Rais Dk Samia Suluhu Hassan anatarajia kuondoka nchini leo Oktoba 29 kuelekea Des Moines, lowa, nchini Marekani kuhudhuria Mjadala wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug ulioandaliwa na Taasisi ya Worl Prize Foundation ya nchi hiyo.
Mjadala huo hufanyika kila mwaka na kuhudhuriwa na viongozi, wataalamu, watu mashuhuri, watunga sera, hususan za kilimo, lishe na usimamizi wa rasilimali.
Shabaha ya majadiliano hayo ni kutafuta suluhu ya changamoto ya upatikanaji wa chakula duniani, ambayo inachochewa na mabadiliko ya tabianchi.
Rais Dk Samia ni miongoni mwa Marais wanne kutoka Afrika, waliopewa heshima ya kushiriki na kuchangia kwenye mjadala huo wenye kaulimbiu: “Mbegu za Fursa: Kuunganisha Vizazi na Kustawisha Diplomasia”(Secds of Opportunity: Bridging Generations and Cultivating Diplomacy).
Viongozi wengine watakaoshiriki ni kutoka Sierra Leone, Madagascar na Nigeria.
Mbali na Mjadala huo, Rais Dk Samia pia atashiriki hafla ya utoaji tuzo ya World Food Prize kwa mwaka 2024 kwa watu wenye mchango mkubwa katika sekta ya kilimo, ikiwa ni mwendelezo wa kumuenzi Hayati Dk Norman E. Borlaug aliyehamasisha usalama wa chakula duniani kwa watu wote.
Sambamba na kushiriki kwenye majadiliano hayo, Rais Dk Samia atakutana na kufanya mazungumzo (round tables discussion) na viongozi kutoka Serikali na sekta binafsi ya Marekani, hususan waliopo kwenye sekta ya kilimo.
Lengo la mazungumzo hayo ni kujadili uwekezaji katika sekta hiyo na kuongeza mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo ambayo ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini.