Na Deodatus Balile
Wiki iliyopita ilikuwa na matukio mengi, ila nitayagusia makubwa machache. Kwanza nianze la kesho Jumatano, Machi 9, 2022 ambapo Jukwaa la Wahariri Tanzania litakuwa linafanya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 2022.
Huu mkutano utahusisha wahariri zaidi ya 150. Kwa mara ya kwanza tutapata wahariri kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zimbabwe na Malawi. Mgeni rasmi ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi. Vituo kadhaa vya televisheni vimetuunga mkono na vitarusha ‘live’ mkutano huu. Ni siku muhimu kwa wahariri.
Sitanii, baada ya utangulizi huo, nichukue fursa hii kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu, kwa kuamua kumfutia mashitaka Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe. Hatua hii ya Rais Samia imeendelea kutekeleza kauli yake kwa vitendo ya kuwataka Watanzania kuponya majeraha.
Mbowe anayo majeraha mengi. Ukiacha kushindwa ubunge katika mazingira ya kutatanisha, ambapo aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Hai kabla ya uchaguzi alimwambia kuwa hawezi kushinda, Awamu ya Tano anayo mengi ya kusimulia.
Shamba lake la mboga za majani wilayani Hai mipira ya umwagiliaji maji ilikatwakatwa na aliyekuwa mkuu wa wilaya, kwa madai kuwa amelima karibu na chanzo cha maji.
Mashamba yake mkoani Morogoro nayo yakapata zahama. Jengo la Bilcanas kulipokuwa na Night Club ya Bilcanas likavunjwa, vifaa vyake vya muziki, viti, meza na vinywaji vilivyokuwamo hadi leo haijulikani vilipo. Amekaa rumande miezi minane kwa kesi ya ‘kubumba’. Nikiri, namfahamu Mbowe angalau kwa miaka 20 sasa.
Sitanii, Mbowe ni kiongozi msikivu. Si mtu wa mabavu au shari. Ndiyo maana pamoja na kukaa rumande miezi minane, bado amekwenda Ikulu kuonana na Rais Samia na akatamka kuwa kuna kila sababu ya kufanya siasa za kistaarabu. Wala hakuanza leo kuonyesha uungwana wake. Mtakumbuka mwaka 2020 katika uchaguzi ulipotokea mtifuano kati ya Chadema na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), nilimwita Mbowe, nikamwita Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk. Ayub Rioba na nikamwomba Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Charles Mahela, awepo, tukakaa, tukazungumza, tukayamaliza. TBC na Chadema wakaendelea kushirikiana.
Mbowe angekuwa sawa na baadhi ya wanasiasa nisiotaka kuwataja hapa, ambao wakikorofishana na wabunge anawaambia Out… Out… Out…, wala asingekubali kukaa meza ya mazungumzo na TBC au asingetoka rumande alikokaa miezi minane hadi akafikisha umri wa miaka 60 akiwa rumande, lakini bado akakubali kwenda Ikulu kukutana na Rais na bado akatoa kauli ya kiungwana kuhamasisha Watanzania kufanya siasa za kistaarabu.
Sitanii, wakati unamsifia mtu kwa mbio, ni vema pia usisahau kumsifia aliyekuwa akifukuzana naye. Wakati nikisifia uungwana wa Mbowe, hapa tusisahau uungwana wa aina yake wa Rais Samia. Rais Samia alisema anataka kuifungua nchi. Alipata kutoa kauli ya kuomba aachwe ajenge nchi kwanza, watu hawakumwelewa. Kwa vyovyote iwavyo, naamini sasa wengi wanamwelewa.
Tanzania ilikuwa kisiwani katika suala la corona, ameifungua nchi. Uhuru wa vyombo vya habari ulikuwa kitanzini, Februari 10, 2022 ameyafungulia magazeti ya Mwanahalisi, Mseto, Tanzania Daima na Mawio.
Baada ya kumaliza hayo, lilibaki kubwa la Mbowe kuwa gerezani kutokana na kesi ‘iliyoumbwa’ miaka miwili iliyopita, kabla Rais Samia hajaingia madarakani. Sasa nalo amelimaliza.
Najua yapo mengine mawili ambayo Rais Samia ameishaanza kuyapatia ufumbuzi. Mikutano ya hadhara na Katiba Mpya. Hili ameliundia kikosi kazi. Ni matumaini yangu kuwa mwendo anaokwenda nao Rais Samia wa kutatua tatizo moja baada ya jingine, Tanzania itarudi katika nafasi yake kikanda na kimataifa. Nchi zote zinazotuzunguka, zamani ziliiona Tanzania kama msuluhishi, ila siku za karibuni tumeshuhudia mifarakano ya kisiasa isiyomithirika. Tumetoka huko wala tusirudi.
Sitanii, nilipooandika makala za kumwomba Rais Samia kumwachia huru Mbowe, nilisema kuna masalia ya waoneaji wasiofurahishwa na hatua anazozichukua Rais Samia za kuwapa watu haki. Kama nilivyotegemea genge la ‘makuwadi’ wa uonevu likamtuma kijana asiye na maadili kuniandika kwa lugha chafu kwenye mitandao ya kijamii, akidhani ningejibu mapigo. Kijana huyo tulimfukuza uanachama katika Jukwaa la Wahariri Tanzania kutokana na tabia zake za ‘uyoyoni’ na vitendo vya rushwa. Kuniita mimi chawa, anatafuta pa kuinulia jina lake, nami sitampa nafasi hiyo, nimeamua sitamjibu.
Nafasi inazidi kuwa finyu. Wakati nikimpongeza Rais Samia kwa kumwachia huru Mbowe, sitatenda haki nisipogusia hili la vita ya Urusi na Ukraine. Hapa mtu unahitaji kuwa refarii huru tu, wala hutakiwi kutumia nguvu kuthibitisha nani anaonewa katika mgogoro huu. Marekani imepigana vita zaidi ya nchi 40 tangu mwaka 1945, haijawahi kufungiwa na FIFA wala kuwekewa vikwazo.
Urusi mara kadhaa imeomba kuwa ilikwisha kuvunja Warsaw Pact, ila ikaomba ipewe uanachama kwenye NATO, kwa pamoja washirikiane kuongeza usalama wa dunia. Marekani haitaki.
Wakati Marekani wanataka kujenga mitambo ya kijeshi jirani na Urusi kwa maana ya nchini Ukraine, wanasahau kuwa Ukraine ilikuwa sehemu ya Urusi hadi mwaka 1991. Rais Vladimir Putin amehoji iwapo Urusi inaweza kuanzisha uhusiano wa kijeshi na Mexico au Canada na Marekani wakaendelea kuwa na amani, hawajajibu swali hili.
Nafasi imekuwa finyu, naendelea kufuatilia kwa karibu vita ya Urusi na Ukraine na siku za usoni nitaendelea kuandika ukweli kuhusu kinachoendelea. Asante Rais Samia kufungulia magazeti na kumwachia huru Mbowe. Mungu ibariki Tanzania.