Na Deodatus Balile, Rio de Janeiro, Brazil
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa hotuba ya kihistoria kwa kuuliza maswali magumu katika mkutano wa G20, ambapo akiwa anasikilizwa na Rais wa Marekani, Joe Biden, Rais wa China, Xi Jimping, Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer na viongozi wakuu wa nchi hizo 20 tajiri, ametaka dunia kukataa umaskini ulitopea, kumaliza janga la njaa, kuipa Afrika nafasi, kuweka usawa katika upatikanaji wa fedha za maendeleo na kubwa zaidi, amewasilisha ombi la nchi zinazoendelea kufutiwa madeni.
“Natoa shukrani zangu kwa Rais Lula da Silva [wa Brazil] kwa mwaliko na kwa ukarimu wa hali ya juu. Leo hii, tunajikuta katika dunia yenye utajiri mkubwa, lakini bado Afrika inakabiliwa na viwango visivyovumilika vya umasikini, njaa, magonjwa, utapiamlo, na uzalishaji hafifu. Dunia ambamo idadi kubwa ya vijana inakumbwa na changamoto zilizoambatana na migogoro na sera za kimataifa zinazoongeza uhaba wa chakula, kuzorotesha ushindani, na kupunguza fursa za kufikia masoko na teknolojia inayohitajika.
“Dunia ambayo wengi bado wanasubiri ahadi ya utandawazi ya ustawi itimie, huku wakiendelea kuwa na matumaini kwamba mageuzi ya utawala wa kimataifa yatawaletea uwakilishi wa haki na upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika kutokomeza umasikini. Hata hivyo, tukiacha dunia kama ilivyo, swali tutakalouliza mwaka 2030 halitakuwa ‘tulikosa kufikia SDGs kwa kiasi gani,’ bali ‘ni watu wangapi zaidi dunia imewaacha nyuma.’
Baada ya kuwaeleza ukweli huo mchungu, Rais Samia akaongeza: “Waheshimiwa, tunaamini kuwa dunia yenye usawa, haki, na endelevu itapatikana pale nchi zinazoendelea kama yangu zitakapopata msaada, rasilimali, na uwakilishi unaohitajika ili kuendesha maendeleo endelevu.
“Licha ya vikwazo vilivyopo, Tanzania imefanikiwa kufanya mageuzi makubwa ya kisera na kitaasisi pamoja na uwekezaji mahsusi ili kubadilisha mifumo yetu ya kilimo na chakula. Kwa kuwa 61.5% ya nguvu kazi yetu ipo kwenye sekta ya kilimo, juhudi zetu zimeongeza kiwango cha ukuaji wa sekta hiyo hadi 4.2%, zimefikisha kiwango cha kujitosheleza kwa chakula hadi 128%, na zimepunguza viwango vya umasikini hadi 26.4% mnamo mwaka 2023.
“Pamoja na mafanikio haya, changamoto bado zipo, zikiwemo uhaba wa mashine, mbolea na utafiti na maendeleo (R&D). Tunaamini kuwa kwa msaada mahsusi, tunaweza kutumia uvumbuzi kwa ufanisi zaidi, kujenga ustahimilivu, na kuwezesha ukuaji wa maana na jumuishi.”
Sitanii, Rais Samia akagusa mfumo wa uchumi duniani: “Maombi yangu mahsusi kwa G20 ni kugawa upya Haki za Kuweka Akiba (SDRs) kwa Taasisi za Kifedha za Afrika kama vile Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Pamoja na haja ya mfumo wa usawa wa mgao katika muundo wa sasa wa kifedha wa kimataifa, Tanzania inatoa wito wa kuwepo kwa mifumo zaidi ya msamaha wa madeni, misaada, na mikopo yenye masharti nafuu inayoshughulikia mahitaji yetu na udhaifu wetu.”
