*Azindua treni ya kisasa, vituo vyapewa majina ya marais

*Ni treni ya umeme ndefu kuliko zote Afrika, ya tano duniani

*Tayari wamekusanya bilioni 3.1, umeme inatumia milioni 1

*Inasafirisha watu 7,000 kila siku, Mama Mosha atoa ya moyoni

Na Deodatus Balile, JamhuriMedia,Dodoma

Rais Samia Suluhu Hassan amezindua treni ya mwendo kasi (Standard Gauge Railway (SGR) na kuandika historia baada ya miaka 114 ya Tanzania kujenga reli ndefu na kusema, “Mradi wa SGR siyo ndoto tena, bali ni uhalisia.”

Kauli hiyo ameitoa leo Agosti 1, 2022 hapa jijini Dodoma wakati anafanya uzinduzi wa miundombinu na safari za treni kati ya Dar es Salaam na Dodoma kupitia Morogoro. “Nilipopokea kijiti, tulichukua mradi huu na kuuendeleza na kuufikisha hapa ulipo. Niliamua miradi yote ya Awamu ya Tano tunaiendeleza. Mradi wa SGR siyo ndoto tena, bali ni uhalisia,” amesema Rais Samia na kushangiliwa, kisha akaongeza:

“Katika miaka mitatu ya Awamu ya Sita, tumekamilisha vipande viwili vya Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro hadi Dodoma,” amesema na kuongeza kuwa kwa sasa kazi inaendelea katika vipande vya Makutopora hadi Tabora kilomita 368, Tabora – Isaka kilomita 165 na Isaka – Mwanza kilomita 341. Pia Serikali inajenga Tabora – Kigoma kipande chenye urefu wa kilomita 506, Uvinza – Msongati kilomita 565, ambayo itajumuisha kuigia katika nchi za Burundi na DRC.

Sitanii, Rais alikuwa na uwezo wa kuanza miradi mipya akaitelekeza reli kwani ndiyo ulikuwa mradi mgumu kutokana na kwamba wafadhili na taasisi za kifedha hazikuwa tayari kuikopesha Tanzania, ila akasema Kazi Iendelee. Viongozi wa Afrika walio wengi huwa hawamalizii miradi ya watangulizi wao ambapo Mrisho Mpoto amesema “hata akikuta kiwanja kimepandwa miti, anaikata na kupanda upya.” K

ati ya Dar es Salaam na Dodoma zimetumika Sh trilioni 9.9, ambapo Serikali imelipa zaidi ya Sh trilioni 6.83.

Sitanii, uzinduzi wa reli hii unakwenda kukomesha msemo wa “Kigoma mwisho wa reli” kwani reli hii sasa inakwenda kupitiliza Kigoma kwenda Burundi na DRC. DRC kuna mzigo mkubwa wa madini ambao unastahili kusafirishwa kwenda nje ya nchi, ila usafiri ndiyo kimekuwa kikwazo ikubwa. Reli hii ndiyo ndefu kuliko zote barani Afrika zinazoendeshwa kwa umeme na ni ya tano kwa urefu duniani.

Nchi zilizoendelea hazikutaka SGR ijengwe

Sitanii, Rais Samia anasema nchi zilizoendelea hazikutaka kuona Tanzania inakamilisha mradi huu wa SGR kwani zinafahamu kuwa mradi huu ukikamilika Tanzania inafuta umaskini. Amesema kuna mzigo mkubwa kati ya DRC na nchi nyingine jirani, ambao utasaidia Bandari ya Dar es Salaam kuwa na mzigo wa kutosha na kutengeneza faida kubwa. Rais Samia amewataka TRC reli hii waiendeshe kwa faida isiombe tena ruzuku kutoka Serikalini, bali itoe gawio.

Maneno ya Rais Samia yanathibitishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara. “Kwa sasa treni kwenda Dodoma inatumia umeme wa Sh milioni 1. Tangu tumeanza tumetengeneza kama Sh bilioni 3, na matumizi yetu ni kama milioni 500, hivyo tuna zaidi ya Sh bilioni 2.5 kwenye akaunti. Hii biashara ni nzuri mno,” amesema Prof. Kahyarara. Amesema ikiaza kusafirisha mizigo, itaanza kutengeneza faida kubwa.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, akatoa jibu la msingi juu ya mapato. “Tunawashukuru Watanzania hadi sasa tumesafirisha abiria 160,000 ambao wametulipa Sh bilioni 2.4,” amesema Kadogosa. Amesema fedha hizo zilitokana na nauli walizolipa wasafiri kuanzia Juni 14, 2024 hadi Julai 27, 2024. Kati ya Julai 28, 2024 hadi Agosti Mosi, safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma, TRC imesafirisha abiria 28,600 ambao wamelipa jumla ya Sh milioni 744.

