Na Mwandishi Wetu Zanzibar

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amezishauri Balozi za Tanzania zinazoiwakilisha nchi kimataifa kuona haja ya kuanzisha vituo vya kutoa elimu juu ya utamaduni wa mswahili ili kukikuza na kukieneza Kiswahili Kimataifa.

Dk. Samia pia amezipongeza Balozi za Tanzania nchini Korea ya kusini, Cuba, Falme za kiarabu, Uhalozi, Ufaransa, Zambia, Zimbabwe, Nigeria na Sudan, kwa ubunifu wao wa kuanzisha vituo vya kufundishia utamaduni na lugha ya Kiswahili ikiwa ni jitihada za kukieneza Kiswahili nje ya nchi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi alitoa rai hiyo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, aliyemuwakilisha kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kiswahili duniani, katika ukumbi wa Polisi Ziwani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema, Kiswahili ni lugha ya kwanza Afrika kupewa heshima kimataifa kwa kuwekewa siku yake kuadhimishwa kimataifa na kuongeza kuwa ni fahari kubwa kwa Tanzania na nchi za ukanda wa Afrika Mashariki ambako ni chimbuko la lugha ya Kiswahili.

Rais Dk. Mwinyi alisifu jitihada za Ubalozi wa Tanzania nchini Korea Kusini kwa kuanzisha kituo kinachotoa mafunzo ya utamaduni wa Mswahili unaohusisha vyakula, ngoma, mavazi na lugha ya Kiswahili na kuzitaka balozi nyengine za Tanzania kuiga mfano huo kwa kuitumia vema fursa waliyonayo kukieneza Kiswahili duniani kote.

“Balozi zetu zote zione haja ya kuanzisha vituo vya lugha ya Kiswahili na utamaduni wake kwa lengo la kuitangaza na kuieneza lugha hii nje ya nchi yetu” ameshauri Rais Dk. Mwinyi.

Pia, Dk. Mwinyi alieleza kufanyika kwa shehehe hizo Kimataifa ni njia moja ya kutoa hamasa ya kukitambulisha na kuieneza Kiswahili kimataifa pamoja na kuhamasisha matumizi sahihi ya lugha hiyo duniani.

Dk. Mwinyi, alieleza matumaini yake ya kufunguka fursa nyingi zaidi za lugha ya Kiswahili na matarajio yake kwa walimu wa Kiswahili nchini kupata fursa ya kufundisha kwenye vituo vya balozi za Tanzania nje ya nchi.

“Nina matumaini fursa sasa zitafunguka zaidi ili walimu wetu wapate fursa zaidi za mahitaji ya walimu kwenye balozi zetu nje ya nchi, natoa rai kwa pande zote za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania zishirikiane kikamilifu kutoa mafunzo hayo nje ya nchi na suala hili liratibiwe vizuri ili walimu wengi wanufaike na fursa hizo” alishauri Rais Dk. Mwinyi.

Aidha, alisifu mbinu wanazozitumia Watanzania wanaoishi nje ya nchi kwa kutumia vyema fursa walizonazo kukifundisha Kiswahili kupitia balozi za Tanzania nje ya nchi.

Aidha, Dk. Mwinyi aliiasa jamii ya watanzania kujitahidi kuzifuatilia na kuzitumia fursa za Kiswahili zilizomo ndani na nje ya nchi kwani mahitaji ya lugha hiyo yanaendelea kuongezeka kila siku duniani.

Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kiswahili duniani kilikua na kauli mbiu, “Kiswahili chetu, Umoja wetu”