Haki za Kuweka Akiba ni mfumo ulioanziswa na Shiria la Fedha Duniani ( IMF) mwaka 1969 amba unatambua rasilimali au mali zenye thamani kubwa ambazo uwekwa kama dhamana na kupewa mikopo kwa bei nafuu. Nchi nyingi duniani zilikuwa zinaweka dhahabu kama dhamana na hivyo vinakopesheka kwa riba ndogo, lakini miaka ya karibuni nchi tajiri zimetambua sarafu tano duniani ambazo zinatambulika badala ya dhahabu. Sarafu hizo ni dola za Marekani, Yen ya Japan, Pauni ya Uingereza Ero ya Ulaya na Renminbi ya China.
Sitanii, ingawa dhahabu si fedha inayoweza kununua kitu, ikitambuliwa kama rasilimali yenye thamani kubwa, Tanzania na nchi nyingine zenye madini ya aina hiyo, zinaweza kupewa mikopo yenye kiwango kidogo ca riba za asilimia 2. Hoja hii ikikubaliwa, ni wazi itazikomboa nchi zinazoendelea kwani zinatumia sehemu kubwa ya makusanyo ya kodi zao kwa ajili ya kulipa madeni, ambayo kiwango kikubwa cha madeni kinatokana na riba.
Rais Samia ameunga mkono ushirikiano ulioimarishwa kama vile Muungano wa Kimataifa wa G20 Dhidi ya Njaa na Umasikini ili kuchochea uvumbuzi na ukuaji jumuishi. “Mkutano huu unadhihirisha dhamira yetu ya pamoja ya kutoiacha dunia kama ilivyo. Tunapaswa kuongeza juhudi zetu na kufufua ahadi zetu za kujenga dunia yenye usawa, ustawi, na haki,” amesema.
Sitanii, mkutano huu wa G20 umempa Rais Samia fursa ya kupiga hatua nyingine katika juhudi zake za kiufungua Tanzania kidiplomasia na kukuza uchumi wa taifa letu. Dunia imezidi kumpa heshima Rais Samia na sasa amekuwa Rais wa kwanza kutoka Tanzania kushiriki mkutano wa mataifa 20 yenye uchumi mkubwa duniani,hapa de Jenairo, Brazil.
Takwimu zinazotolewa na taasisi mbalimbali duniani zinaonyesha kwa sasa uchumi wa dunia una thamani ya dola trilioni 110. Kiuhalisia uchumi wa dunia unashikiliwa na nchi 10 ambazo zinachangia asilimia 76 ya pato la dunia na zinashikilia zaidi ya asilimia 50 ya biashara zinazofanyika duniani. Nchi maskini ikiwamo Tanzania zinashikilia asilimia 8 tu ya biashara ya dunia.
Wanachama wa G20 ni nchi 19 na Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU). Ukubwa wa uchumi wa nchi hizi (GDP) kwa mwaka 2024, kwa thamani ya dola za Marekani kwa trilioni (trn), ni kama ifuatavyo:
Marekani (26.7), China (19.37), Ujerumani (4.72), India (4.47), Japan (4.4), Uingereza (3.07), Ufaransa (2.78), Urusi (2.24), Canada (2.14), Italia (2.01), Brazil (1.92), Australia (1.68), Korea Kusini (1.67), Mexico (1.41), Indonesia (1.31), Saudi Arabia (1.1), Uturuki (0.91), Argentina (0.63), Afrika Kusini (0.4). Umoja wa Ulaya unakisiwa kwa ujumla wake kuwa na uchumi wenye thamani ya dola trilioni 16. Afrika takwimu hazitolewi.
Sitanii, mkutano wa G20 ni jukwaa linalojumuisha nchi zilizo na uchumi mkubwa duniani, una faida kubwa kwa Tanzania inaposhiriki kama mwalikwa. Tanzania inapata fursa ya kushiriki mijadala ya kimataifa inayohusu uchumi, maendeleo, biashara na changamoto za dunia kama mabadiliko ya tabianchi na usalama wa chakula.
