Na Edward Kondela, JamhuriMedia, Tanga
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua nchi kiuchumi zimesaidia uwepo wa miradi mbalimbali ikiwemo ya kuwasaidia wafugaji.
Prof. Shemdoe amebainisha hayo juzi wakati alipokuwa akifungua rasmi mafunzo ya ufugaji bora kwa baadhi ya wafugaji wa ng’ombe wa maziwa wa Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga katika Kampasi ya Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Buhuri mjini Tanga, ambapo amesema ni wakati kwa wafugaji kutumia fursa hizo kujikwamua kiuchumi.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanayofadhiliwa na ubalozi wa nchi ya Ireland hapa nchini, kupitia mradi wa Maziwa Faida yanatoa pia fursa kwa vijana kupata elimu ya ufugaji bora kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji na vijana wenyewe kujiingiza kwenye ufugaji kibiashara.
Aidha, amesema kutokana na changamoto za uwepo wa ajira nchini, vijana wanaweza kutumia fursa ya ufugaji kujiajiri na kufuga kisasa kwa ajili ya kulenga masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa LITA Dkt. Pius Mwambene, amesema hii ni awamu ya tatu kwa mafunzo ya wafugaji 288 ambapo lengo ni kufikia wafugaji 3,000 katiika kipindi cha miaka mitatu ijayo na kuwaasa wafugaji kuwa makini na mafunzo hayo.
Amebainisha kuwa mafunzo kwa wafugaji yanalenga kushirikiana kutatua changamoto zilizopo kwa kutafuta suluhu ya pamoja na kutoa ushauri kwa serikali namna ambavyo wanaweza kufuga kwa tija.
Pia, Dkt. Mwambene amefafanua kuwa ufugaji unapaswa kubadilika badala ya kuwa na ufugaji wa kujikimu wa kupata maziwa kidogo na kuwa na ufugaji wa kibiashara kwa kupata maziwa mengi na kuchangia upatikanaji wa malighafi ya maziwa kwa ajili ya viwanda vilivyopo nchini.
Ameongeza kuwa uwepo wa viwanda vya kuchakata maziwa nchini kikiwemo cha Tanga Fresh, viwe chachu ya kuwa deni kwa wafugaji kuhakikisha wanasamabaza maziwa ya kutosha kwa viwanda hivyo ambapo yote yanawezekana kwa kuwa na ufugaji wa ng’ombe kwa njia ya kisasa, hivyo kutumia fursa ya mafunzo hayo kujijengea uwezo zaidi.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Kanda ya Mashariki Dkt. Zabron Nziku ambaye ni Mratibu Mkuu wa mradi wa Maziwa Faida akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa baadhi ya wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kutoka Wilaya ya Muheza amesema mradi huo wa miaka mitano wenye thamani ya Shilingi Bilioni 8 unalenga kuboresha mnyororo wa thamani ya maziwa nchini.
Dkt. Nziku ameongeza kuwa mradi huo unatekelezwa na TALIRI kwa kushirikiana na taasisi ya nchini Ireland iitwayo Teagasc pamoja na wadau mbalimbali kikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambacho kimekuwa kikitoa mafunzo kwa watafiti wa TALIRI na wakufunzi wa LITA pamoja na viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa Wilaya ya Muheza.
Pia, amesema mradi huo umewezesha kununuliwa kwa vifaa mbalimbali pamoja na ukarabati wa miundombinu kwa ajili ya kuwezesha kukuza Sekta ya Mifugo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kubadilisha wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kufuga kwa tija na kujiongeea kipato.
Akizungumza kwa niaba ya wafugaji wenzake wa ng’ombe wa maziwa kutoka Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga Bw. Mwijuma Mohammed Ramadhan amezishukuru serikali za Tanzania na Ireland kwa kuwezesha kuwepo kwa mradi wa Maziwa Faida ambapo unaleta chachu ya maendeleo kwa wafugaji hao.
Amesema kupitia mradi huo wafugaji wataweza kupata fursa ya kutatua changamoto zinazowakabili na kufikia malengo ya kufuga kisasa ili kupata matokeo chanya ya kupata maziwa mengi zaidi na hatimaye kuuza kwenye viwanda vya kuchakata maziwa.
Katika, hatua nyingine Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe baada ya kufungua rasmi mafunzo kwa wafugaji hao alipata fursa ya kuwatembelea na kuzungumza na vijana waliopo kwenye Programu ya Kielelezo ya Jenga Kesho iliyo bora (BBT – LIFE) waliopo LITA Kampasi ya Buhuri – Tanga na kuwapongeza kwa kuwa kituo kilichofanya vizuri zaidi katika programu hiyo awamu ya kwanza.
Amewataka vijana hao kuendelea kupata elimu zaidi juu ya unenepeshaji wa mifugo hususan ng’ombe na kufuga kibiashara ili watakapomaliza programu hiyo waweze kujiendeleza na kuwafundisha wengine namna ya ufugaji bora.
Baadhi ya vijana hao wameishukuru serikali kwa namna ambavyo imewapatia ajira kwa njia ya kuwapatia mafunzo ya unenepeshaji wa ng’ombe ambapo wanasema lengo lao ni kujiajiri kwenye Sekta ya Mifugo kwa kufuga kisasa na kutoa elimu kwa wafugaji wengine ambao bado wanafuga kienyeji.