WAJUMBE wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Taifa wamempitisha Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Rais wa Tanzania, kuwania nafasi hiyo kwa muhula mwingine katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Pia mkutano huo umempitisha Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi kuwa mgombea urais kwa chama hicho kwa upande wa Zanzibar katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Awali akisoma hotuba ya mapendekezo hayo, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM, ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema rai ya wajumbe waliotoa ya kumpendekeza Rais Samia na Dk Mwinyi kuteuliwa kuwania urais kupitia chama hicho haipingwi kwa kuwa kila chama kina utaratibu wake.
Amesema rai ya wajumbe ni rai ya chama hicho hivyo kilichobaki ni utaratibu wa kisheria wa Tume Huru ya Taifa Uchaguzi kuwateua.
“Kama tunataka tuamue leo kwamba Samia ndiyo mgombea wetu na Dk Mwinyi ndiyo mgombea wetu mamlaka hayo tunayo.“Sasa kama tunaamua hivyo ndiyo tumeamua, sasa kinachobaki ni ushauri, wale wanajua taratibu za kisheria, taratibu za hiki, lakini watu wote watajua kwamba CCM kwenye uteuzi wagombea ishamaliza,” amesema Kikwete. Mkutano huo wa CCM unamalizika leo.