Na Wislon Malima, JAMHURI MEDIA Lusaka Zambia


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema wataendelea na dhamira ya kubadilisha Bomba la Mafuta lililopo la Tanzania-Zambia (TAZAMA) na kujenga bomba jipya la gesi asilia kutoka Dar es Salaam hadi Zambia.

Aidha amesema kwa kutambua haja ya kuhakikisha usalama wa nishati na usambazaji wa umeme wa kutosha viwandani, Serikali itaendelea na jitihada za kuunganisha Bwawa la Nishati ya Kusini mwa Afrika na Bwawa la Umeme la Mashariki.

Rais Samia ameyasema hayo leo Oktoba 24, 2023 Ikulu ya Zambia katika maadhimisho ya miaka 59 ya uhuru wa taifa hilo ambapo akiwa katika muendelezo wa ziara yake ya siku tatu ambayo inatarajiwa kumalizika kesho Oktoba 25, 2023.

“Tunapotazama mbele, napenda kusisitiza dhamira ya Tanzania ya kuimarisha uhusiano uliopo wa ushirikiano na urafiki kati ya mataifa yetu mawili. Kufikia lengo hili, maono yetu ya pamoja ya Waafrika wenye mafanikio, amani na umoja yanasalia kuwa kanuni yetu inayoongoza.” amesema.

Mbali na hiyo, Rais Samia amesema tayari wameanza uboreshaji wa mitambo ya Bandari ya Dar es Salaam ili kuhakikisha bandari hiyo inafanya kazi kwa ufanisi, wakati na bila vikwazo katika shughuli zake kutokana na hivyo ameitaka jumuiya ya wafanyabiashara nchini Zambia kuchangamkia fursa hiyo ya kipekee.

Pia Rais Samia amesema tayari Serikali imefanya uamuzi wa kutenga eneo la ardhi hekta 20 katika Bandari Kavu ya Kwala mkoani Pwani kwa ajili ya mizigo inayopelekwa Zambia ambapo Zambia itawezeshwa kwa muda mrefu zaidi wa kuhifadhi bila malipo ambao unaenda hadi siku 45.

“Hatua hii itapunguza msongamano na ucheleweshaji, na hatimaye kupunguza gharama za kufanya biashara nchini Zambia. Kwa hivyo, tunatazamia kwamba hatua hii itakuza zaidi biashara kati ya nchi zetu mbili na kuunda fursa zaidi za kibiashara kwa Watu wetu wawili. Hii ni zawadi kutoka Tanzania unaposherehekea uhuru wako.” Amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema Serikali hizo mbili zitaendelea kuweka mazingira mazuri ili kuhakikisha kunakuwepo na usafirishaji huru wa bidhaa na watu.

“Kwetu sisi mipaka ya kijiografia itabaki tu kama mistari ya kiutawala kati ya watu wawili ambayo haiwezi kutenganishwa kwa sababu ya historia yao ya pamoja, jiografia, undugu wa damu, makabila na utamaduni.” amesema.

Kutokana na hivyo, Rais Samia amemnukuu Rais wa Zamani wa Marekani John F. Kennedy ambaye alisema, “Jiografia imetufanya majirani. Historia imetufanya kuwa marafiki. Uchumi umetufanya washirika, na ulazima umetufanya washirika. Wale ambao Mungu amewaunganisha pamoja, mtu asiwatenganishe.”

Rais Samia aliwahakikishia wananchi wa Zambia kwamba, Tanzania itabaki kuwa mwanafamilia, rafiki wa kutegemewa na mshirika wa kimkakati kama ilivyokuwa wakati wa harakati za ukombozi wa kisiasa ambapo wataendelea kuwa marafiki kwa misimu yote na kukamilishana katika harakati za kubadilisha uchumi wa nchi hizo mbili.

“Waanzilishi wetu waliweza, dhidi ya matatizo yote, kuanzisha tangu mwanzo mojawapo ya njia kuu za kiuchumi kuwahi kujengwa katika Afrika baada ya uhuru.” amesema.

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Zambia, Hakainde Hichilema amesema, wanasherehekea siku ya uhuru wa nchi hiyo huku wakiwa na mikakati ya kuwekeza katika elimu pamoja na kuweka nguvu kwa vijana na wanawake.

Pia ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuimarisha na kuendeleza undugu wa damu ulioanzishwa na waasisi wa nchi hizo mbili ambapo watahakikisha wataleta usawa wa kiuchumi na kijamii katika ugawaji sawa wa rasilimali za nchi