Na Mwalimu Paulo Mapunda
Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Toleo la Pili la mwaka 2004, inaeleza maana ya neno “Demokrasia” kuwa ni mfumo wa kuendesha serikali iliyochaguliwa na watu kwa manufaa ya watu.
Hivyo uhalali wa serikali yoyote ya kidemokrasia unatokana na watu kwa ustawi wa watu, uamuzi wote halali wa nchi unafanywa na watu kupitia sanduku la kura.
Ni katika mnyororo huu wa kufikiri, uamuzi wote uhusuo nchi hufanywa na rais kama kiongozi mkuu wa nchi, kwa kuwa watu (wananchi) wamempa rais uhalali wa kufanya uamuzi huo.
Hali kadhalika Bunge lina uhalali wa kufanya uamuzi kwa kuwa wananchi wamelipatia mamlaka hayo kupitia wawakilishi waliowachagua kupitia sanduku la kura.
Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa mgombea mwenza wa hayati John Magufuli, alizunguka nchi nzima akiinadi Ilani ya CCM yenye kurasa 303, huku akiomba ridhaa ya wananchi kuichagua CCM, hivyo kuwachagua Magufuli na Samia Suluhu Hassan.
Baada ya kifo cha Dk. Magufuli, mgombea mwenza ambaye kwa ridhaa ya wananchi alichaguliwa kuwa makamu wa rais akawa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba. Ibara ya 37(5), inasema hivi: “Where the office of president becomes vacant by reason of death, resignation, loss of electoral qualifications or inability to perform his functions due to physical infirmity or failure to discharge the duties and functions of the office of the president, then the vice president shall sworn in and become the president for unexpired period of the term of five years and in accordance with the conditions set out in Article 40, and after consultation with the political party to which he belongs, the president shall propose the name of a person who shall be vice president and such appointment shall be confirmed by the National Assembly by votes of not less than fifty percent of all the members of parliament.
Ibara ya 40 (4) inatoa ufafanuzi zaidi wa maelekezo kwa anayechukua nafasi ya rais. Rais Samia yuko Ikulu kwa mujibu wa katiba ambayo ni sheria mama, hiki ni kielelezo kilicho wazi kabisa cha utekelezaji wa demokrasia.
Ibara ya 33 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inamwelezea Rais kama; Kiongozi wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama. Ibara ya 36 vifungu vidogo vya (1), (2), (3), vinampa rais mamlaka ya kuteua viongozi katika ofisi na idara mbalimbali za utumishi wa umma.
Ni kwa mujibu wa Ibara ya 36 ya Katiba ya JMT, siku chache zilizopita Rais aliwateua wakuu wa mikoa. Nachukua fursa hii kumpongeza Rais Samia kwa kutekeleza takwa hili la kikatiba. Zaidi nimpongeze kwa kuonyesha ukomavu wa kidemokrasia kwa kuwateua Queen Sendiga (mgombea urais 2020 kwa tiketi ya Chama cha ADC) kuwa mkuu wa Mkoa wa Iringa kuchukua nafasi ya Ally Ally Hapi aliyehamishiwa Mkoa wa Tabora.
Miezi michache iliyopita Queen Sendiga alikuwa majukwaani akiipeperusha bendera ya chama chake ili kuomba ridhaa ya kuongoza Tanzania.
Kwa maneno mengine, alichuana na hayati Magufuli pamoja na Rais wa Awamu ya Sita, Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika kugombea nafasi yoyote ile, silaha zote hutumika, hivyo uko uwezekano akiwa jukwaani Queen pengine alipata kutamka maneno yasiyofaa dhidi ya CCM na wagombea wake, lakini Rais Samia amefunika kombe na kumteua kuwa mkuu wa Mkoa wa Iringa. Hongera sana Rais Samia.
Uteuzi mwingine ni wa David Kafulira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu. David anafahamika dhahiri kuwa ni zao la Chadema na NCCR.
Aliteuliwa kwa mara ya kwanza na hayati Dk. Magufuli kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, lakini Rais Samia amemuamini zaidi na kumteua kuwa mkuu wa mkoa.
Mkuu wa mkoa ni mwakilishi wa juu kabisa wa Rais katika mkoa husika. Vilevile ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa.
Kwa ujumla mkuu wa mkoa ndiye kiongozi wa juu kabisa ndani ya mkoa husika. Kwa Rais kuwateua Kafulira na Sendiga kushika nafasi hizo ni kiwango cha juu kabisa cha demokrasia alichoonyesha na anatukumbusha kuwa nchi hii ni yetu sote, Mwenyeezi Mungu ametupatia nchi hii, tuna wajibu wa kuilinda, kuitunza kwa ajili yetu na kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Nitumie nafasi hii kuwakumbusha wapinzani kuwa wana wajibu wa kumsaidia Rais katika utekelezaji wa mipango yake ili kuitoa nchi hapa ilipo na kusonga mbele zaidi.
Jukumu la upinzani si kueneza chuki dhidi ya serikali iliyo madarakani, bali ni kuwaunganisha wananchi na serikali yao.
Hiki si kipindi cha kampeni, bali ni kipindi cha kujenga nchi kwa kuhamasisha maendeleo kwa kusisitiza umoja na mshikamano kwa Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa.
Wapinzani wana wajibu wa kuelimisha wanachama wao kuhusu demokrasia ya vyama vingi kwamba upinzani si uadui wala si ugomvi, bali ni ushindani wa hoja, mwenye hoja yenye nguvu ndiye anayeshinda.
Hakuna sababu ya kununiana wala kuchukiana, kwani sisi sote ni ndugu, tunajenga nyumba moja hivyo hatuna sababu ya kugombea fito.
Tuwasiliane: [email protected]
0755 671 071