Sitanii, jumla tangu treni ya mwendo kasi imeanza kazi tayari imezalisha wastani wa Sh bilioni 3.14. Hadi leo ilikuwa imesafirisha jumla ya abiria 188,000 ambapo zaidi ya Watanzania 7,000 wanatumia treni hii kila siku. Katika kuboresha usafi na kuhimili kiwango cha mizigo, daraja la uchumi, abiria anaruhusiwa kusafiri na kilo 20 na daraja la biashara kilo 30. Abiria haruhusiwi kuingia na chakula, wala silaha kwenye treni hii.

Kadogosa amesema Aprili 20, 2021 wakati Rais Samia Suluhu Hassan anahutubia Bunge jijini Dodoma, aliahidi kuendeleza SGR kwa kumalizia vipande viwili vya Dar es Salaam – Morogoro na Morogoro – Dodoma. Wakati huo Kipande cha Dar es Salaam – Morogoro kilikuwa kimekamilika kwa asilimia 83, ilihali kile cha Morogoro – Makutopora kilikuwa kimekamilika kwa 57%.

Rais Samia aliahidi kujenga vipande vingine vitano, ambavyo hadi sasa Isaka – Mwanza kimefikia asilimia 60 na ujenzi unaendelea kwa Makutopra – Tabora, Tabora – Isaka na Tabora – Kigoma. Serikali ipo katika hatua za mwisho kuanzisha ujenzi kipande cha Uvinza –Msongati – Burundi. “Mikoa ya Mbeya, Tabora na Singida, Sinyanga, Simiyu, Mwanza, Kagera, Geita, Mara, reli wanayoiona Dodoma itafanana hivyo hivyo kwa zitakazojengwa kwao,” amesema Kadogosa. Amesema ujenzi wa reli katika baadhi ya maeneo utaendelea hadi mwaka 2027 na 2028.

Ujenzi wa tuta umechukua udongo cubic meter 138 milioni, madaraja yana ujazo wa cubic meter milioni 1.8, mifuko ya saruji imetumika milioni 19.1, mataluma milioni 1.2, nondo tani milioni 143 na zimejengwa station 12 ndogo. Usanifu wa majengo kwa jengo la Tanzanite – Dar es Salaam limechukua muundo wa milima ya Uluguru na la Dodoma wamejenga kwa aina ya nyumba zao (tembe). Wamejenga vituo vya kupozea umeme 11 na vituo vidogo 54.

Mradi huu mkubwa na wa mfano umehusisha ujenzi wa nguzo za kuwezesha ishara na mawasiliano. Minara 71, ambayo inatumiwa na SGR pekee na ni mingi kuliko ya Vodacom katika njia hiyo. Wamejenga fibber kilomita 536 kwa ajili ya kuongozea na kuimarisha usalama njiani. Wameweka mifumo ya TEHAMA ndani ya SGR.

Pia, wamejenga Transmission line ya Tanesco kwa ajili ya uendeshaji wa reli tu, hawaingiliani na mtu yeyote, ndiyo maana tangu waanze hawajapata matatizo ya umeme siku yoyote. Njia hiyo (Transmission Line) imeunganishwa kwenye chanzo cha umeme hivyo ili SGR isipate umeme nchi nzima itakuwa gizani. Matatizo ya machache yanatokea ya umeme kukatika kutokana na wanyama kama ngedere na bundi kusakama nyaya au waendeshaji wa treni kutokana na upya wa teknolojia kwao. Hadi sasa wana vichwa 19, mabehewa 65 ya abiria yameishapokewa kati ya 89, treni za vichwa mchongoko 10, ingawa hadi sasa zilizowasili nchini ni nne.

Mradi umeshirikisha sekta binafsi, ambapo jumla ya watoa huduma 2,460 wameshiriki katika ujenzi wa mradi huu na mikataba yenye thamani ya Sh trilioni 3.7 imesainiwa na kampuni za Tanzania, ambazo zimelipwa. “Fedha hizi zinarudi katika mzunguko wa hapa nchini… Tumetoa ajira 30,146, ambao wamelipwa mishahara Sh bilioni 358.4 [katika mradi huu],” amesema Kadogosa.

