Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa yamekamilika katika eneo la Mtumba jijini Dodoma huku Serikali ikitoa maelekezo kwa mikoa yote nchini kufanya maadhimisho hayo kwa kufanya usafi, upandaji miti na shughuli nyingine za kijamii.
Hatua hiyo ni baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza kujengwa eneo la kumbukumbu lenye hadhi ya Makao Makuu kutokana na umuhimu wa siku hiyo badala ya kuendelea kulitumia eneo la mashujaa Jamatini Jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maadhimisho hayo leo Julai 24,2023 Jijini hapa,Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Jenister Mhagama amesema hayo ni maelekezo ya Serikali na kwamba maadhimisho hayo yanafanyika kitaifa Jijini hapo.
Amesema katika kumbukumbu hiyo ya kuwaenzi Mashujaa waliojitoa kupigania haki ya watanzania,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ataweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi wa eneo hilo .
“Tunampongeza sana Rais Samia kwa maono ya kujenga mnara huu kwa hadhi ya makao makuu hi I’mi inadhihirisha namna anavyowaezi Mashujaa na kulinda historia na hazina ya taifa jambo ambalo ni urithi mkubwa wa taifa,”amesema
Amesema siku hiyo ni muhimu kwa sababu inawakumbusha watanzania Kwa ujumla kuhusu wajibu wao wa kutunza historia ya Mashujaa waliopigania, kutetea na kulinda Uhuru wa nchi ikiwa ni pamoja na kuitunza na kuihifadhi vema ili kurithisha vizazi vijavyo.
“Ni mumuhimu watanzania kutumia historia hii kukuza na kuendeleza amani na mshikamano wa kitaifa,historia hii inatupa deni kwetu la kuutafsiri na kuutumia ujasiri wa Mashujaa wetu kufanya maamuzi ya kiujasiri yanayojielekeza katika kuleta mageuzi ya kiuchumi ili kizazi cha sasa na kijacho kifaidike na vitendo vya kijasiri vilivyofanywa na Mashujaa hao,”amesema
Hata hivyo Waziri huyo amefafanua kuwa ujenzi wa mnara uliopo ambao utatumika kesho ni wa muda na kwamba ujenzi wa mnara wa kudumu wa kishujaa unaendelea kujengwa kwa awamu katika eneo hilo hilo.
“Wizara zetu mbili ya Ulinzi na Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma tumeshirikiana mpaka kukamilisha hili kwa ujumla maandalizi yamekamilika,”ameeleza Waziri Mhagama.
Kwa upande wake Waziri wa ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Wizara yake imejiandaa vizuri kwa gwaride maalumu na kutumia nafasi hiyo kuwaalika wanachi kwenda kushuhudia maadhimisho hayo.
“Niwaombe Wanahabari, Viongozi wa Wizara, Taasisi, Idara zinazojitegemea, Wakala ya Serikali, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Kimila na Viongozi wa Vyama vyote vya Siasa kuwahimiza Wananchi, Watumishi wa Sekta ya Umma na Binafsi, Waumuni na Wanachama wa Vyama vya Siasa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Maadhimisho haya,”amesema
Pamoja na mambo mengine,shughuli za Mashujaa zitatanguliwa na uwashaji wa Mwenge wa Mashujaa saa 6:00 Usiku leo 24 Julai, 2023 kuamkia tarehe 25 Julai 202 ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amepewa heshima ya kuuwasha Mwenge huo wa Mashujaa kwa niaba ya Watanzania na Mwenge huo utazimwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma tarehe 25 julai 2023 saa 6:00 Usiku.