Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dodoma
Haijapata kutokea. Haya ni maneno aliyopenda kuyatumia aliyekuwa Mbunge wa Ulanga Magharibi (CCM), Theodos James Kasapira. Nikiri nilipopewa mwaliko wa kuja hapa Dodoma kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, niliifahamu ajenda moja ya msingi ya kumpata Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara.
Sitanii, ratiba ilikwenda kama ilivyopangwa hadi Jumapili ya Januari 19, 2025 pale Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, alipotoa hoja ya kumtaka Rais Samia Suluhu Hassan atoke kwenye kikao ili Mkutano Mkuu Maalumu umjadili na umtendee jambo. Rais Samia alijibu hoja hiyo kuwa ndiye mwenyekiti, anapaswa kusimamia mkutano mwanzo hadi mwisho.
Baada ya kauli hiyo ya Rais Samia, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa, yeye alipasua yai. Akasema Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM ufanye uamuzi, kwamba Rais Samia ndiye awe mgombea pekee wa urais kwa tiketi ya CCM. Ukumbi ukalipuka kwa shangwe. Rais (mstaafu), Jakaya Kikwete, alibaini kuwa Rais Samia amepigwa butwaa katika hoja hii ambayo ilishangiliwa kwa nguvu kubwa.
Sitanii, kutokana na ukongwe na uzoefu, Kikwete akapendekeza kuwa sasa badala ya kila mtu kusema tu, basi lipitishwe azimio kwamba Dk. Samia ndiye mgombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Katika mazingira hayo, Mwenyekiti wa CCM mbaye ni Rais Samia, akaagiza sekretarieti iandae azimio, lisomwe, kisha lipitishwe na wajumbe.
Ni katika hatua hiyo mambo yalianza kwenda kama upepo wa kisulisuli. Sekretarieti iliandaa azimio ikalileta, likapitishwa. Lakini azimio hilo likaja na azimio la pili kwamba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, naye apitishwe kuwa mgombea wa CCM Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Katika hatua hiyo, Mwenyekiti akaagiza Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM ikutane kujadili azimio hilo. Lakini pia kama lilivyo takwa la kikatiba, ikabidi Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar ikae na kupendekeza iwapo Dk. Mwinyi ndiye awe mgombea pekee kwa Zanzibar au la. Kamati Maalumu ikampendekeza Dk. Mwinyi, na NEC ikapitisha jina lake, maana kikatiba mgombea urais wa Zanzibar anapitishwa na NEC.
Viongozi waliporejea ukumbini, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, akapewe jukumu la kutoa mwelekeo. Kabla ya hatua hiyo, Mwenyekiti wa CCM, Dk. Samia, akasema anafahamu kuwa Dk. Nchimbi angesema wanakwenda katika kupiga kura za kumchagua kuwa mgombea wa CCM kwa mwaka 2025, hivyo anapaswa kuacha kikao mikononi mwa Mwenyekiti wa muda, binafsi akasema anamkabidhi Dk. Mwinyi uenyekiti.
Sitanii, mambo yakaenda kasi kweli kweli. Zikapigwa kura. Kura zote 1,924, hakuna iliyoharibika au hakuna iliyosema hapana. Rais Samia akapata kura zote asilimia 100. Ikumbukwe hapo wajumbe wa Mkutano Mkuu wametengua kanuni. Si Rais Samia, wala Dk. Mwinyi aliyechukua fomu kuomba uteuzi kama ulivyo utaratibu wa siku zote.
Baada ya Rais Samia kuwa ameteuliwa, akasema kama zilivyo taratibu na kanuni za CCM, inabidi apatikane Mgombea Mwenza. Kama sinema vile, Kamati Kuu ya CCM ikakutana kwa muda. Baada ya dakika 22, huku wajumbe wakifurahia ushindi wa Simba wa magoli mawili kwa bila dhidi ya Constantine, likaja tangazo la Mgombea Mwenza. Mara tukatangaziwa kuwa ni “kijana wetu, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.”
Shangwe zikawa kuu. Nimesema haijapata kutokea. Kwanza, utaratibu wa kumpata mgombea kwa njia ya azimio ni mara ya kwanza CCM kuutumia kupata wagombea wake. Lakini pili, CCM haijapata kuteua mgombea na mgombea mweza karibu mwaka mmoja kabla ya tarehe ya uchaguzi. Mkutano wa Uteuzi huwa unakuwa mwezi Julai, lakini zamu hii umefanyika miezi sita kabla – Januari.
Jambo kuu nililoliona, utaratibu uliotumika umezima fursa za misuguano na mpasuko ndani ya CCM. Nafahamu kuwa bado hata ungefuatwa utaratibu wa kawaida wa kuchukua fomu, kuomba wadhamini katika mikoa angalau 10 ikiwamo miwili ya Zanzibar, bado Rais Samia angeibuka kidedea ndani ya CCM, lakini wakati mchakato huo unaendelea pengine wangejitokeza wa kujitoa mhanga.
Kadiri mchakato ambavyo ungetumia muda mrefu ndani ya chama, ndivyo gharama zingeongezeka, lakini na lile kundi lenye roho ya “kwa nini” lingepata nafasi ya kupenyeza habari japo kwenye mitandoa ya kijamii.
Kimsingi kwa utaratibu huu, hili kundi limepigwa na kitu kizito. Katika makala zijazo nitaandika kwa kina juu ya kwa nini Rais Samia anastahili, ila leo itoshe kusema hatua ya kwanza ambayo ni kubwa na ya msingi ameipiga. Ameteuliwa kuwa mgombea urais.
Sitanii, CCM imeingia katika kumbukumbu za dunia kuwa chama tawala cha kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kusimamisha mgombea mwanamke. Nafahamu vyama vya upinzani vimepata kusimamisha wagombea wanawake, lakini si vyama tawala. Nikuume sikio tu Rais Samia kuwa uteuzi wa Dk. Nchimbi umelamba dume. Anakifahamu chama na anaifahamu nchi.
Nafahamu mzee Stephen Wassira amekuwa Makamu Mwenyekiti. Cheche zake amezianza siku ya kwanza tu alipochaguliwa akasema tunaridhiana kama nchi na si mtu mmoja mmoja.
Dk. Nchimbi akifunga ‘busta’ za mtandao wake kwa vijana na wazee wa nchi hii, yeyote anayejipanga kushindana na timu hii Oktoba 2025 ajiandae vilivyo, maana wawili hawa, Dk. Samia na Dk. Nchimbi watafagia kama upepo wa kisulisuli. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404827