Kwa ushiriki huu, Rais Samia anaimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na mataifa yenye ushawishi mkubwa duniani. Hii itavutia wawekezaji wakubwa na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kiteknolojia. Wataalamu wanasema Tanzania itatumia fursa hii kuvutia uwekezaji kwenye miradi ya kimkakati kama kilimo, miundombinu na nishati mbadala.
Kupitia ushiriki huu Tanzania inapata nafasi ya kushawishi ajenda za kikanda na kimataifa zinazoendana na masilahi yake. Kwa mfano, moja ya ajenda inazolenga kupenyezwa ni umuhimu wa usaidizi wa kifedha kwa nchi zinazoendelea, kwa maana ya kupata mikopo yenye masharti nafuu kwa nchi zinazoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na inalenga kuhimiza biashara yenye usawa kwa bidhaa za kilimo na maliasili.
Ushiriki huu unaipa Tanzania nafasi ya kujifunza mbinu bora za kuwaletea wananchi maendeleo kwa kujifunza nchi wanachama wa G20 zilifanikiwaje, ikiwa ni pamoja na sera za kiuchumi na teknolojia za kisasa. Pia inatoa jukwaa la kuonyesha mafanikio yake na kuvutia washirika wa maendeleo.
Kwa kushiriki kama mwalikwa, Tanzania inaongeza nafasi yake ya kushiriki zaidi kwenye uamuzi wa kimataifa, hivyo kuboresha ushawishi wake katika masuala yanayoathiri dunia. Ushiriki huu ni hatua muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kidiplomasia ya Tanzania.
Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda, amewaambia wahariri waliopo hapa Rio de Jenairo kuwa mkutano huu unafanyika kwa siku mbili ambazo ni Novemba 18 na 19, mwaka huu.
Tanzania ni moja ya nchi zilizoalikwa na Mwenyekiti wa mhula unaokwisha, Rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva. Nchi nyingine 18 zikiwamo Misri, Nigeria, Angola na Msumbiji zimealikwa pia. Hii ni mara ya kwanza katika historia ya G20 kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kualikwa.
Kabla ya G20 kulikuwapo na G8 iliyoasisiwa mwaka 1999, ambayo hadi 2008 ilikuwa na wanachama wanane. Mwaka 2005 aliyekuwa Rais, kwa sasa hayati Benjamin William Mkapa, alishiriki mkutano wa G8 na mwaka 2008, aliyekuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete naye alishiriki. Baada ya hapo zilipoongezeka kuwa G20, ushiriki wa Tanzania ulikoma.
Sitanii, pia Rais Samia anakuwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kupata fursa ya kushiriki mkutano wa G20. Mkutano huu umetanguliwa na mikutano ya ngazi ya mawaziri, iliyoanza kufanyika tangu Desemba mwaka jana.
Kaulimbiu ya mkutano huu ni kujenga “Dunia yenye haki, usawa na maendeleo endelevu.” Mkutano wa G 20 una vipaumbele vitatu, ambavyo ni:
- Ushirikishwaji wa jamii katika mapambano dhidi ya njaa na umaskini (usalama wa chakula).
- Mabadiliko ya nishati sambamba na kukuza maendeleo endelevu katika nyanja za uchumi, jamii na mazingira.
- Mageuzi ya mifumo ya kiutawala katika taasisi za kimataifa.
Sitanii, vipaumbele hivi vinaakisi kaulimbiu ya mkutano huu, kuondoa umaskini uliokithiri katika Bara la Afrika, ambako zaidi ya watu milioni 600 hawana nishati ya umeme.
Pia zaidi ya watu milioni 950 Afrika wanatumia nishati isiyo safi kupikia, kwa maana ya kuni, mkaa, kinyesi cha mifugo na nyingine zenye athari kwenye mazingira, uchumi na maendeleo, kwani wanatumia muda mwingi kutafuta kuni.