Kazi ambazo si za moja kwa moja, mradi umetoa ajira zaidi ya 150,000. Tanzania imeweka historia ambapo katika ujenzi wa mradi huu, asilimia 49 ya wataalam waliojenga mradi wametoka Tanzania, wakati kwa nchi nyingine huwa wataalam wazawa wanakuwa chini ya asilimia 15 na miradi ikikamilika inaendeshwa na kampuni za kutoka nchi ilikotoka kampuni iliyojenga reli kama China, India au Ulaya, ila SGR ya Tanzania inaendeshwa na Watanzania wenywe.

Kadogosa amesema mradi wa SGR umechelewa kukamilika kutokana na changamoto ya Uviko 19 na mvua zilizonyesha kuliko kawaida, hali iliyoathiri ujenzi. Alihitimisha hotuba yake kwa kusema: “Reli ya Kusini, Reli ya Kaskazini wakae mkao wa kula tunakwenda [huko]. Nchi jirani nako tunakwenda… Reli hii ni mali ya Watanzania. Watanzania waitunze reli baada ya miaka 100 ijayo tuwe na cha kuonyesha. Kaulimbiu yetu ni “Twendeni Tukapande Treni Yetu, Tuitunze na Tuithamini.”

Profesa Mbarawa anena mazito

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema hadi sasa kiasi cha Sh trilioni 10.8 kimewekezwa kupitia mikataba mbalimbali ya ujenzi wa reli. Serikali imelipa Sh trilioni 6.83, sawa na asilimia 68 ya fedha zote za mradi.

Amesema vipande viwili vya ujenzi kati ya Dar es Salaam na Dodoma wamejenga jumla ya kilomita 722, ambazo ni njia kuu na barabara za kupishania. Kwa sasa wanajenga vipande vitano vipya venye urefu wa kilomita 1,560 kati ya kilomita 2,102 za reli yote, urefu unaoifanya reli hii kuwa ya kwanza barani Afrika kwa treni inayotumia umeme. Kipande cha Saba cha Uvinza, Msongati, Kitega – Burundi, kwenda Kindu nchini DRC mchakato unakamilishwa.

Rais Samia awaza makubwa

Rais Samia ameeleza maono makubwa juu ya kuunganisha nchi jirani kwa usafiri wa SGR. Amesema kukosekana kwa miundombinu bora kumeshusha pato la Afrika kwa asilimia 2 na kuongeza gharama ya huduma kwa asilimia 40. “Muda wa safari unapunguzwa kwa asilimia 60 kati Dar es Salaam na Dodoma kutoka saa 9 hadi saa tatu na nusu. Sasa mtu anaweza kuchagua kama anakwenda Dar es Salaam – Bukoba atumie ndege, Dar es Salaam – Bukoba atumie treni hadi Dodoma, kisha apande basi hadi Bukoba,” amesema.

Amewataka wamiliki wa mabasi kuwaza kuingia ubia na TRC ambapo abiria anaweza kuwa tiketi moja, ambayo akishuka kwenye treni anapanda mabasi kutumia tiketi moja ileile. “Kuna fursa kadhaa. Treni itasaidi kupunguza ajali, na msongamano wa magari barabarani. Itapunguza uharibifu wa mazingira kwani inatumia nishati ya umeme, magari barabarani yanatoa hewa ukaa kwa wingi. Itakuza shughuli za kiuchumi katika viwanda, kilimo, ufugaji na chakula,” amesema.

Rais anatarajia ukuaji wa viwanda katika maeneo mbalimbali inakopita reli ya SGR kwani inarahisisha kufikia masoko kwa wakati na inaweza kubeba mizigo mikubwa kwa wakati mmoja hivyo malori mengi yatapungua barabarani. Kisha akatoa kibonzo kuwa Kadogosa aliwahisha treni kuanza kazi, baada ya kubaini kuwa kama ingepita Julai 25, 2024 angemtumbua kwani ahadi za kuanza kwa safari za treni zisizotekelezeka zilikuwa zimezidi idadi.

Historia ya mradi wa SGR na faida zake

Rais Samia ametoa historia ya SGR nchini kwa kusema mwaka 2001 hayati Rais Benjamin Mkapa aliandaa Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025. Dira ililenga Tanzania iwe na miundombinu itakayosaidia kukuza uchumi. Mwaka 2002 marais wa Tanzania, Kenya na Uganda walijadiliana kuhusu hitajio la kukarabati reli na kujenga reli mpya kukuza biashara na kuunganisha nchi hizi. Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete wakati wa uongozi wake alifanya tathmini na kuelekeza dira ivunjwe katika miaka 5 na akaamua ijengwe reli mpya.

