DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Ndugu wa mmoja wa mahabusu aliyepo katika Gereza la Keko anayetuhumiwa kwa kesi ya mauaji, Saidi Hamisi Lubuva, wameangua kilio ndani ya ofisi za gazeti hili wakati wakihadithia madhila anayokumbana nayo.
Hali hiyo imetokea wiki mbili zilizopita wakati ndugu hao walipozungumza na JAMHURI na kusema kwa miaka saba sasa ndugu yao yumo katika Gereza la Mahabusu la Keko, Dar es Salaam, kwa kesi isiyokuwa yake.
Pamoja na maelezo yao, wamelipatia JAMHURI nakala ya barua yake ya malalamiko.
“Ninataabika kwa miaka yote hii bila mafanikio licha ya kuandika barua mbalimbali kwa mahakimu na mamlaka nyingine husika,” anasema Lubuva katika barua hiyo, akimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati.
Anamwomba Rais, ikimpendeza, aunde tume ichunguze mashitaka yanayomkabili yeye na watuhumiwa wengine kadhaa waliopo mahabusu kwa muda mrefu na kuwachukulia hatua askari wachache wanaolichafua Jeshi la Polisi, na kulitaja jina la askari anayetumika kumkandamiza.
“Huyu askari ndiye kinara wa kuwabambikizia watu kesi mbalimbali na kuwaweka rumande,” anasema.
Barua yake hii hapa kama alivyoiandika:
Mh Rais; Kuna askari anaitwa (jina linahifadhiwa) ndiye kinara na kiongozi mkuu wa kubambikia watu kesi. Amekuwa akionekana kufanya kazi vizuri katika Jeshi la Polisi na kupandishwa vyeo – kwa uonevu wake anaoufanya.
Mheshimiwa, mimi nilikamatwa tarehe 13/06/2014 kwa tuhuma za wizi na kupelekwa Kituo cha Kati (CENTRAL DAR) mpaka ilipofika tarehe 8/07/2014 na kuhamishiwa Kituo cha Polisi Oysterbay na kukaa hapo mpaka tarehe 15/07/2014 na kurudishwa tena Kituo cha Kati.
Nilikaa hapo mpaka ilipofika tarehe 1/08/2014 na kupelekwa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na kusomewa kesi namba CC340/2014 ya wizi na nyingine namba P117/2014 ya mauaji.
Hati ya mashitaka ya mauaji hayo inaonyesha kuwa yalifanyika tarehe 6/07/2014. Nililalamika kwa hakimu kwamba tarehe ambazo polisi wanadai yalifanyika mauaji hayo mimi nilikuwa Kituo cha Polisi cha Kati chini ya uangalizi wa jeshi hilo.
Baada ya hapo (kutoka mahakamani) nilipelekwa Gereza la Segerea mpaka ilipofika tarehe 23/09/2014 na kurudishwa tena mahakamani ambako nilibadilishiwa hati ya mashitaka pamoja na tarehe ya tukio lenyewe, kisha wakaniongezea mshitakiwa mwingine ili kupoteza uasilia wa ubambikiwaji wa kesi.
Huyo mshitakiwa waliyemuongeza anaitwa Frank Adamu Mwakatobe kwa mujibu wa hati ya mashitaka. Mungu alivyo mkubwa, naye tulikuwa wote Gereza la Mahabusu Keko akikabiliwa na kesi namba CC9/2014 Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Samora, tarehe ambayo Polisi wanadai yalifanyika mauaji hayo.
Mh. Rais, mshitakiwa aliingia gerezani tarehe 16/01/2014 mpaka tarehe 19/05/2014 alipopata dhamana, na kwa mujibu wa hati ya mashitaka inaonyesha mauaji yalifanyika tarehe 7/04/2014.
Mbaya zaidi, hata hayo majina ya mshitakiwa mwenzangu si sahihi, kwani wameyatoa (wameyatunga) wao Polisi, jina lake halisi ni Isack Frank Mwakatobe. Na si kama lile jina waliloandika Polisi katika hati ya mashitaka.
Mh. Rais, hata tarehe ambazo wanadai mtu huyo aliuawa, pamoja na RB namba zake kutofautiana; moja inaonyesha alifariki dunia tarehe 6/07/2014 na nyingine tarehe 7/04/2014, jina lake ni Erick Msaki wa maeneo ya Mbezi Beach, Kilongawima.
Sasa Mh. Rais, kwa hali ya kawaida, inawezekana vipi mtu mmoja akafariki dunia mara mbili? Haya yote yanatokana na Polisi kushindwa kufanya mahojiano na washitakiwa, ndiyo maana wameshindwa kutoa taarifa sahihi zinazotuhusu sisi washitakiwa.
Kuanzia majina mpaka tarehe ya tukio washitakiwa walikuwa wapi? Ukweli ni kwamba sisi washitakiwa wote wawili hatukuwahi kuhojiwa kuhusu tuhuma zinazotukabili hadi sasa.
Mh. Rais, ili kuthibitisha majina sahihi ya mshitakiwa kama alikuwapo Gereza la Keko siku ya tukio, tarehe 19/12/2016 mshitakiwa (Mwakatobe) alihukumiwa kifungo kwa shitaka hilo hilo na kupelekwa Gereza la Ukonga.
Kwa taratibu za Magereza, iwapo mfungwa mpya anaingia gerezani hupigwa picha, kupimwa urefu na kuchukuliwa alama za vidole. Mshitakiwa huyo kwa sasa yupo Gereza la Mahabusu Segerea, akikabiliwa na tuhuma hii hii.
