Na Mbaraka Kambona,JamhuriMedia,Pwani
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuboresha maisha ya Watanzania hususan vijana kwa kuwawekea mazingira wezeshi ya kujiajiri kupitia shughuli za uvuvi na ukuzaji viumbe maji ili kukuza kipato chao na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamefahamika wakati wa hafla fupi ya kuzindua programu ya mafunzo atamizi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji kwa vijana iliyofanyika Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani mwiahoni mwa wiki.
Akiongea wakati akizindua programu hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Mashimba Ndaki alisema kuwa Rais, Dkt. Samia amedhamiria kuwawezesha vijana kujiajiri na ndio maana katika mwaka huu wa fedha wa 2022/23 ameridhia kutengwa fedha ili vijana 500 waweze kupatiwa mafunzo atamizi ili waweze kujiajiri.
“Mwaka huu tumepanga kuwawezesha vijana 500, awamu hii ya kwanza tumeanza na vijana 200 halafu watafuatiwa na vijana wengine 300, hii programu ni endelevu na mwakani tutaendelea kutenga bajeti, lengo ni kutengeneza vijana watakaokuwa jasiri kukabiliana na mazingira yanayowazunguka”,amesema Ndaki
Ameongeza kwa kusema kuwa programu hiyo inasimamiwa na Wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu kwa lengo la kutimiza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha vijana wanaondokana na changamoto ya ajira nchini.
Naye, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Sekta ya Uvuvi), Dkt. Nazael Madalla alisema kuwa mafunzo hayo ambayo yatagharamiwa na Serilali yatawawezesha vijana kuongeza maarifa na mbinu mbadala za uvuvi na ukuzaji viumbe maji, kupata elimu ya ujasiriamali, namna bora ya kupata mitaji na mikopo kupitia taasisi za kifedha, namna ya kuanzisha na kusajili kampuni na elimu ya kutunza na kusimamia rasilimali fedha.
Ameongeza kwa kusema kuwa vijana hao watapatiwa mafunzo kwa vitendo kwa muda wa miezi mitatu (3) katika vituo 16 vilivyoainishwa na serikali, ambavyo ni FETA Mikindani- Mtwara, BERTHA AQUA SOLUTION FISH FARM-Ukerewe, DR. CHARLES TIZEBA- Nyamagana na EDEN-Chanika Dar.
Vituo vingine ni GEORGE RUCHO/ TAFIRI-Sota – Rorya, JKT BULAMBA- Bunda, JOHN KASENGENYA FISH FARM- Ukerewe na JWTZ MAKOKO-Musoma.
Mafunzo hayo pia yatafanyika katika vituo vya KONGA AGRIBUSINESS-Magu, MECKY FISH FARM- Sengerema, MOHAMED LIBUBURU- Chato, MPANJU FISH FARM- Nyamagana, PETER SAMWEL MWERA – Rorya, SHARIFU RAJABU MWEMA-Magu, TANLAPIA-Bagamoyo na VICTORIA MMARI – Sengerema.
Kwa upande wa wanufaika wa programu hiyo, Theofik Wilson na Miriam Donald walimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutenga fedha ili vijana waweze kupatiwa mafunzo hayo huku wakisema kuwa hatua hiyo itasaidia sana vijana kubadili fikra zao na kufanya shughuli za kujiajiri wao wenyewe na kutekeleza miradi mbalimbali itakayosaidia kuwaongezea kipato chao na Taifa kwa ujumla.