Upembuzi yakinifu na tathmini aliyoifanya Rais Kikwete, Rais John Pombe Magufuli alianza kuutekeleza kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa 2017 – 2021. Mpango huo ulibainisha ujenzi wa reli kama mradi wa kielelezo na msingi mmojawapo wa mageuzi ya kiuchumi. Serikali ilianza rasmi kujenga reli kati ya Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro – Dodoma.

Ufanisi kwa Bandari ya Dar es Salaam unakwenda kuongezeka kwa kusafirisha mzigo mkubwa zaidi kutokana na treni hii kuwa na uwezo wa kuhudumia tani milioni 17 kwa mwaka. Nchi jirani zisizokuwa na bandari zinazofahamika kama Ushoroba wa Kati za Burundi, DRC na Uganda zitaitumia bandari hii kupitisha mizigo yake.

Rais amesema kuna watu wasiotaka heri, ambao wanakwenda kukata nyaya zilizowekwa kuzuia wanyama na watu kuingia kwenye reli. “Tutunze na kulinda mradi huu. Tuitumie kujiongezea kipato kwa ajili ya kuendeleza rasilimali na vitendea kazi… Wekeni mikakati ya kuendesha treni au reli hii kibiashara. Haitapendeza serikali kuendelea kulipa deni wakati shirika haliendi kwa faida. Ingependeza sana, shirika kupata faida.

“Msajili wa Hazina ukae na Bodi ya Managementi ya TRC muweke KPIs (vipimo vya utendaji) za kufuatiliwa na mzitumie kwa ukaribu zaidi. Reli hii imekuwa chachu ya Watanzania kujiamini kwamba hatima ya maendeleo yetu iko mikononi mwetu wenyewe. Reli ianzishe ushoroba wa maendeleo ya kiuchumi kote inakopita. Huo ushoroba wote uwe na shughuli za maendeleo. Reli ipunguze gharama za usafirishaji wa abiria na bidhaa, ituongezee pato kiuchumi.

“Reli ifungamanishwe na sekta za kuchochea ukuaji wa uchumi… Kuanza kwa safari za mizigo kutakamilisha shabaha ya mradi huu ya kujenga uchumi shindani. Tunakwenda kuendeleza maeneo ya kuweka mizigo hiyo hapa Dodoma na maeneo mbalimbali. Ihumwa kutakuwa na sehemu ya kuweka mizigo.

“Serikali iko katika hatua za mwisho za kuifufua reli ya Tazara, iendane na mahitaji na matarajio yetu. Reli ya Kati na TAZARA zitumie mabehewa kwa pamoja. Baada ya Bandari ya Dar es Salaam, tumejenga Bandari Kavu Kwala, na tunajenga Ihumwa (Dodoma), Isaka (Tabora) na maeneo mengine watakapoona kuna umuhimu wa kufanya hivyo… Tunaposema tunaifungua nchi, tunaifungua nchi kwa njia ya nchi kavu, angani na majini.”

Rais Samia atoa maagizo 10

Rais Samia ametoa maagizo 10 kwa Wizara na watendaji wengine:

  1. Wizara ya Uchukuzi hakikisheni vipande vya reli inayoendelea kujengwa vikamilike kwa wakati na ubora na viwango vilivyokusudiwa.
  2. Ujenzi wa meli na ukarabati wa meli kwenye maziwa Victoria na Tanganyika, hakikisheni yanakamilika kabla ya kukamilika kwa mradi huu zitumike kusafirisha mizigo.
  3. Hakikisheni mnaingiza reli katika Terminal III ya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, mizigo [na abiria] itoke moja kwa moja.
  4. Shirikisheni wadau na watoa huduma kwenye mradi huu [wa SGR].
  5. Tumieni mifumo ya kisasa ya TEHAMA, ikiwamo ulinzi wa reli na ukataji wa tiketi. Tusirudi tena kwenye tiketi za mkono.
  6. Hatutarajii TRC kuomba ruzuku kutoka Serikalini, bali tunatarajia gawio [kutoka TRC]. Tuwe na akaunti mbili za kifedha kama ilivyokuwa wakati wa ujenzi wa SGR na MGR (reli ya zamani). Tukichanganya hatutajua kipi kinatupa faida na kipi kinamnyonya mweziwe.
  7. Hakikisheni kuzingatia viwango vya Kimataifa katika utoaji huduma. Watalii wanaokwenda Mikumi sasa hawachukui tena ndege ndogo, wanatumia SGR kisha wakifika hapa Morogoro wanatumia magari kwenda Mikumi.
  8. Hakikisheni Usalama wa mizigo na abiria.
  9. Jengeni utamaduni mpya wa kazi, wekeni mifumo mipya ya ukarabati, wasomeshe wafanyakazi wajifunze tuwe na ufanisi.
  10. Mafaniko hayatatokana na TRC yenyewe pekee, bali yatatokana na serikali kuu, mikoa na wilaya, shirikianeni.

