Na Mwandishi Wetu, JAMHURI MEDIA, Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amevunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zuhura Yunus leo Novemba 09, 2023 imeeleza kuwa bodi hiyo ilivunjwa kuanzia tarehe 07 Novemba, 2023.
Sambamba na hilo Rais Samia amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali akiwemo Mkurugenzi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC).
Amemteua Balozi James Gilawa Bwana kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Afrika kusini. Balozi Bwana anachukua nafasi ya Balozi Meja Jenerali Gaudence Salim Milanzi ambaye amestaafu.
Rais Samia amemteua Balozi Said Hussein Massoro kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Kuwait.
Balozi Massoro anachukua nafasi ya Balozi Said Shaib Mussa ambaye aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Amemteua Kaimu Abdi Mkeyenge kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC). Kabla ya uteuzi huu Mkeyenge alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC). Mkeyenge anachukua nafasi ya Dkt. Elirehema Doriye ambaye atapangiwa kazi nyingine.