Sitanii, ikumbukwe Rais Samia ndiye kinara wa kuhamasisha Nishati Safi ya Kupikia barani Afrika. Lengo ni kuondoa umaskini na kupunguza madhira kwa kina mama wanaotumia muda mwingi kutafuta kuni na wengine kuishia kubakwa wanapokuwa maporini.
Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 inalenga kuondoa umaskini na njaa kwa kujenga viwanda. Dira ya Taifa 2050 inaendelea kubeba ajenda nzima ya kumaliza njaa.
Mkutano huu una fursa za uwekezaji, mitaji, kuwapo sauti katika ngazi ya kimataifa kuhamasisha sera zinazosaidia nchi za ulimwengu wa tatu katika kufikia malengo ya kuendeleza watu wake.
Balozi Kaganda anasema ushiriki wa Rais Samia haujatokea kwa bahati mbaya, bali umetokana na kushamiri kwa diplomasia ya Tanzania.
“Kwa sasa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imeendelea kupokea mialiko mingi sana, ambapo Rais ameshiriki michanche, mingine amewatuma wasaidizi wake akiwamo Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango, Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko. Hii inaashiria kuimarika na kupaa kwa diplomasia ya nchi,” anasema Balozi Kaganda na kuongeza:
“Amekuwa Rais mwenye mvuto, hivyo kuwezesha viongozi wenzake kushiriki. Tanzania inacho cha kuchangia. Tumejipambanua kwenye eneo la nishati, kuzuia njaa, kudai usawa na kuongeza sauti katika mifumo ya utawala – Mfuko wa Fedha wa Kimataifa, Benki ya Dunia, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa… sauti ya Tanzania imekuwa ikisikika. Anachokifanya kinaendana na falsafa yake ya 4R, ambazo ni maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya. Hilo ndilo analifanya Rais Samia kimataifa.”
Balozi Kaganda anaamini Rais Samia atatumia mkutano huu kuhamasisha ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia. Mwakani Januari kutakuwa na mkutano wa marais wa Afrika unaoandaliwa na Benki ya Dunia juu ya Nishati Safi ya Kupikia na Tanzania imepewa heshima ya kuandaa mkutano huu.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye madini ya kimkakati ambayo yanatumika kutengeneza betri za simu na magari, ambazo zitaendesha mitambo na magari, hivyo kuwa mbadala wa mafuta yanayotokana na Kisukusi (fossils) yanayochafua mazingira. Ipo Nikel pale Kabanga, Ngara, na kwa sasa nchi inayo gesi ya kutosha inayoweza kuzalisha LNG.
Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa kwenye kilimo, miundombinu na teknolojia zinazoongeza tija na thamani katika eneo hilo la kilimo. Tanzania imefikia asilimia 128 katika uwezo wa kulisha watu wake chakula, hivyo kwa sasa iwekeze katika lishe. Mkutano huu ni mwendelezo wa alama kubwa ambayo Tanzania inaendeleza sasa kwenye anga za diplomasia.
Katika ziara hii, pia Rais wa Tanzania anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake Rais wa Brazil, Lula, ambapo watajadili maeneo ya ushirikiano na Brazil kwa maendeleo ya Watanzania.
Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kwa jinsi wananchi walivyofikiwa umeme vijijini na dunia nzima inataka kujifunza Wakala wa Umeme Vijijini (REA) umewezaje kufanya kazi hii kwa ufanisi mkubwa kiasi hiki.
Mwakani kiti cha G20 kinahamia nchini Afrika Kusini, hali inayoaminiwa kuwa Afrika itakuwa na sauti kubwa zaidi. Brazil inatarajiwa kuwasilisha Azimio la Usalama wa Chakula ambapo Tanzania imesema italiunga mkono azimio hili na Uingereza inataka kuanzisha ushirika wa nishati duniani (Global Power Alliance), suala ambalo Balozi Kaganda amesema Tanzania italiunga mkono pia.
0784404827