Serikali inatarajia kuanza kutekeleza ujenzi wa mradi wa maji wa miji 28 katika mji wa Songea mkoani Ruvuma unaogharimu shilingi bilioni 145.7.
Hayo yamesemwa Machi 10,2023 na Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Aweso ambaye amewakilishwa na Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Marypriska Mahundi katika hafla ya utiaji Saini mkataba wa ujenzi wa mradi huo kati ya serikali na Mkandarasi, Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation.
“Mkataba wa ujenzi wa mradi huo ni wa miezi 32 kuanzia Machi 10,2023,kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa maji wa miji 28 katika mji wa Songea kutaleta manufaa makubwa ikiwemo SOUWASA kuongeza uwezo wa kuzalisha maji kutoka lita milioni 11.58 kwa siku hadi kufikia lita milioni 42.581 kwa siku,” amesema Aweso.
Amesema mradi huo unakwenda kumaliza kero ya maji katika Manispaa ya Songea kwa sababu upatikanaji wa maji utakuwa uhakika na kwamba mradi una uwezo wa kuwahudumia wananchi wapatao 440,794.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba akizungumza kabla ya kusainiwa mkataba huo amesema mradi huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi wa Songea hadi mwaka 2045, ambapo idadi ya wakazi manispaa ya Songea inatarajiwa kuwa zaidi ya 400,000.
Amezitaja kazi ambazo zinatafanyika kwenye mradi huo ni ujenzi wa bwawa lenye uwezo wa kujaza maji lita milioni 4.8,ujenzi wa mtambo wa kuchuja maji lita milioni 16 kwa siku,ujenzi wa matanki ya maji lita milioni tisa,kulaza mabomba yenye urefu wa kilometa 10.5 yatakayosafirisha maji kutoka kwenye mabwawa hadi kwenye matanki.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara maji. Amesema katika utekelezaji wa mradi huo kutakuwa usambazaji wa maji wenye urefu wa kilometa zaidi laki nane.
“Serikali imeamua kutekeleza mradi wa maji miji 28 kwa kuangalia maeneo ambayo huduma ya maji haijawafikia wananchi ipasavyo,usanifu wa mradi huu unafanyika kwa miezi sita’’,alisisitiza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) Mhandisi Patrick Kibasa amesema hivi sasa SOUWASA ina jumla ya vyanzo vya maji 13 vyenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 11.58 kwa siku ikiwa ni sawa na uzalishaji wa asilimia 57 ambapo mahitaji halisi ya maji kwa wananchi wapatao 286,285 kulingana na sensa ya watu ya mwaka 2022 ni lita milioni 20.336 kwa siku.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kuwa wananchi wa Ruvuma wanakuwa sehemu ya kupata huduma ya maji safi na salama.
Kanali Thomas amesema Mkoa wa Ruvuma umepiga hatua kubwa katika utoaji huduma ya maji safi na salama ambapo hadi sasa utoaji huduma ya maji mijini umefikia asilimia 80.95 ambapo katika Halmashuri ya Manispaa ya Songea umefikia zaidi ya asilimia 90 na utoaji wa maji mjini Songea ni saa 22 kwa siku.
Hata hivyo amesema upatikanaji wa maji vijijini mkoani Ruvuma,kati ya vijiji 525 vilivyopo mkoani Ruvuma.vijiji 355 vinapata maji safi na salama sawana asilimia 67.
Naye Mbunge wa Songea mjini ambaye pia ni Waziri wa Sheria na Katiba Dkt.Damas Ndumbaro ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha hizo zinazotokana na mapato ya ndani ili kutekeleza mradi huo mkubwa wa maji.
Dkt.Ndumbaro amesema kutekelezwa kwa mradi huo kunakwenda kumaliza kero ya maji katika mitaa yote 95 na kata zote 21 zilizopo Manispaa ya Songea ambapo amemuomba Mkandarasi wa mradi huo kumaliza kazi ndani ya mkataba.
SOUWASA ni miongoni mwa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanzania Bara iliyoanzishwa mwaka 1997.