Mama Rais Samia, kama utapenda kutuma maofisa wako wakafanye naye mahojiano, watamkuta huko. Kwa hiyo tunakuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vyombo vinavyohusika na uonevu kama huu, kuunda Tume ya Uchunguzi dhidi ya mashitaka haya yanayotukabili hadi sasa tukiendelea kuteseka gerezani kwa miaka saba. Hii itakuwa fundisho kwa askari wachache wanaolichafua Jeshi la Polisi Tanzania.
Mama Rais Samia, huyo askari hufanya huo ubambikizwaji wa kesi hasa kwa watu wenye kesi zenye dhamana kisheria ili kuwawekea mfumo wa kesi nyingine wasidhaminike.
Pia hizo kesi anazobambikia watu yeye mwenyewe ndiye huziandikia maelezo ya awali ya mshitaki, pamoja na kujaza fomu ya utambuzi wa mshitakiwa bila utambuzi huo kufanyika. Mambo yote hayo huyafanya bila kumhusisha mtuhumiwa wa kesi husika; pamoja na kujisainisha hizo karatasi mwenyewe.
Ila kama Tume (ikiundwa) itafanya uchunguzi, alama za vidole za washitakiwa zitamuumbua kwa sababu sio za washitakiwa husika.
Askari huyu pia amekuwa akiwatumia walinzi shirikishi kwenda mahakamani kutoa ushahidi wa uongo. Mbaya zaidi, hao shirikishi anaowatumia wanafahamika; wanatoka Manzese Tip Top, majina yao ni (anataja majina matatu; yanahifadhiwa) hawa watu hupatiwa pesa na huyo askari kisha huenda mahakamani kuwatolea watu ushahidi wa uongo.
Pindi wafikapo mahakamani kutoa ushahidi, mtuhumiwa ana haki ya kuwauliza vitambulisho mashahidi hao, ili kuthibitisha na kufananisha majina halisi ya mlalamikaji (wa awali) aliyekwenda kupeleka malalamiko Polisi siku ya kwanza ya tukio.
Hawa (walinzi shirikishi) hukataa kuonyesha vitambulisho, wakisema hawana kitambulisho chochote!
Askari huyu anapokosa mashahidi wake wa uongo, huziondoa hizo kesi zenye muda mrefu mahakamani, kisha huzirudisha tena muda huo huo hapo mahakamani zionekane kuwa ni kesi mpya; za mwaka huo. Kumbe kesi hizo zina miaka mitano hadi saba.
Mfano, kesi yangu ni ya mwaka 2014 lakini sasa inaonekana kuwa ni ya mwaka 2018! Zipo kesi nyingi sana za aina hiyo hapa Dar es Salaam.
Mh. Rais, nimelalamika sehemu mbalimbali dhidi ya tuhuma hizi; kuanzia Ofisi ya Tume ya Malalamiko Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia barua yenye kumbukumbu namba 78/Dar/3/XVII/78 ya tarehe 31-12-2018 na wao kunijibu kwa barua yenye kumbukumbu namba GA102/362/01‘A’/36 ya tarehe 20-5-2019, wakinitaka kuwa na subira kwani suala langu wanalifuatilia.
Nikawaandikia tena kupitia barua yenye kumbukumbu namba 78/Dar/3/XVIII ya tarehe 8 -7 -2019 pamoja na kuambatanisha na vielelezo vyangu, lakini mpaka leo sijapata majibu yoyote.
Pia nilimwandikia barua Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) yenye kumbukumbu namba 78/Dar/5/Z/100 ya tarehe 19/7/2016 na kuambatanisha na vielelezo vyangu, lakini bila mafanikio hadi leo.
Ndiyo maana ninakuomba Mh. Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala hili pamoja na vyombo husika kuwashughulikia baadhi ya askari wanaolichafua Jeshi la Polisi kwa masilahi binafsi.
Sisi mahabusu tunazifuatilia sana hotuba zako na utendaji wa kazi kupitia magazeti, radio na televisheni. Tunaona jinsi unavyopenda haki itendeke makazini na kuondoa uonevu kwa wananchi.
Sisi mahubusu na wafungwa wote wa Tanzania ni wafuatiliaji wakubwa wa hotuba zako, kwani wewe ndiye kiongozi wetu na Mama yetu.
Mungu akuongoze katika serikali yako pamoja na viongozi wengine wanaotenda haki kama wewe. Mungu awabariki sana; Amina.
Mh. Rais ninakuomba sana, tena sana, unilinde dhidi ya hawa watu niliowaweka wazi kwako kwani bado wana nguvu kubwa serikalini. Bado wana nafasi ya kunidhuru.
Huyo askari pia amekuwa akibambikia watu kesi nyingine za aina ‘robbery’ (unyang’anyi) ambazo hazina dhamana. Hizo ndizo nyingi sana, hazina idadi. Ukitembelea Gereza la Segerea na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni utajionea mwenyewe!
Kesi anazobambikia watu amezipachika majina yake. Kwa mfano, kesi ya robbery huiita DUDE na ya mauaji huiita KUBWA.
Tunawashukuru sana ndugu zetu wa vyombo vya habari Tanzania, hasa Gazeti la JAMHURI na vyombo vingine, kwani huwa tunasoma habari na kusikiliza, kuangalia kupitia TV zetu magazeti yetu mwenendo mzima wa serikali, hasa hotuba za Mama yetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pongezi nyingi sana kwa Gazeti la JAMHURI kwa kutenda haki na kutoa habari zote bila ubaguzi. Mungu awabariki sana uongozi mzima wa gazeti hili na mafanikio mema.