Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa nchini kutumia mikutano ya hadhara kutoa hoja na fikra zenye tija zinazolenga kuimarisha utendaji serikalini.
Rais Samia ametoa wito huo leo wakati akifungua mkutano wa Baraza Maalum la Vyama vya Siasa kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).
Aidha, Rais Samia amevitaka vyama vya siasa kutumia mikutano ya hadhara kujitangaza ili kukua kisiasa na kuutumia uhuru wa kujieleza kutoa mawazo mbadala yatakayoendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Rais Samia pia amesema uhuru wa kutoa maoni kusisababishe kudhalilisha watu wengine, kuibua hisia za kidini, ukabila au kubaguana kwa misingi yoyote ile.
Vile vile, Rais Samia amesisitiza kutumia uhuru huo vizuri bila kuingilia haki na uhuru wa watu wengine pamoja na kufuata sheria, kanuni na taratibu.
Kwa upande mwingine, Rais Samia ametoa wito kwa viongozi wa dini kwenye maeneo yao kuisaidia serikali kurejesha maadili mema katika jamii.
Hali kadhalika, Rais Samia amesema kumekuwepo na mmomonyoko wa maadili, udhalilishaji na ukatili wa kijinsia katika jamii ambapo vijana hufanya matendo yaliyo kinyume na mila na desturi za Kitanzania.