Na Tatu Saad,JamhuriMedia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amevunja Bodi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kufanya utenguzi katika shirika la ndege za serikali.

Rais Samia amemtengua mhandisi John Nzulule kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA).

Vilevile Rais Samia ametoa maelekezo kwa Katibu Mkuu Kiongozi katika kuhakikisha Makatibu Wakuu na Watendaji wote wa taasisi za Serikali wanaipitia kwa kina Taasisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kujibu na kuzifanyia kazi kwa haraka hoja zote zinazogusa maeneo yao.

Katika hatua nyingine Rais Samia ameelekeza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa watendaji watakaobainika kuhusika na uzembe au ubadhirifu.

Ripoti ya CAG iliwasilishwa bungeni jijini Dodoma Alhamisi, Aprili 6, 2023 ikihusisha madudu lukuki yaliyofanywa na taasisi za umma.

Katika hotuba yake wakati akipokea ripoti hiyo, Rais Samia alikemea vikali watendaji wasio waadilifu, akisisitiza walioshindwa wampishe.