutoka Morogoro hadi Dodoma ni kilomita 256.

Mara nyingi nikiwa naendesha gari, tena mwendo wa kawaida kabisa, ingawa nayo inapaswa kutazamwa au tufikirie njia mbili pia, natumia saa tatu kati ya Dodoma hadi Morogoro. Hapo tena nikiwa na IST. Enzi hizo nikiwa na Freelander ilikuwa natumia saa 2:20 tu, tena mwendo wa kawaida. Umbali wa Dar es Salaam hadi Dodoma ni kilomita 445, lakini safari ya kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma inachukua saa 10. Hii ina maana tunaendesha wastani wa kilomita 45 kwa saa.

Barabara ya kutoka Arusha hadi Dodoma kupitia Babati ina urefu wa kilomita 430. Nikiwa na IST, hivi karibuni nimetoka Arusha hadi Dodoma kupitia Babati kwa muda wa saa 4 tu. Hii ina maana nimetembea wastani wa kilomita 108 kwa saa. Katika barabara kuu, mwendo wa kilomita 120 kwenye barabara iliyojengwa vizuri si kitu. Ilimradi tairi ziwe nzuri na gari limetengenezwa vema.

Hivi karibuni nilikuwa Guangzhou, China ambako nilishuhudia wao barabara kuu (highway) nyingi wamejenga njia tatu hadi tano. Kuna vibao kabisa vinavyoonyesha kuwa baadhi ya njia (lane) ukiingia unapaswa kutembea kasi ya kuanzia kilomita 140 kwenda juu. Zipo njia za kasi ya kilomita 100 na zipo za kilomita 80 maeneo ya mijini. Usanifu wa barabara unahusisha vivuko vya waenda kwa miguu.

Mfano sasa hivi barabara ya Kimara hadi Kibaha Maili Moja imejengwa vizuri sana njia sita, ila ni kero. Kila hatua 20 kuna kivuko cha waenda kwa miguu. Barabara imejazwa vibao vya 50 hadi inapoteza maana ya kujenga barabara nzuri kama ile. Matrafiki wamejibanza kila kona na kamera. Usanifu wa barabara unapaswa kuhusisha vivuko vya waenda kwa miguu wapite ama juu au chini ya barabara. Waenda kwa miguu hawapaswi kukatiza katikati ya barabara kuu (highway).

Sitanii, wakati nikiwapongeza TANROADS na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi mwafaka kabisa wa kujenga njia nne kwenda Morogoro, nashauri vivuko vya waenda kwa miguu viwe chini au juu, badala ya kuijaza barabara vibao vya 50. Pia sehemu zenye milima, kama ilivyo Barabara ya Arusha – Babati – Dodoma, ziwekewe njia za mpando (climbing lane) kwa ajili ya malori. Barabara ikiwa nzuri, kasi inaongezeka na ajali zisizo za lazima zinazuiwa.

Barabara ya Morogoro imeua watu wengi hadi idadi haihesabiki kutokana na kuwa njia moja. Ikijengwa njia mbili na kuacha gema katikati kuepusha ‘walevi’ wanaoendesha wakitambaa kila kona barabarani wasiingie upande wa kwenda au kurudi, tutaokoa maisha ya wananchi na tutakuza uchumi kwa kasi kubwa kuliko tunavyodhani. Huu ni uamuzi sahihi na naomba tuunge mkono. Mungu ibariki Tanzania.