Rais Samia amesema ujenzi huu umethibitisha “uthubutu na ustahamilivu wetu kama taifa.” Amemshukuru mkandarasi Yapi Merkezi wa Uturuki na kusema Serikali ilijibana ndani ya mfuko mkuu wa serikali na kuanza ujenzi wakati wafadhili wakiwa hawataki kufadhili mradi wa SGR, lakini sasa Benki ya Afrika (ADB) imekubali kutoa fedha za kujenga vipande viwili vya mwisho.

Amemshukuru Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kwa kuipatia Tanzania ujuzi na uzoefu. Pia, Uturuki imeipatia Tanzania dola bilioni 6.4 kuendeleza ujenzi wa SGR. Amezishukuru Sweden, Denmark na Korea (Kusini), Standard Chartered [Bank], Shirika la Chakula Duniani (WFP) kwa kuipatia Tanzania mabehewa nane yanayotumia nishati ya jua kuhifadhi bidhaa zinazoharibika sizipowekwa kwenye jokofu. Pia ametambua mchango wa wizara ya fedha, ikianza na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango wakati mradi huu unaanza na Waziri wa sasa wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba.

Mradi huu umepokea tuzo mbili kimataifa kwa namna ulivyoandaliwa. Ameishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Due Diligence (uchunguzi wa kina) wa wazabuni. Pia amelishukuru Bunge la Tazania kwa kuiongoza vyema serikali katika mradi huu. Hasahau kuwashukuru waandishi wa habari waliokuwa wanatoa habari mbalimbali za mradi huu muda wote.

Amevipa majina vituo vya treni kama inavyoonyesha kwenye mabano kwa Kituo cha Dar es Salaam (John Magufuli), Morogoro (Jakaya Kikwete), Dodoma (Samia Suluhu Hassan), Tabora (Ali Hassan Mwinyi), Shinyanga (Abeid Aman Karume), Mwanza (Mwalimu Julius Nyerere) na Kigoma (Benjamin Mkapa).

Uzinduzi huu umehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar Dk. Huseein Mwinyi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu Dk. Doto Biteko, Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete na Rais (mstaafu) Amani Abeid Karume. Mawaziri Wakuu wastaafu Mizengo Pinda, Frederick Sumaye na Joseph Warioba. Pia walikuwapo Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson na Spika (mstaafu) Job Ndugai na viongozi wengine wakiwamo mawaziri na makatibu wakuu.

Mama aliyekaa kiti kimoja na Rais Samia anena

“Leo nimefarijika sana kukaa naye Rais [Samia] meza moja na kuzungumza naye. Na pia nimefurahi kupiga naye picha. Kwani hiyo ni kumbukumbu nzuri,” amesema Assumpta Richard Mosha, ambaye anafanya biashara eneo la Ilala Mchikichini (Karume). “Sikuwahi kuwaza maishani kuwa nitakaa na Rais meza moja,” ameongeza.

“Nakubali utendaji kazi wake, kwa sababu kama ameweza kusimamia miradi yote hii mikubwa na mingine imekamilika na mingine amejiongeza kwamba ataongeza baadhi ya maeneo reli ifike, kwa kweli mimi kama Mama Mtanzania, nampongeza sana, namwombea afya njema ili aendelee kuwatumikia Watanzania wote,” amesema.

Alipoulizwa picha aliyopigwa na Rais Samia atatumiaje, amesema: “Ile picha naisafisha. Mume wangu huko wameishamwambia mkeo si wa kwaida, amepiga picha na Rais Samia? Amenitumia meseji. Nitaisafisha na nitaiweka nyumbani kwangu na kwenye biashara yangu, anayekuja anaikuta. Anauliza hiyo habari ilikuwaje. Nyumbani na kwenye biashara yangu… Ni kiongozi anayejali makundi yote na anayasikiliza kwa ukaribu zaidi na wenye changamoto kubwa tumeona akizitatua.”

Rais Samia amefanya mahojiano na waandishi wa habari waliokuwa kwenye behewa namba 3303, ambapo nilikuwa mmoja kati ya waandishi wawili waliomhoji na mahojiano kamili juu ya ugumu wa kujenga reli ya SGR, maisha kama Rais na mengine, nitayachapisha kwenye toleo la Gazeti la JAMHURI, Jumanne ijayo.

Please follow and like us:
Pin Share