Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 25 ya Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA).

Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu ya ‘Kusherehekea Utofauti na Mshikamano katika usawa wa Jinsia’ yatafanyika Januari 19 hadi 23, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 19, 2024 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TAWJA na Jaji Mahakama ya Rufani, Barke Sehel amesema maadhimisho hayo yatakusanya wadau mbalimbali wakiwemo wanachama wa TAWJA, washirika wa Kimataifa, wawakilishi wa Serikali, mashirika ya kiraia, Balozi, Taasisi pamoja na Taasisi za kifedha.

“Maadhimisho ya Miaka 25 yanasherehekea mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika maeneo hayo. Inasherehekea michango ya TAWJA katika usawa wa kijinsia ndani ya mfumo wa Mahakama na juhudi zake za kuboresha haki za wanawake na makundi dhaifu.

“Hadi sasa, mafanikio ya TAWJA yanatufanya tuzingatie maendeleo yaliyofikiwa na kazi endelevu inahitajika ili kuendeleza mfumo wa kisheria wenye usawa na unaojumuisha wote,” amesema.

Akizungumzia miaka 25 ya Chama hicho, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo, Sophia Wambura amesema katika kipindi hicho TAWJA imefanikiwa kukuza hali ya usawa kwenye ngazi ya utendaji wa Mahakama.

“Vilevile tumehamasisha usawa kwenye jamii katika kuijengea uwezo kutambua haki zao katika mirathi, talaka na haki za usawa na masuala mengine ya kijamii,” amesema.

Hata hivyo Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Arusha na mwenyekiti wa kamati mwenyeji ya maandalizi ya maadhimisho hayo, Aisha Bade amesema bado kuna changamoto za dhamana.

Amesema pamoja na kwamba dhamana zinakua wazi lakini wahusika wanashidwa kutimiza masharti ya dhamana kwa kukosa baadhi ya mahitaji kama mdhamini na vitambulisho, jambo ambalo katika maadhimisho hayo pia watatoa elimu hiyo.