Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Adam Kighoma Malima kutokana na vifo vya watu wawili katika ajali ya ndege.
Ajali hiyo imetokea katika kiwanja cha ndege cha Matambwe kwenye Hifadhi ya Taifa ya Nyerere mkoani humo na kusababisha vifo vya watu wawili na majeruhi wawili.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,ndege aina ya Cessina 192 5H-FZS ikiwa na abiria watatu (3) na rubani 1 ilipata ajali wakati ikiruka katika kiwanja hicho.
Katika ajali hiyo askari wawili wamejeruhiwa na hali zao sio nzuri ambapo baada ya kuokolewa walikimbizwa zahanati kwa ajili ya kupata huduma ya kwanza huku wakisubiri ndege ya kuwapeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.
Aidha, miili ya marehemu imehifadhiwa kwa muda katika zahanati ya hifadhi hiyo.
Rais Samia anawapa pole wafiwa wote na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Waliofariki ni Rubani mstaafu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bernard Shayo kutoka FZS na Amani Mgogolo huku Theonas Nota ambaye alikuwa Askari Mhifadhi amefikwa na mauti baada ya ndege iliyokuwa ikimkimbiza hospitali kutua Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wakati ndege hiyo ikiruka kwenda katika doria ikiwa na abiria watatu na rubani mmoja.
Majeruhi ni Evanda Elisha, askari wa uhifadhi wa Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa) ambaye amejeruhiwa na anaendelea na matibabu.