Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ruvuma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 7.2 kupitia mradi wa BOOST kujenga shule 12 mpya za msingi na miundombinu mbalimbali katika shule 44 mkoani Ruvuma.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema fedha hizo zimetolewa katika mwaka wa fedha za 2022/2023 na kwamba kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi bilioni 4.34 zimetumika kujenga shule mpya.
Amebainisha kuwa ujenzi wa shule hizo mpya umehusisha ujenzi wa madarasa ya msingi 98,madarasa ya elimu ya awali ya mfano 24,matundu ya vyoo ya elimu ya msingi 136 na matundu ya vyoo ya elimu ya awali 72.
Miundombinu mingine katika shule hizo ameitaja kuwa ni matundu ya vyoo vya walimu 24,vichomea taka 12 na majengo ya utawala 12.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa zaidi ya shilingi bilioni 2.9 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ambayo inahusisha madarasa ya msingi 87,matundu ya vyoo ya msingi 114,madarasa ya elimu ya awali 16,matundu ya vyoo vya awali 48 na nyumba za walimu mbili.
Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Ruvuma Mwl.Edith Mpinzile amesema Mkoa umepokea shilingi milioni 264 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya walimu 12 katika Halmashauri zote nane za Mkoa.
“Mkoa pia umepokea shilingi bilioni 1.56 kupitia mradi wa SWASH kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo 607 katika shule za msingi 47 na ujenzi upo katika hatua mbalimbali”,alisema Mpinzile.
Akizungumzia elimu maalum,elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi,Afisa Elimu huyo Mkoa amesema hadi kufikia Novemba 2022,Mkoa ulikuwa na vituo 109 katika shule za msingi vinavyotekeleza mpango wa Elimu ya msingi kwa Watoto walioikosa (MEMKWA).
Amesema Mkoa wa Ruvuma hivi sasa una vituo 302 katika shule za msingi na sekondari vyenye Watoto wenye mahitaji maalum.
Hata hivyo amesema idadi ya Wanafunzi wasiojua KKK kwa darasa la kwanza na la pili imeendelea kupungua kutoka wanafunzi 7,427 mwezi Juni 2023 hadi kufikia 6,188 mwezi Desemba 2023 ikiwa ni sawa na asilimia 16.6.
Ameitaja mikakati ya kuinua elimu na kuongeza taaluma kuwa ni kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mtaala wa elimu katika ngazi za Halmashauri na shule,kuhimiza utoaji motisha kwa wanafunzi na walimu katika shule zinazofanya vizuri kwenye taaluma na kuhimiza wananchi utoaji chakula kwa wanafunzi wawapo shuleni.
Naye Mwalimu Mkuu shule mpya ya Msingi Nahange iliyojengwa kupitia mradi wa BOOST iliyopo Kata ya Suluti wilayani Namtumbo Mwl. Nahale Ponera amesema serikali imetoa shilingi milioni 331.6 kujenga shule hiyo ambayo imeanza tangu
Amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 529 wanaosoma katika vyumba tisa kuanzia awali hadi darasa la saba ambapo wanamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kutoa fedha za kujenga shule hiyo inayovutia wanafunzi kutokana kuwa na miundombinu ya kisasa.
Shaban Nyahale ni Mwanafunzi shule mpya ya msingi Mzalendo iliyopo Kata ya Masuguru wilayani Namtumbo amesema anamshukuru Rais Samia kwa kuwajengea shule yenye mazingira rafiki kwa kusomea.