Na Wilson Malima
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Shahada ya juu heshima ya udaktari katika fasihi ‘Doctor of Letters. Honoris Causa ‘ ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika mahafali ya 52 duru ya tano leo Novemba 30, 2022.
Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam Dkt. Jakaya Kikwete amemtunuku shahada hiyo ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuleta maendeleo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya miundombinu, jamii na utu.
Akihutubia katika mahafali hayo mara baada ya kutunukiwa heshima hiyo Rais Samia ameeleza nia na majaribio yake ya kuitafuta Shahada ya Uzamivu ya kuwa hakufanikiwa kwani muda haukuwa rafiki kwake kutokana majukumu mengi aliyonayo.
“Ndugu zangu siku chache zilizopita Makamu Mkuu wa chuo aliniandikia barua kunifahamisha uamuzi wa Baraza la Chuo la Seneti kunitunuku shahada ya heshima ya udaktari wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, nilikubali kwa moyo mkunjufu kwa kutambua kuwa heshima hiyo yangu peke yangu bali pia ni ya Watanzania walionipa dhamana kuwa kiongozi mkuu wa nchi.”
“Lakini nilijiuliza maswali kadhaa sababu huko nyuma nilijaribu kuitafuta shahada hii lakini muda haukunipa nafasi” amesema Rais Samia .
Amesema maeneo manne aliyoyasimia kama falsafa yake katika kujenga jamii iliyobora yenye haki na usawa
“Katika mpango wangu nikakaa na dhana ya R4 ambazo ni Reconciliation, Resilience, Reforms na Rebuilding of our nation au kwa maana nyingine maridhiano, ustahamilivu, mabadiliko na kujenga upya Taifa letu kwa mtirirko wake dhana hii inagusa maeneo yote ya maisha ya Mtanzania na binadamu kwa ujumla na pengine ndio wasifu ulioelezwa ukagusia mengi katika maeneo mbalimbali niliyoweza kuchangia hadi tulipofikia.
“Nilikuwa naamini kabisa kuwa maendeleo hayawezi kuja bila wananchi kuungana na taifa kuwa kitu kimoja tunaweza kutofautiana mitazamo lakini sote ni Watanzania wenye lengo moja la maendeleo ya nchi yetu.
“Nimekuwa nikiamini kabisa kuwa kila kitu kikizidi kiwango huwa na kasoro na hivyo nikaona madhara ya kuzigeuza siasa kuwa kila kitu ikiwa ni pamoja na kuzifanya siasa kuwa njia za uchumi hivyo nikahisi kuja na mambo haya manne na nikiyafanyia kazi vizuri pamoja na wasaidizi wangu tutaweza kulirudisha taifa kuwa moja na wote tutaweza kujenga nchi yetu kwa ushirikiano.” amesema.
Aidha Rais Samia ameeleza suala la haki na usawa katika jamiii na kubainisha kwamba maendeleo ya jamii si vyema aina ya watu tu ndiyo wanapaswa kushiriki na wengine kubaki nyuma .
“Maenedeleo ninayoyasema hapa huletwa na watu katika umajumui wao hivyo si vyema kufanya aina ya watu tu ndio washiriki kwenye maendeleo wengine wabaki nyuma. Lakini pia kama Ibara ya 12 kifungu kidogo cha kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyosema ” binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa” nimekuwa nikipigania usawa wa kijinsia pia.” amesema.
Rais Samia anakuwa miongoni mwa watu mashuhuri na viongozi mbalimbali kutunukiwa shahada ya juu ya heshima lakini pia kuungana na jopo la wasomi waliopita katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam akiwemo aliyekuwa Rais wa Dkt. Congo Hayati Joseph Kabila Rais Yowel Kaguta Museveni wa Uganda na wengine wengi.
Shahada ya juu ya Heshima ‘Honoris Causa’ ni heshima ambayo hutolewa kwa mtu aliyefanya jambo kubwa lenye tija na mchango mkubwa katika jamii na miongoni mwa viongozi ambo wamewahi kutunukiwa shahada hiyo ni pamoja na Hayati Dkt.John Magufuli, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete naye Dkt. Pius Msekwa.